Jonas Kamaleki – Moshi
Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro , Mama Anna Mghwira amekemea vitendo vya rushwa barabarani na kusema kuwa Askari atakayebainika atachukuliwa hatua kali za kisheria.
Mama Mgwira ameyasema hayo leo mjini Moshi wakati akifunga Maadhimisho ya Wiki ya Nenda kwa Usalama Barabarani ambayo yamefanyika kitaifa Mkoa wa Kilimanjaro .
Amesema kuwa kupokea au kutoa rushwa kwa masuala ya barabarani ni kuua watu na jamii kwa ujumla hivyo kuwataka matrafiki kuacha vitendo hivyo mara moja.
“Nawaambia ninyi mnaokula rushwa barabarani muache mara moja vinginevyo mtakiona cha moto, na nataka kauli Mbiu ya mwaka huu isemayo, Zuia Ajali, Tii Sheria, Okoa Maisha, iongezwe haya, Acha Rushwa Barabarani,” alisema Mghwira .
Aliongeza kuwa ajali nyingi za barabarani zinasababishwa na rushwa hivyo kuwataka madereva na matrafiki kuacha na na rushwa.
Aidha, Mkuu huyo wa mkoa amesema rushwa inafanya watu wakose ubunifu katika kutengeneza bidha na kuiga za wengine na hivyo kulitaka Shirika la Viwango Tanzania (TBS) kuwa makini na watu wa namna hiyo.
“Tukiacha rushwa na kutii sheria, Ajali za Barabarani zitapungua,” aliongeza Mghwira
Kwa upande wake, Kamanda wa Kikosi cha Usalama Barabarani , SACP, Fortunatus Muslimu amesema Ajali za Barabarani zinaepukika sheria zikizingatiwa.
Amesema wananchi washirikiane na kikosi cha Usalama Barabarani ili kuepusha ajali za barabarani na kuokoa maisha ya Watanzania.
Alimalizia kwa kusema Tanzania bila Ajali inawezekana kila mmoja atimize wajibu wake.
Maadhimisho hayo yalifunguliwa tarehe 16, Oktoba 2017 na Makamu wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na kufungwa rasmi na Mkuu wa Mkoa wa Kilimanjaro , Mhe. Anna Mghwira. Kauli Mbiu ya Maadhimisho hayo ni Zuia Ajali, Tii Sheria, Okoa Maisha.
SOMA ZAIDI
Post a Comment