Waziri wa Nchi ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
(OR-TAMISEMI) Mhe. George Simbachawene amewataka Wakuu wa Mikoa na
Wakuu wa Wilaya kupita madarasani kukagua wanachokifundisha walimu ili
kuhakikisha kuwa wanafunzi wanapata elimu iliyokusudiwa na Serikali.
Akizungumza na wakazi wa vijiji vya Wotta na Wangi katika halmashauri ya
Wilaya ya Mpwapwa jana Waziri Simbachawene alisema kuwa Viongozi hao
wana jukumu kubwa la kufuatilia maendeleo ya wanafunzi ili baadaye
waweze kutoa ushauri na si kuwaachia jukumu hilo wakaguzi peke yao.
Aidha Waziri Simbachawene ameziagiza Mamlaka za Serikali za Mitaa nchini
hususani halmashauri zihakikishe kuwa zinashirikiana katika kukagua
miradi hususan inayohusu maendeleo ya elimu ili kuona kuwa inakidhi
ubora kulingana na gharama iliyotolewa.
"Tushirikiane na wataalamu tupite na kukagua hata madaftari ya watoto
mara nyingi tumekua tukikagua miradi ya majengo ya shule, vituo vya
afya, nyumba za walimu lakini ifike mahala tuwe tunakagua hata ubora
unaotufanya tuwekeze kiasi kikubwa cha fedha,"alisema Mh. Simbachawene.
Alisema kila mwezi Serikali hutoa takribani shilingi bilioni 23 kwa
ajili ya uendeshaji wa shule na pia kuanzia mwezi wa nane mwaka huu
serikali imekuwa ikiwapa walimu wakuu wa shule za msingi shilingi laki 2
kila mwezi kwa ajili ya kuhakikisha kuwa huduma muhimu zinapatikana
shuleni hivyo viongozi wa halmashauri hawana budi nao kupita katika
shule hizo ili kuona mapungufu yanayoweza kujitokeza katika baadhi ya
shule.
Aidha Waziri Simbachawene alisema kuwa sekta ya elimu ya msingi ina
changamoto nyingi hivyo aliwashukuru wadau kwa kuitikia wito wa Rais wa
awamu ya tano Mhe. John Pombe Magufuli wa kutengeneza madawati mashuleni
na aliwataka viongozi hao kufuatilia utengenezaji wa madawati hayo.
"Wakuu wa wilaya, wakurugenzi, watendaji wa kata, watendaji wa vijiji na
waheshimiwa madiwani hakikisheni madawati haya yanaingia madarasani,
bado yapo madawati mengi kwa mafundi na makandarasi tumeyaona mengine
pembezoni mwa barabara, madawati haya yanatakiwa yawe shuleni na watoto
wakalie," alisisitiza Mh. Simbachawene
Pia aliwataka viongozi wa halmashauri kutumia vizuri rasimali za
halmashauri hasa katika kufanya ukaguzi wa miradi mbalimbali kwa
kushirikiana idara moja na nyingine ikiwezekana hata kuambatana kwa
pamoja ili kuthibitisha kazi hizo.
"Lakini nitoe rai kwa viongozi wa halmashauri kuungana kwa pamoja kila
idara wanapo kwenda kukagua mambo yaliyopo katika vijiji ili kuweza
kuokoa gharama kubwa kwenye halmashauri zao na nachukua nafasi hii
kuwaagiza wakuu wa mikoa halmashauri kuhakisha kwamba wanatembelea bila
kukosa lakini watumie gari moja au mbili,"alisema
Pia aliongeza kuwa lazima kuwa wazalendo wa nchi na kusimamia watu wa
hali ya chini kwasababu ndipo walipo watu wenye mahitaji zaidi ili
kuweza kubadilisha maisha yao.
Post a Comment