Na. Eliphace Marwa .
JUMLA ya Vijana 31 wanatarajia kuiwakilisha Tanzania katika tamasha la dunia la vijana linalotarajia kufanyika Jijini Sochi nchini Urusi kuanzia tarehe 14 hadi tarehe 22 Oktoba mwaka huu.
Akizungumza na ujumbe wa Vijana hao leo Jijini Dar es Salaam wakati wa kukabidhiwa bendera ya Taifa, Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Erick Shitindi alisema tamasha hilo litakuwa na zaidi ya washiriki ishirini elfu kutoka nchi 150 Duniani kote.
Shitindi aliwapongeza vijana hao kwa fursa ya kuiwakilisha Tanzania katika tamasha hilo na kuwaomba kuitumia vyema fursa hiyo kwa ajili ya kuiwakilisha vema na kutangaza uzuri wa nchi viongozi kwa mataifa mbalimbali.
“Tamasha hili litatoa fursa kwenu vijana wa Tanzania na mtakapokuwa huko kuzungumzia mambo mazuri ya Tanzania na hasa kutangaza uzuri wa nchi yetu kwa vijana wa mataifa mengine” alisema Shitindi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Erick Shitindi (katikati) akimkabidhi bendera mmoja wa vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la vijana na wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi, kulia ni Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Vijana Bi. Venerose Mtenga.
Mkurugenzi Msaidizi wa Maendeleo ya Vijana Bi. Venerose Mtenga toka Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu akitoa taarifa kwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu - Kazi, Ajira, Vijana na Wenye Ulemavu Bw. Erick Shitindi juu ya vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la Vijana na Wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi.
Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Erick Shitindi (aliyevaa tai) akiwa katika picha ya pamoja na vijana watakaoshiriki tamasha la 19 la Dunia la vijana na wanafunzi jijini Sochi nchini Urusi mapema hii leo jijini Dar es Salaam. Picha na Eliphace Marwa – Maelezo.
from Michuzi Blog
Soma Zaidi
Post a Comment