Na.Samuel Samuel
Baada ya kuwashudia mabingwa watetezi wa ligi kuu Tanzania bara Yanga SC jumamosi wakiwabanjua 1-2 Azam FC ndani ya uwanja wao wa Azam Complex , Mbeya City wakitoka sare tasa ya 0-0 na Mtibwa Sugar kutoka Morogoro, Mwadui FC wakiwa nyumbani pia dhidi ya Mji Njombe wakitoka sare ya 2-2 , leo vinara wa ligi hiyo Simba SC watakuwa wenyeji wa wana Lizombe Majimaji FC katika dimba la uwanja wa Taifa.
Emanuel Okwi kinara wa ufungaji wa ligi kuu Tanzania bara mwenye magoli 10 ambayo yote ameyapata ndani ya jiji la Dar es salaam yaani yote ameyafunga katika viwanja vya Uhuru na taifa na kuifanya Dar es salaam kama ngome yake ya kuziadhibu timu zote ambazo zinaikabili Simba SC akiwa na kikosi hicho.
Kuelekea mchezo huo ambao umeteka hisia za wengi kutokana na kasi ya wanamsimbazi hao katika kuusaka ubingwa wa ligi kuu kwa kushinda kila mechi mbele yao, Emanuel Okwi amenyoa nywele zake na kubaki kipara akijinadi kumaliza duru la kwanza la ligi kuu kwa kishindo ukiwa ni muonekano wake mpya.
“ kikubwa ni ushindi kwa timu yangu. Kama nitapata fursa ya kucheza nitashirikiana na wenzangu kuipa ushindi timu yetu ili kujiweka pazuri katika harakati zetu za kuusaka ubingwa . Nikipata fursa ya kufunga nitashukuru pia “
Hivi karibuni Simba SC chini ya kocha wao msaidizi Masoud Djuma wamekuwa wakitumia mfumo wa 3-5-2 ambao umegeuka mwiba mkali kwa timu mbalimbali ligi kuu. Ni mfumo ambao umeibadili kabisa Simba katika mfumo wao wa kushambulia na kujilinda kwa kuipa uwiano mzuri kwa kila idara uwanjani kucheza kwa uelewano mkubwa . Ni mfumo ambao umeifanya Simba kuwa na umiliki mzuri wa mpira kwa kutumia viungo wengi kati pia kuongeza kuwa na uwezo mzuri wa kushambulia pande zote .
Saidi Hamisi Ndemla amegeuka mfalme wa mfumo huu ndani ya kikosi cha Simba SC akisimama kama mpishi mkuu wa magoli ya timu pia kufunga.
Simba wanaingia uwanjani leo kwa mara ya kwanza chini ya kocha wao mkuu mpya raia wa Ufaransa Pierre Lechantre ambaye mbali na mbinu zingine amesema hataubadili mfumo wa timu hiyo wa 3-5-2 ambao umeanzishwa na msaidizi wake Masoud Djuma zaidi ya kuongeza mbinu zake nyingine kuuboresha hususani katika kasi ya kushambulia, umakini wa kutengeneza nafasi nyingi za kufunga na kuzitumia pia umiliki mzuri wa mpira na nyinginezo ambazo ni siri yake dhidi ya wapinzani wake.
Licha ya ubora wa Simba, Majimaji FC sio timu ya kubeza licha ya kushika nafasi ya 14 katika msimamo wa ligi wakiwa na alama 12 tu baada ya kucheza mechi 14.
Mechi ya mwisho Majimaji walicheza na Azam FC katika uwanja wao wa nyumbani mjini Songea na kutoka sare ya 1-1 Majimaji wakisawazisha kwa kona safi iliyojaa golini moja kwamoja kipindi cha pili. Azam kabla ya kuivaa Majimaji walitoka Zanzibar kutwaa kombe la Mapinduzi wakiwa na moto mkali na mfumo wao wa 3-5-2 lakini kocha wa Majimaji mzee Kondo aliweza kuwajenga vyema vijana wake kuizuia Azam kuondoka na alama tatu uwanjani kwao licha yakuwa katika kiwango kizuri kama timu pia uwezo mzuri wa mchezaji mmoja mmoja .
Simba wana uwezo mzuri wa kushinda mechi ya leo kutokana na ubora wao kama timu na uwezo wa mchezaji mmoja mmoja lakini hili litawezekana endapo wataiheshimu Majimaji kama washindani wa kweli.
Majimaji msimu huu licha ya kusuasua kwenye ligi lakini imekuwa na uwezo mzuri wa kuzicheza ‘ big matches ‘ . Sare ya 1-1 dhidi ya Yanga mwanzoni mwa ligi pia mechi ya mwisho ya 1-1 dhidi ya Azam FC na sare nyingine ya 1-1 na Singida United ni kengele ya hatari kwa Simba SC kuiendea mechi ya leo kwa tahadhari kubwa. Sare hizo ni mtaji mzuri kisaikolojia kwa Majimaji FC kujenga hali ya kujiamini kuivaa Simba ikiwatumia washambuliaji wake wazoefu Mapunda na Jerry Tegete na mfumo wao wa 4-4-2.
Kikubwa kwa upande wa Majimaji ni kujipanga kuicheza mechi hiyo kitimu zaidi na sio kuwapa tension kubwa baadhi ya wachezaji wa Simba kama Ndemla na Okwi kutokana nakuwa na viwango vizuri hivi karibuni. Simba kwa mfumo inaotumia imekuwa hatari zaidi kwa kuruhusu kila mchezaji kuwa na uwezo mzuri wa kukaba na kushambulia inapopatikana nafasi ya wazi. Simba wamekuwa na uwezo mkubwa wa kutengeneza nafasi za kufunga katika njia zote tatu kulia, kushoto na kati.
Ujio wa Shomari Kapombe ni mtaji mwingine mkubwa kwa Simba SC katika mfumo wao wa 3-5-2 unaotaka wing backs wenye uwezo mzuri kupanda juu kusaidia mashambulizi. Akicheza mechi yake ya kwanza katika msimu huu 2017-18 baada ya majeruhi ya muda mrefu dhidi ya Kagera sugar aliweza kutoa pasi nzuri ya goli kwa John Rafael Bocco ndani ya 18 na bila ajizi akaipatia Simba goli la pili.
SOMA ZAIDI

Post a Comment