Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo.
Simu: 0766054094/0718878887
Gereza la Butimba ni muda wa kuonana
na wafungwa kama ratiba inavyoruhusu. Ni utaratibu kwa siku za jumatatu,
jumatano na ijumaa kuanzia saa 8 mchana mwisho saa 10 jioni. Kuna wanaokuja na
vyakula, vinywaji na vitu vidogo vidogo kama miswaki, dawa za meno, sabuni na
vinginevyo vifaavyo kwa wafungwa. Ni sheria kama umekuja na chakula au kinywaji
kuonja kwanza ili kuepusha kutilia sumu kwenye chakula. Jumatatu hii watu
hawakua wengi.
Waliandika majina ya ndugu na jamaa zao waliomo gerezani na pia
jina la mtu aliyekuja kumtembelea katika daftari maalum kisha askari alikwenda
kumuita mfungwa kadiri ya jina lililoandikwa.
Pascal
Mtumbuka alikuja katika eneo maalum la kuonana na aliyekuja kumtembelea baada
ya kuitwa jina na askari magereza. Alipofika eneo la kuonana na wageni
aliangaza macho huku na huku kuchambua mtu aliyekuja kumwona mahali hapa pa
kurekebisha tabia ambapo hapapendwi na wengi. Inasemwa gereza si kaburi lakini
kwa mateso na upweke na kukosa uhuru mara nyingine ni afadhali ya kaburi.
Macho
ya Pascal yakagota moja kwa moja kwenye sura ya mtu aliyekuwapo eneo hili nae
akimtumbulia macho. Anakumbuka kukutana nae mahali fulani lakini hakumbuki kama
anamfahamu. Sura anaifahamu lakini kwa jina hamfahamu sawia. Anavuta kumbukumbu
anakumbuka mahali alipowahi kuonana na mtu huyu. Anamtazama kwa chati na
kumbukumbu inapita kichwani mwake………….mlinzi anamsogelea mtu aliyeketi
bustanini kisha anamkata kibao kikali, mtu anageuka anafikiri kwa muda kisha
anamcheka mlinzi. Mlinzi anaghadhibika zaidi anamsemesha kwa hasira, mtu
anamtazama mlinzi kisha anacheka tena. Sisi nasi tunacheka hili tukio.
Aliepigwa kibao anatutazama kisha anatucheka. Mtu wa ajabu! Mlinzi anaondoka
kwa ghadhabu. Kijana anatusogelea anatusemesha maneno fulani kisha wote tunaandika
namba zetu za simu kwenye karatasi aliyotupatia huku tukicheka. Kisha
anaichukua anaondoka nayo. Anaondoka akituacha tunacheka lakini akituahidi
jambo fulani……………..Pascal anamaliza kukumbuka jambo fulani anamsogelea mgeni
kwa lengo la kumsemesha.
“Habari kaka, labda wewe ndiye mgeni
wangu?” Pascal akamsaili.
“ Yeah, mimi ndiye, pole na matatizo”
Mgeni akakubali.
“Asante ndugu, ndio changamoto ya
maisha ndugu yangu, napata adhabu ya kosa sijawahi hata kufikiri kulitenda,
hapa nilipo sijawahi kuua hata inzi kama niliua sisimizi ni kwa bahati mbaya na
sikujua, sifahamu nina uadui na nani sifahamu kabisa” Pascal alilalama.
“ kaka adui ni adui tu, na rafiki pia
ni adui, tena rafiki aweza kuwa adui m’baya zaidi. Ni rahisi kwa aliekutendea
mabaya kwa muda mrefu akaja kwa unyenyekevu wote akakutaka radhi ukamsamehe
lakini kuwa makini dunia ni tambara bovu akiwa mwema mshukuru Mungu lakini
usijipe asilimia zote kwamba kesho hawezi kurudia kukutenda tena, yeye
alikufanyia jana na leo anaweza kukufanyia kwani binadamu hubadilika kwa dakika
moja. Kosa laweza kuwa dogo sana kwako lakini kwake ni kubwa sana. Unaweza
kumtendea mtu jambo dogo sana yaani dogo sana lakini kwake likawa ni kubwa
kupitiliza, huwezi kujua huenda kapitia historia mbaya na hilo jambo lako lililo
dogo analiunganisha na makubwa aliyopitia hapo ndio udogo wa jambo lako
linapokuwa kubwa. Kumbuka pema usijapo pema ukipema si pema tena” Mgeni
alielezea.
“kaka mbona sijakuelewa?”, unatumia
lugha ngumu” Pascal alitoa malalamiko.
“Ndugu yangu fumbo mfumbie mjinga
mwerevu huling’amua. Unaweza kufikiri huna maadui lakini kumbuka hata kauli
yako ndogo tu, au ishara fulani, jambo fulani dogo tena ulilofanya bila
kukusudia linaweza kutengeneza uadui mkubwa tena bila kujua. Kumbuka mwindaji
huwinda akiwa amejificha au hata hajulikani, swala porini akimwona simba huwa
anakimbia mbali japokuwa simba mwenyewe
ameshiba, ukiona wanyama wawindao au hata mwindaji mwenyewe hajitokezi
hadharani ili anayemwinda amwone la
hasha, huwinda kwa kuvizia akiwa amejificha. Mimi sijaja kuongea maneno mengi
lakini mara nyingi unaweza usielewe jambo kwa sasa lakini baada ya kutafakari
ukalielewa vyema tena ukajilaumu kwanini hukuelewa kabla. Mara ya mwisho tulipoonana
ulikua unacheka tena nisingekufahamu bila nyinyi kunicheka, kicheko ni furaha
lakini kinyume cha furaha ni huzuni. Lakini kuna kauli nilisema NIKICHEKA
UTALIA mimi katika maisha yangu sipendi kucheka. Mtu atacheka kwa furaha lakini
akumulikae mchana usiku hata kuchoma, hebu tafakari vyema ni kwanini uko hapa
gerezani, ni kweli hujafanya kosa hebu jiulize mimi najuaje na hatukua pamoja
na kama hujafanya kosa ni nani aliyefanya?”. Mgeni aliongea maneno mengi ya
kuchanganya Pascal kichwa kilivurugika hakuelewa nini mgeni huyu anaongea.
Mgeni akaongeza
“Ndugu wacha mimi niende najua mjinga
akierevuka mwerevu yupo matatani, kwaheri” Mgeni aliongea kisha akajiondoa kwa
mwendo wa taratibu nyuma akimwacha Pascal hana kauli akibaki amepigwa na butwaa
kama mtu asiejielewa.
Baada
ya mgeni kuondoka Pascal aliondoka taratibu kichwa kikiwa kizito miguu
ilimwongoza kurudi vyumba ambavyo wanatumia wafungwa kisha akaketi chini
akajiinamia kwa mawazo lukuki.
Pascal
anakumbuka ni zaidi ya wiki tangu ahukumiwe kwenda jela miaka 30 kwa kosa la
mauaji tena mauaji ya mpenzi wake.
Ajabu!
Pascal hakuwahi kuwa na uhusiano na
Betty bali ni urafiki tu wa kawaida, Alikumbuka alikua anamwona Betty darasani
na maeneno ya chuo pengine na sehemu nyingne lakini hawakua wakifahamiana wala
hawakuwahi kuzoeana. Mazoea na Betty yalikuja baadae baada ya kupangwa katika
kundi moja la kufanya kazi za darasani (Group Discussion). Ni katika kundi
ndipo walifahamiana na marehemu Betty na Mwanaidi mpaka wakawa marafiki
waliozoeana.
Iweje aambiwe Betty mpenzi wake?!
Aliendelea
kutafakari maneno ya mgeni aliyekuja kumtembelea ambae anaongea misemo migumu
kuing’amua…. Fumbo mfumbie mjinga…….mjinga akierevuka…..
“Ina maana mimi ndiye mjinga
aliyemzungumzia?!” Pascal alijiuliza.
Alivuta kumbukumbu ya mgeni huyu
lakini alikumbuka tu alimwona pindi mlinzi akimzabua kibao kisha mgeni
akachukua namba zao akiahidi kuwaambia kilichomchekesha.
“Mbona hakutuambia? Au wenzangu
walishaambiwa?” Alinong’ona kimya kimya.
“Oooh halafu……” Pascal alivuta
kumbukumbu.
……..mgeni alinipigia simu siku moja ijumaa na aliniahidi kuja
kunitembelea kabla sijaenda kwenye kipindi jioni, hakuniambia hata jina,
niliangalia namba yake imesajiliwa jina gani nilipojaribu kumtumia hela jina
lililoonekana ni ZAINABU SHAMTE!. Inamaana anaitwa Zainabu?! Hapana Zainabu?!
Mbona ni jina la kike? Hapana sio jina lake. Aliniahidi kuja lakini sikumwona
mpaka leo hii. Halafu Bertha alinitumia meseji, nakumbuka ilinisisimua na kamwe
siwezi kuisahau, SWEETHEART
NIPO PEKE YANGU MPWEKE, NAJUA UPO FREE, PLEASE NJOO UNIPE KAMPANI NA
KUNA KITU KIZURI NATAKA NIKUPE. NJOO NA JUISI YA AZAM MANGO PLEASE. NIJIBU
NIKUPE DAKIKA NGAPI? Ilinisisimua nilikurupuka mbio mbio na juisi yangu halafu
mbona nilimkuta tayari anakunywa juisi aliyoniagiza au alikua ananijaribu?
Lakini mbona aliniuliza na wewe umeniletea juisi pia ina maana kuna mtu
aliyekua ameshaileta tayari!!!.....................nakumbuka alisema
mchekeshaji ameenda kuchukua chakula halafu hakurudi. Ni nani huyu mchekeshaji?
Ni kwanini hakurudi?.................. Mchekeshaji……………mchekeshaji wa wapi
hasa………..nimewahi kumwona?...........Siku tuliyokuwa tunacheka ni pale huyu
mgeni aliyenitembelea leo alipopigwa kibao kisha akacheka, akatucheka pia
Mwanaidi alifariki siku chache kabla, Bertha amefariki. Au na mlinzi
niliyemsikia amefariki kwa kudondoka dirishani ni yule aliyempiga kibao. Oooh
inawezekana……mimi nilikimbilia kwa Betty meseji yake ilinisisimua naanza kupata
picha kwa mbali huenda ni yale mambo ya mtaka nyingi nasaba hupata mwingi
msiba.unaweza kumkosea mtu kosa dogo kwake likawa kubwa………..nikicheka
utalia……..mlinzi alimpiga kofi amefariki lazima ni yeye, Mwanaidi alicheka ni
marehemu……..Betty nae alicheka yu kaburini………..Mimi pia nilicheka…………..niko
gerezani……. Ahaaaaa mlinzi alilia hata kama hakulia ndugu zake walilia…..
Mwanaidi alilia…. Betty nae…… mimi…….fumbo mfumbie mjinga….. halafu mjinga
akierevuka……NOOOOOOOOOOOOOOOOOO………………HUYU MGENI NDIYE
MUUUUAJIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIIII………….MIMI
SIJAUAAAAAAAAAAAAAA…….MKAMATENI MGENIIIIIIIIIIIII………………….. Pascal alizinduka
kwenye lindi la mawazo akapiga kelele kwa nguvu sana.
▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄
Jumatatu
jioni baada ya Riziki kutoka Butimba gerezani alikwenda moja kwa moja kwenye
maeneo ya nyumba za wahadhiri chumba anachoishi Jovin. Alimkuta amejipumzisha.
Dhumuni la kwenda ni kwa ajili ya kuazima kamera ya kurekodi video ili akafanyie
kazi iliyotolewa darasani ambayo ilimtaka kila mwanakozi kuandaa habari ya
televisheni isiyozidi dakika 5. Alimkuta Jovin kajipumzisha wakaongea hili na
lile kisha akafanikiwa kupata kamera aliaga na kuahidi kuirudisha baada ya siku
moja ambayo ni siku ya jumatano.
Ni
wanakozi watatu tu ndio waliokuwa wakimiliki kamera za kurekodi video. Wengi
walitegemea kamera za studio ambazo ni mbili pekee na hivyo zilikua na foleni
kubwa ya kuazima. Jovin rafiki wa Riziki nae alikua anamiliki kamera yake ndogo
ya kisasa ya kidigitali ambayo ilitumia kadi za kumbukumbu. Mwingine Clepas
Maima na mwingine mmoja.
ITAENDELEA.....................
Toa maoni yako, ushauri katika kisanduku hapa chini. Maoni yako yawe ni kwa ajili ya kuboresha na kukuza blog yetu.
Asanteni.............
ALFRED GASTO TARIMO
Post a Comment