SERIKALI
imesema kuwa hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya kuridhisha na
kuwataka wananchi kupuuza taarifa zinazodai kuwa hali ya chakula ni
mbaya.
Hayo
yamebainishwa leo jijini Dar es Salaam na Waziri wa Kilimo, Mifugo na
Uvuvi Dkt. Charles Tizeba wakati akizungumza na waandishi wa habari
kuhusu hali ya upatikanaji na chakula nchini.
“Ndugu
waandishi ukweli ni kwamba hali ya upatikanaji wa chakula nchini ni ya
kuridhisha sana katika maeneo mengi, hivyo siyo kweli kwamba kuna tatizo
la njaa kama baadhi ya watu wanavyojaribu kupotosha,” alisisitiza Dkt.
Tizeba.
Aidha
Dkt. Tizeba aliongeza kuwa pamoja na kuwepo kwa hali nzuri ya chakula,
Serikali kupitia Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) imeendelea
kuweka akiba ya chakula kwa kununua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi
ili kuhakikisha nchi inaendelea kuwa na chakula cha kutosha,
Dkt.
Tizeba amesema kuwa kwa mwaka wa fedha 2016/2017 Serikali imejipanga
kununua jumla ya tani 100,000 za chakula ambapo hadi kufikia Januari 8
mwaka 2017 imenunua jumla ya tani 62,087.997 za mahindi sawa na asilimia
62 ya lengo ililojiwekea.
“Kati ya
kiasi kilichonunuliwa, tani 38,162.280 zimenunuliwa kupitia vituo vya
ununuzi na tani 23,925.717 kupitia vikundi vya wakulima hivyo hadi
kufikia tarehe 12 Januari, 2017 Wakala wana akiba ya tani 88,152.443 za
mahindi,” alisema Dkt. Tizeba.
Waziri
Tizeba ameongeza kuwa hadi kufikia katikati ya mwezi Januari, 2017 hali
ya chakula na upatikanaji wake hapa nchini bado ni ya kuridhisha na hasa
upatikanaji wa vyakula kama mchele na maharage ikilinganishwa na zao la
mahindi.
Aidha,
Wizara kwa kushirikiana na Ofisi ya Waziri Mkuu, TAMISEMI, FAO, TFNC
pamoja na wadau wengine wanaendelea kufanya tathmini ya kina ya hali ya
chakula na lishe nchini ambayo inatarajiwa kukamilika Januari 28 mwaka
2017 na itazihusisha Halmashauri 55, tathmini hiyo itaiwezesha Serikali
kupata taarifa za uhakika zaidi kuhusu hali ya chakula na lishe nchini.
Amefafanua
kuwa kutokana na hali ya mwenendo wa unyeshaji wa mvua za vuli na msimu
kutokuridhisha katika maeneo mengi ya nchi, Serikali imewashauri
wakulima kutumia mbegu zitakazokomaa mapema na kupanda mazao
yanayostahimili ukame pamoja na kutumia kwa uangalifu na kuhifadhi akiba
ya chakula cha kutosha kwa matumizi katika kaya.
Aidha,
Sekta binafsi zimehamasishwa kuendelea kushiriki katika kutoa masoko ya
kununua na kuuza mazao katika maeneo yenye ziada na kuyauza katika
maeneo yenye uhaba.
Ufafanuzi
huo umetolewa kufuatia kuwepo kwa taarifa za upotoshwaji juu ya hali ya
upatikanaji wa chakula hapa nchini ambapo Dkt. Tizeba amesema huo ni
upotoshaji wenye lengo la kuwatia hofu wananchi
Post a Comment