ASASI ZA KIRAIA ZAANZISHA KUCHANGISHA FEDHA KWA AJILI YA KUNUNUA VIFAA VYA WAHUDUMU WA AFYA KUJIKINGA NA CORONA | Tarimo Blog


Charles James, Michuzi TV

Katika kuunga mkono juhudi za serikali kwenye mapambano dhidi ya ugonjwa wa Corona, Asasi za Kiraia zimeanzisha kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kusaidia mapambano hayo.

Kampeni hiyo imelenga kuchangisha fedha kwa ajili ya kuwanunulia vifaa vya kujikinga na ugonjwa wa Corona wahudumu wa afya nchini.

Akizungumzia kampeni hiyo, Mkurugenzi Mtendaji wa AZAKI, Francis Kiwanga amesema wao kama Asasi za Kiraia wameguswa na mapambano ya ugonjwa huo hivyo wakaona ni vema pia kutumia ushawishi wao kuchangisha fedha lengo likiwa kununua vifaa mbalimbali kwa ajili ya wahudumu wa afya kama ambavyo Shirika la Afya Duniani (WHO) wameelekeza.

" Tunafahamu vita ilivyo kubwa dhidi ya ugonjwa huu hatari duniani, pamoja na kwamba tulishatoa fedha kama sehemu ya mchango wetu lakini tumeguswa tena kuendelea kushirikiana na serikali katika mapambano haya ya Corona.

Hivyo niwasihi wananchi mbalimbali, mashirika, wadau wa maendeleo tuungane kuchangia kampeni yetu hii ambapo fedha zitakazopatikana zitatumika kuwanunulia wahudumu wa afya vifaa vya kujikinga na ugonjwa huu," Amesema Kiwanga.

Aidha Kiwanga amesema kampeni hiyo imeanza April 22 na itakamilika Mei 5 ambapo watakabidhi vifaa ambavyo vimepatikana kutokana na michango iliyochangwa.

" Vifaa ambavyo tutanunua ni mavazi maalum ya watoa huduma, miwani maalum ya upasuaji, Barakoa za Upasuaji, Barakoa N95, Glavu za Upasuaji, Sabuni za kunawa mikono na vitakasa mikono.

Niwaombe wote watakaoguswa kutuma mchango watume kwenda namba 0762 767237 ambapo jina lililosajiliwa ni Foundation for Civil Society au ambaye atanunua vifaa pia tutashukuru sana na tutamuomba avilete ofisini kwetu," Amesema Kiwanga.
 Mkurugenzi Mtendaji wa AZAKI, Francis Kiwanga Akizungumzia kampeni ya kuchangisha fedha kwa ajili ya kununua vifaa vya kujikinga na maambukizi ya Corona kwa watoa huduma bwa afya.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2