MFUKO WA WAATHIRIKA WA AJALI ZA BARABARANI UANZISHWE

Jonas Kamaleki- Moshi

Baraza la Ushauri la Watumiaji wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA CCC) limeomba
Kuanzishwa kwa Mfuko wa Waathirika wa Ajali za Barabarani ili kuwasaidia Waathirika hao kupata huduma za matibabu pindi wapatapo ajali.

Rai hiyo imetolewa leo mjini Moshi na Afisa Elimu Watumiaji , Nicholaus Kinyariri katika mahojiano maalum na Idara YA Habari (MAELEZO) wakati wa wiki ya nenda kwa usalama
Barabarani inayofanyika kitaifa mkoani Kilimanjaro.

Kinyariri amesema kuwa majeruhi wengi wa ajali za barabarani hukosa matibabu ya haraka pindi wanapopata ajali kwani wengine hukutwa hawana kipato au Bima za Afya kugharamia matibabu yao.

Unakuta mtu anagongwa na gari halafu gari hilo linakimbia kiasi kwamba aliyepata ajali hawezi kujua nani kamugonga ili aweze kuhudumiwa, matokeo yake mwathirika hukosa matibabu na hatimaye hupoteza maisha.

“Ni muhimu sana kuanzishwa kwa Mfuko wa Waathirika wa Ajali za Barabarani ili kupunguza ama kuondoa adha wanazozipata watu hao,” alisema Kinyariri.

Afisa huyo amesisitiza kutolewa kwa Elimu kuhusu masuala ya Usalama barabarani ili kuongeza uelewa kwa wananchi jinsi ya kupunguza ajili za barabarani.

Aidha, Kinyariri amesema kuwa SUMATRA CCC imeanzisha mafunzo kuhusu Haki na Wajibu wa mtumiaji wa barabara ili kupunguza ama kuondoa Ajali za barabarani.

Amesema kwa kulitambua hilo SUMATRA CCC imetoa mafunzo kwenye mikoa tisa nchini ambapo jumla ya wanafunzi 666 wamepata mafunzo hayo kwa kipindi cha miezi michache iliyopita.

Amewaomba wananchi wapaze sauti zao kupinga ajali za barabarani na kwa kufanya hivyo hatua madhubuti zitachukuliwa na serikali na kuzuia ajali hizo.

Kwa upande wake, Afisa Mfawidhi SUMATRA Mkoa wa Kilimanjaro, Johns Makwale amesema kuwa ili kupunguza ajali inabidi madereva wawe wanapata mafunzo ya mara kwa mara kuhusu masuala ya Usalama barabarani.

Ameiomba Serikali kuboresha miondombinu hasa ya barabara kwani nayo hawa ni chanzo cha ajali nyingi za barabarani.

Amewataka madereva kuwa makini wawapo barabarani na kuzingatia sheria za barabarani hasa alama za barabarani.

Makwale amewataka watoa huduma za usafiri wawe na utu na kuwajali wenzao ili waweze kuwahudumia vizuri na kuepusha migongano na kuwaza sana maslahi kitendo ambacho kinachangia kusababisha ajali.

Naye Mratibu wa Mradi wa Kupunguza Vifo na Majeruhi wa Bloomberg , wakili Mary Kessy amesema Ajali za Barabarani zinaepukika kwa kuondokana na uzembe wa madereva na abiria kwa ujumla.

Madereva na abiria wakitimiza wajibu wao wakiwa barabarani ajali nyingi zitaepukika, aliongeza Kessy.

Amesema kwa Tanzania ni viashiria vitano vya ajali ambavyo vikitiliwa mkazo, ajali zitapungua . Amevitaja viashiria hivyo kuwa ni mwendokasi, ulevi, kutofunga mikanda ya usalama, kutokuwa na vizuizi vya watoto na kutovaa kofia ngumu kwa waendesha pikipiki.

Maadhimisho haya, yalizinduliwa na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, mjini Moshi ambapo alisisitiza watanzania kushirikiana kupambana na Ajali za barabarani. Kauli Mbiu ya mwaka huu ni Tii sheria, Zuia Ajali, Okoa Maisha.


SOMA ZAIDI

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2