DC SONGEA ATOA BAISKELI KWA WALEMAVU | Tarimo Blog




Na Muhidin Amri, Songea

MKUU wa wilaya ya Songea mkoani Ruvuma  Pololet Mgema ,amewataka vijana wilayani humo kuhakikisha wanajiunga katika vikundi ili iwe rahisi kwa Serikali kupitia Halmashauri za wilaya kuwapa mikopo  isiyo na riba ambayo itawawezesha kuanzisha vikundi vya kiuchumi  na kujikwamua na umaskini.

Mgema ameyasema hayo jana wakati akikabidhi msaada wa baiskeli ya magurudumu matatu na fedha shilingi laki moja kwa mkazi  wa mtaa wa Bombambili manispaa ya Songea Frowin Fungo ambaye ni mlemavu wa miguu
anayejishuhulisha kushona na kung’arisha viatu  katika kituo cha
mabasi cha Mfaranyaki Manispaa ya Songea.

Amesema kuwa, Fungo amefika ofisi ya mkuu wa Wilaya mara tatu  kuomba
fedha ili aongeze  mtaji wake, kwa hiyo aliwasilina na wadau kwa ajili
ya kupata baiskeli ambayo itamsaidia kwenda na kurudi katika shughuli
zake za kila siku.

Kwa mujibu wa mkuu wa Wilaya, Fungo amepata msaada wa baiskeli na
fedha hizo kutokana na yeye mwenyewe kuanza kuchukua hatua  na
kuanzisha shughuli ambayo ina muingizia kipato kinachomsaidia
kuendesha maisha yake licha ya ulemavu alionao badala ya kukaa
barabarani na kuomba omba kwa wapita njia.

Amesema, kama walemavu na vijana wakiungana pamoja itakuwa rahisi kwa
Halmashauri kuwapa mikopo ambayo inarejeshwa kwa kipindi cha muda wa
miaka mmoja tena bila riba yoyote.

Mbali na Fungo, pia mkuu wa Wilaya amemkabidhi mkazi wa kijiji cha
Mpitimbi  ambaye pia ni mlemavu wa miguu anayejishughulisha na kilimo
Aron Ponera, mwenye mke na watoto watano baiskeli ili iweze kumsaidia
kwenda shambani na kurudi nyumbani badala ya kutambaa kwa magoti

Ameeleza, suala la ulemavu halimpi haki mtu kuwa omba omba, kwa hiyo
walemavu ni kama sehemu ya jamii ni lazima wawe wabunifu kwa kuanzisha
miradi midogo ya kiuchumi ambayo mbali na kuwaingizia kipato pia
itawaondolea aibu ya kudharauliwa  na jamii.

"Watu wenye ulemavu wana uwezo wa kufanya kazi na hivyo
ulemavuo sio kizuizi cha kufanya kazi kama ilivyo kwa Ponera ndiyo
maana serikali na wadau wengine wakaona ni vema kumsaidia baiskeli ili
iweze kumsaidia katika safari zake za kimaisha."Amesema.

Pia mkuu wa wilaya amehaidi kumsaidia mbolea kwa ajili ya shughuli
zake za kilimo ili aweze kuzalisha kwa wingi mazao  yatakayomsaidia
yeye na familia yake  kama chakula na  kiasi kingine kuuza ili aweze
kupata fedha.

Vilevile amempongeza Ponera kwa kujituma na kuwataka walemavu  na wale wasio walemavu kuiga mfano mzuri wa Ponera ambaye kila mwaka anatumia muda mwingi katika shughuli za kilimo  badala ya kukaa nyumbani na
kusubiri msaada kutoka kwa watu wengine.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti Ponera na Fungo wamemshukuru mkuu wa Wilaya kwa huruma yake ambayo imewawezesha kupata baiskeli hizo ambazo zitawasaidia katika shughuli zao za kujitafutia riziki.

Fungo alisema, kwa muda mrefu shida yake kubwa ilikuwa ni kupata
usafiri wa kutoka nyumbani hadi kwenda katika shughuli zake  kutokana
na changamoto anazokutana nazo kwenye usafiri wa umma hasa daladala.

Kwa upande wake Aron Msigwa,amewashukuru wadau wote wakiongozwa na
mkuu wa wilaya kwa moyo wao kumsaidia baiskeli ambayo itamsaidia
kumfikisha shambani na wakati mwingine kuitumia katika majukumu
mengine ya kijamii.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2