Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa
Mhe.George Simbachawene amesema kuwa wanafunzi 526,653 kati ya 555,291
waliofaulu mtihani wa kumaliza darasa la saba mwaka huu wamechaguliwa
kujiunga Kidato cha Kwanza mwakani katika shule za sekondari za
Serikali.
Kwa mujibu wa takwimu hizo, idadi hiyo ya wanafunzi waliochaguliwa
kujiunga na kidato cha kwanza katika awamu ya kwanza ni sawa na asilimia
94.85 ya wanafunzi wote waliofaulu.
Akizungumza na Waandishi wa habari tarehe 28 novemba 2016 mjini Dodoma
Mheshimiwa Simbachawene ameeleza kuwa wanafunzi 28,638 wakiwemo wavulana
12,937 na wasichana 15,701 hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza ya
uchaguzi.
Aidha Waziri Simbachawene aliitaja mikoa ambayo wanafunzi wake walifaulu
lakini hawakuchaguliwa katika awamu ya kwanza kuwa ni pamoja na Dar Es
Salaam (18,820), Arusha (4,752), Songwe (1,465), Kigoma (1,208), Manyara
(1,141), Lindi (608), Mbeya (406) na Katavi (238).
Kuhusu wanafunzi waliochaguliwa Mheshimiwa Simbachawene amesema kuwa,
wasichana ni 268,052 sawa na asilimia 94.5 na wavulana ni 258,601 sawa
na asilimila 95.2.
Aidha, Mheshimiwa Waziri wa Nchi amesema kuwa wanafunzi wote wenye
ulemavu waliofaulu wamechaguliwa kujiunga na Kidato cha Kwanza mwaka
2017.
Kwa mujibu wa Mheshimiwa Simbachawene mchanganuo wa wanafunzi
waliochaguliwa kujiunga kidato cha kwanza katika shule za serikali
umegawanyika katika makundi manne ambapo kundi la kwanza limehusisha
wanafunzi 900 wakiwemo Wavulana 480 na Wasichana 420 ambao wamepelekwa
katika shule za Bweni kwa wenye ufaulu mzuri zaidi.
Ameongeza kuwa kundi la pili limehusisha wanafunzi 1005 ikiwa ni
Wavulana 915 na Wasichana 90 ambao wamepelekwa katika shule za Bweni
mahsusi kusomea Ufundi.
Pia amesema kuwa kundi la tatu limewahusisha Wanafunzi 780 wakijumuishwa
Wavulana 430 na Wasichana 350 ambao wamechaguliwa kujiunga na Shule za
Bweni Kawaida na kundi la nne limewahusisha wanafunzi 723 wakiwemo
wavulana 405 na wasichana 318 wa shule za bweni kwa ajili ya wanafunzi
walio na Ulemavu.
Kulingana na takwimu hizo, Waziri Simbachawene amesema kuwa jumla ya
wanafunzi 3,407 wamechaguliwa kujiunga na shule za bweni kidato cha
kwanza ambapo wavulana ni 2,230 sawa na asilimia 65.4 na wasichana 1,178
sawa na asilimia 34.6, pia watahiniwa wapatao 6,260 sawa na asilimia
0.78 ya waliosajiliwa hawakufanya mtihani.
Aidha Waziri Simbachawene amesema kuwa wanafunzi 523,245 wakiwemo
wavulana 256,371 na wasichana 266,874 wamechaguliwa kujiunga na kidato
cha kwanza katika shule za kutwa.
Wakati huo huo Mhe. Simbachawene amesema hatasita kuzichukulia hatua,
shule zilizohusika na udanganyifu wa mitihani kwani wanarudisha nyuma
maendeleo ya taaluma nchini yanayofanywa na Serikali.
"Serikali imeanza kuwachukulia hatua kwa mujibu wa taratibu wale wote
waliohusika na udanganyifu huu� hatua hizo ni pamoja na kuwavua madaraka
waliokuwa Waratibu Elimu Kata na Walimu Wakuu, kuwashtaki mahakamani na
kupeleka mashauri yao Tume ya utumishi ya Walimu (TSC)," amesema
Mheshimiwa Waziri.
Pia ametoa agizo kwa Wakuu wa Mikoa kubainisha sababu za wanafunzi
walioingia darasa la kwanza kutomaliza masomo yao kama ilivyotarajiwa.
"Naagiza Wakuu wa Mikoa kubainisha sababu za wanafunzi hao kutomaliza na
hatua stahiki za kuchukuliwa ili kuhakikisha kuwa wanafunzi wote
wanaoandikishwa darasa la kwanza wanamaliza mzunguko wa masomo kwa
mujibu wa Sera ya Elimu," amesisitiza Mhe. Simbachawene na kutaka Wakuu
wa mikoa kuchukua hatua stahiki zilizoelekezwa.
Post a Comment