Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo
Simu: 0766054094/0718878887
Ngoja
nikupe kisa kimoja kilichonitokea siku hiyo ya Valentine miaka minne iliyopita.
Naitwa
Riziki, nakumbuka siku hiyo nilijiandaa vyema kwani nilishafanya maandalizi ya
kutosha siku chache kabla ya siku yenyewe. Uwezo na kipato changu ni kidogo
lakini haikunifanya nishindwe kudunduliza kununua tisheti mbili nyekundu zenye
maua ya kuvutia ya rangi ya upendo yangu mimi na ya mpenzi wangu Happy,
nilinunua na vizawadi kadhaa ambavyo nilitaka nimfurahishe laaziz wangu barafu wa
moyo wangu. Niliandaa pia vijihela vya kutosha kwa matumizi ya siku hiyo.
Basi
siku ya siku ilifika na kwa kweli niliisubiri kwa hamu kwani sikuwahi
kusherehekea siku hii nikiwa na mpenzi wangu. Tangu asubuhi niliziona saa
zikijongea taratibu sana kama vile kuna mtu alikua akizishikilia zisisogee.
Hatimae muda uliwadia nikaanza
kujiandaa. Mimi nilikua naishi chumba cha kupanga maeneo ya Kambarage Shinyanga
mjini lakini mpenzi wangu Happy yeye aliishi Mwadui kilometa kama 25 hivi
kutoka shinyanga mjini. Kwakua tulikubaliana na Happy aje Mjini ambako ndipo
pamechangamka tofauti na kule Mwadui basi wakati nafikiria kujiandaa nae
alinipigia simu ndio anajiandaa kutoka. Basi nilianza kujiandaa taratibu kwani
kutoka Mwadui mpaka shinyanga ni umbali wa kama lisaa limoja. Mtoto wa kiume
nikaoga mara mbili mbili nikamaliza nikaingia kuvaa nikatupia jinzi langu la
mabaka mabaka nililonunua mitumbani soko la Ngokolo juu nikatupia tisheti langu
jekundu ambalo lingine nilimpa Happy kwa ajili ya siku hiyo shingoni nikaning'iniza
cheni kubwa la rangi ya Silva ambalo nilimtapeli mshkaji wangu Fulani, chini
nikatupia raba zangu nyeupe ambazo nilizipiga rangi nyeupe kwa ufundi mkubwa
zikang'aa na kunifanya nipendeze nahisi tangu nizaliwe sijawahi kupendeza hivi
Riziki Mimi. Nilipomaliza nilichukua vimarashi vyangu nilivinunua buku jero
lakini vina harufu nzuri utadhani pafyumu ya gharama sana. Baada ya hapo
nikachukua simu yangu ya kichina ambayo niliinunulia kava la bei ghali
ikavutia, kisha usoni nikatupia miwani nyeusi ambayo niliiokota kwenye gari
siku moja hivi kisha nikatia komeo chumba changu nikaelekea kituoni kumpokea wa
ubani wangu. Njiani mwondoko nilibadilisha. Kwa kua kituo hakikua mbali basi
niliamua kutembea, basi mwanaume nikatembea nadunda kama viatu vina springi.
Mkononi nina kimfuko chenye maua ya kupendeza ambamo ndani yake kuna zawadi za
happy.
Basi nikiwa kituoni niliwasiliana na Happy
ambae aliniambia yupo karibu nikavuta subira kumsubiri chaurembo wangu. Kwa
kweli mapigo ya moyo yalikua kasi na moyo ulidunda kwa nguvu kama kuna mtu
anapiga ngoma ndani ya moyo wangu.
Wakati namsubiri Mara alishuka dada mmoja
katika bodaboda, alikua amevaa gauni jekundu, mkoba mwekundu na chini viatu
vyekundu hakika alipendeza sio siri na ukichangia vile alikua mzuri acha tuu
Mungu kaumba. Nilimtazama, nikamtathmini akili zikaganda kwa muda, mpaka
akaanza kuvuka barabara ndipo nikahamisha jicho baada ya kuona gari ambayo
inatoka Mwadui ikiingia kituoni.
Asalaaaleee!!!!!
Ghafla kilitokea kishindo na ukelele mkubwa, mamaaaaaaaaa......
Hapo kila mtu aligeuza macho na mimi
nikiwa mmoja wapo. Alikua ni yule dada niliyekua namkodolea macho safari hii
alikua chini anagaragara, watu walianza kusogea eneo lile baada ya boda boda
iliyomgonga kuondoka kwa kasi. Nami nikajisogeza kushuhudia haraka ili nimuwahi
Happy ambae angekua anashuka kwenye gari, nilijipenyeza kwenye kijikundi cha
watu hadi pale alipo yule dada ambae alikua anagara gara pale chini. Cha ajabu
hakuna aliyeonekana kumpa msaada wengi walishuhudia wakawa wanajitoa mmoja
mmoja wanawapisha wengine, cha ajabu wengine badala ya kutoa msaada wao walikua
bize kupiga picha, watanzania sijui tumekuwaje siku hizi. Yule Dada pale chini
alinitupia jicho la kukata tamaa akanisemesha kwa shida, ka..ka
nisa...i..di..ee ta..fa.dhali.. Hapo akili ikafunguka nikajua nini nilipaswa
kufanya. Nikauweka mfuko wangu chini nikamnyanyua japo alikua mnene kiasi
hakunipa shida, angenipaje shida wakati ninafanya kazi za shuruba kila siku za
kubeba magunia ya dengu na choroko kiwandani? Nikambeba kuelekea zilipo taksi,
wakati naikaribia taksi macho yangu yakagongana na ya mpenzi wangu Happy
aliekua ananitazama. Hapo nikashtuka kidogo nikampa ishara ya macho anifuate,
lakini alinitazama tu basi nikaona isiwe shida wacha nimuwahishe hospital niokoe uhai wake kisha nimuwahi
Happy. Tukaondoka mpaka hospitali ya mkoa nikamwacha Happy pale stendi.
Tulipofika hospitali eti wakagoma kumpokea eti mpaka twende polisi tukapewe
sijui wanaita PPF.... Sijui PF nini hata sikumbuki vizuri. Yaani hizi sheria za
Tanzania nazo, eti mgonjwa yu taabani badala ya kupata huduma eti twende
polisi. Basi tukafanya hivyo tukafanikiwa akapokelewa hospital, kwa kua
sikumfahamu jina Basi nilimwandikisha kwa jina la Happy Riziki. Baada ya
taratibu za hospitali niliamua nimuwahi happy wangu kule stendi kwa mgonjwa
ningerudi baadae.
Mhhhhhh!
Nilizunguka mno pale stendi sikumwona happy wangu. Nikaamua nichukue simu ili
nimpigie.
Uuuuufuuuuu!!!!
Nilishusha pumzi za uchovu baada ya kuikosa simu yangu mifuko yote ya suruali.
Riziki
nilichoka. Nilikumbuka mfuko wa wa zawadi za Happy niliouacha pale
nilipomchukua majeruhi nao haukuepo najua walichauchukua
"wajasiriachochote". Basi nilibaki natembea tembea nikirusha rusha
mikono nisijue pa Kumpata Happy kwani namba zake za simu sikuwa nimezikariri
kichwani. Sio kwamba sikutaka kuzikariri bali kichwa changu ni kigumu sana
kukariri namba za simu. Hapo sikua na mawasiliano kabisa na Happy na sikujua
hata simu imepotelea wapi.
Baada ya kukaa na kutuliza kichwa majira kama
ya saa kumi jioni nilinyanyuka chini ya mti niliokua nimekaa nikaamua niende
hospitali kumtazama yule "Happy" majeruhi, bado sikujua kama hali
yake itakuwaje maana alipoteza fahamu na alikua ameumia vibaya. Wakati
najishauri Mara nilimwona Happy wangu akiwa anatembea kuelekea mwelekeo
mwingine na hakua ameniona. Nilipata faraja kubwa na furaha ikanilipuka
nikamkimbilia na nilipomkaribia nikamwita.
Happy.....
Happy....
Aligeuka nikitegemea angenipokea kwa
kumbatio la nguvu. Oooigh nilikua mnyonge happy aliponigeukia kwa hasira kisha
akaongea.
"Nenda
kamwite Valentine wako uliyempeleka
hospitali". Loooh! Niliumia sana nikajaribu kumwelewesha lakini hakua
ananielewa.
"
Hivi Riziki we unajifanya msamaria saana kuliko wote, kama humfahamu kwanini
usingewaacha wengine wampeleke hospitali hadi uwe wewe? Usinifanye mtoto
Riziki".
Nilijaribu
sana kumsihi happy mwishowe kwa shingo upande nilijaribu kumshawishi twende
hospitali pengine tungemkuta mgonjwa na fahamu angeeleza ukweli au labda ndugu
zake wengine wangenisaidia.
Tulifika hospitali, tukawakuta wazazi wa happy ambao niliwatambua kwani
walikua wanaelezewa na nesi niliyemkuta pale na nilipofika tu nesi alinigeukia
sikujua aliongea nini, nami na Happy tukaamua kuwasogelea nilitaka kuwaeleza
kuwa mimi ndiye niliyemleta hospitali. Kabla sijaongea akatokea daktari.
"Nyie
ndio ndugu wa huyu msichana Happy Riziki?"
Wazazi walitazamana lakini mimi niliitika
nikatoa maelezo kwa wazazi kuwa niliandika lile jina sababu sikuwa namfahamu.
Mpenzi wangu Happy alinikata jicho la hasira sana lakini tukatulia kusikiliza
dokta anasema nini. Daktari alitueleza Mgonjwa aliumia vibaya sehemu ya
kichwani na pia ubongo umeshtuka hivyo hata kama akipona atakuwa hana
kumbukumbu au atapatwa na tatizo la kupoteza kumbukumbu mara kwa mara. Baada ya
maelezo nilitaka kuwaeleza wazazi wa binti ambae kumbe aliitwa Angella.
Lahaula!!!
Happy wangu hakuwepo!!! Sikujua aliondoka saa ngapi. Niliamua kuwaaga wazazi
ningerudi baadae nikaondoka nimtafute happy. Wakati natoka getini nilimkuta
pembeni akinisubiri. Alikua na hasira kali, na alinipokea kwa maneno makali.
"Riziki
sikujua kama ni mshenzi kiasi hiki, yaani kumbe unao happy wawili
unatuchanganya utakavyo......" Happy alikunya mbovu kwa hasira
aliniporomoshea maneno bila kunipa nafasi ya kujitetea.
"Kuanzia
Leo sahau kabisa kama tuliwahi kuwa na uhusiano tena Leo hii nakuapia utajuta
kahaba wa kiume" alinidhihaki sana akaniacha wapita njia wakinitazama
wengine kwa huruma, wengine wakicheka wengine wasielewe, nikaondoka kwa aibu na
majonzi kichwa chini kwenda kumalizia Valentine yangu chungu kwenye ghetto
langu.
Ni majira ya saa kumi na mbili jioni nikiwa
naamka ili niende hospitali kumwona Angella aliyepata ajali ambaye nilimbatiza
jina la happy ndipo nilikutana na happy akiwa na kaka yake waliokuja kishari.
Niliwakaribisha ndani na nilipoingia tu mlango ulifungwa na nilipokea kipigo
kitakatifu kutoka kwa kaka yake Happy. Nilijaribu kujitetea lakini sikuhimili.
Nilipigwa nikapigika, nilichapwa nikachapika, waliondoka wakiniacha
nyang'anyang'a. Nilibaki nikiifurahia Valentine kwa mtindo huo.
Baada ya kupata ahueni angalau kidogo basi
nilijiburuza nikajikusanya nitafute wapi kilipo kiberiti wapi jiko na wapi
sufuria nichemshe angalao maji nikande majeraha yangu.
Ni wakati nimemaliza kuwasha jiko langu la
mkaa ndipo nilisikia gari likipaki nje kwa ghafla, kutahamaki waliingia polisi
wawili na bunduki, kabla sijajua nini kinaendelea nilijikuta tayari nina pingu
mkononi na vipigo vikitua tena kwenye mwili wangu. Nilitoneshwa upya maumivu
niliyopata mwanzo kutoka kwa kaka yake Happy kisha waliniburuza na kunisokomeza
kwenye gari yao tukaondoka kwenda kuendelea kusherehekea Valentine day kituoni.
Jamani Valentine yangu mimi.
Kufika kituoni maelezo niliyopata ni kuwa
mimi ndiye niliyemgonga Angella na pikipiki kisha nikakimbia. Kumbe yule boda
boda alieyemgonga Angella alitambulika kwa jina la Riziki na kumbe polisi
walifika hospitali na kukuta jina langu niliyemleta pamoja na maelezo ya wazazi
wa Angella na nesi aliyenipokea nikadhaniwa ni mimi. Kesi ikanivaa nikaendelea
kusherehekea Valentine. Nikiwa kituoni sikuweza hata kutembea kwa maumivu,
nikapelekwa hospitali nikiwa chini ya ulinzi. Baada ya vipimo nikagunduliwa
nimevunjika mguu, nikabaki hospitali nikisherehekea valentine yangu.
Polisi waliniambia nikipata ahueni nina
kesi ya kujibu! Kesi ya kupakaziwa! Wema wangu umeniponza! Msaada wangu umekua
shubiri! Nikaendelea kusherehekea Valentine!
Majira
ya kama saa moja jioni alikuja rafiki yangu ambae nilikuwa nafanya nae kazi
akanipa taarifa kwamba bosi amempigia simu akampa maagizo aniletee kwamba
sipaswi tena kuonekana kazini! Jamani mimi! Nitaishije! Basi nikaendelea
kusherehekea Valentine. Nilimtuma rafiki yangu aende akaweke ghetto langu sawa
ambalo nililiacha hovyo anichukulie na visenti vya kunisaidia. Aliondoka
akarudi baada ya muda, kumbe hakuruhusiwa kuingia chumbani kwangu. Baba mwenye
nyumba alimkatalia, alikifunga chumba akinisubiri nije kuchukua vitu vyangu tu!
Nikaendelea kusherehekea Valentine.
Basi Valentine yangu ikaisha hivyo.
Baada ya wiki siku nne niliruhusiwa kutoka
pale hospitali lakini nilipelekwa moja kwa moja mahabusu kusubiri kesi
inayonikabili. Nilikua sijapona ila nilipaswa kuwa narudi hospitali.
Nilikaa
mahabusu miezi 6 bila ya kesi yangu kusomwa. Niliteseka sana. Tofauti na ndugu
zangu waliokuwa wanakuja kuniona mpenzi wangu Happy hakutokea kabisa! Lakini
bora hakutokea, alichonifanyia yeye na kaka yake nisingetamani kumwona. Yaani
Happy wewe nakulaani kabisa, sitaki hata nikuone hata ukifa sitakuja kukuzika
na hata mtu akinionesha kaburi lako kwa bahati mbaya nitalifuata na kulikojolea
mwanaharamu kabisa. Wazazi wa Angella niliyempa msaada na Angella mwenyewe
sikuwaona kabisa kwa kipindi chote wala sikupata habari yoyote kuwahusu.
Niliachiwa
huru baada ya kukosekana kwa mashtaka dhidi yangu kwa kipindi chote nilichokua
mahabusu. Nilitoka nikaingia uraiani, sina pa kuishi, sina hela, sina kazi,
sina pa kupata chakula na sina mpenzi wangu Happy. Vyote vilipotea siku ile ya
Valentine. Labda bado naisherehekea Valentine. Valentine day ina maana mbaya
kwangu. Naichukia Valentine day. Iliniharibia kila kitu Riziki mimi.
Nakuruhusu
upige stori zote na mimi lakini ukitaka kuvuruga amani we nitajie siku ya
Valentine uone. Nakuhakikishia nitakuonesha hasira yangu. Hata kama sikumudu
lazima nitafanya kitu ambacho utajua huwa nina hasira kiasi gani na siku ya
Valentine. Naichukia sana, sipendi kabisa kuisikia Valentine day.
Jifunze:
Kuna
watu wana historia ya kuumiza ambayo imewatokea kwa kipindi fulani. Inawezekana
ni jambo la kuumiza sana ambalo ndani yake linaweza kumpa mtu maumivu au hasira
kali. Kila mtu ana namna ya kukabili hasira na maumivu yake, huwezi kujua mtu
alivyo unavyojitahidi aidha kumpa faraja au kumshauri pengine unamtonesha
kidonda au unaamsha maumivu na hasira, basi njia sahihi ni kuepuka kabisa
kulijadili na kubadili mada.

Post a Comment