Mahakama yaamuru Zitto akamatwe, hukumu yake mwezi ujao | Tarimo Blog

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV.

MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Kisutu, imetoa hati ya kukamatwa kwa Mbunge wa Kigoma Mjini, Zitto Kabwe kupitia tiketi ya Chama cha ACT- Wazalendo, baada ya kushindwa kufika mahakamani hapo  bila ya kutoa taarifa yoyote.

Amri hiyo, imetolewa leo Aprili 29,2020 na Hakimu Mkazi Mkuu, Huruma Shaidi wakati kesi hiyo ilipokuja kwa ajili ya kupangiwa tarehe ya hukumu, kufuatia upande wa mashtaka kufunga kesi yao na mshtakiwa Zitto kumaliza kujitetea.

Aidha mahakama imesema, Mei 29 mwaka huu itatoa hukumu ya kesi ya uchohezi inayomkabili Kiongozi huyo, baada ya kusikiliza mashahidi 15 wa upande wa mashtaka na mashahidi nane wa upande wa utetezi.


Katika kesi hiyo Upande wa mashtaka umewakilishwa na Wakili  wa Serikali Mkuu, Tumaini Kweka, huku upande wa utetezi haukuwa na uwakilishi wowote akiwemo mshtakiwa mwenyewe (Zitto) kutokuwepo.

Zitto anatetewa na Wakili Peter Kibatala na Jebra Kambole.


"Hakuna mtu aliyekuja na kusema mshtakiwa yuko wapi natoa hati ya kukamatwa kwa mshtakiwa," alisema Hakimu Shaidi

Katika kesi ya msingi Zitto anakabiliwa na mashitaka matatu ya uchochezi ambapo, anadaiwa Oktoba 28, 2018 akiwa katika mkutano na waandishi wa habari, uliyofanyika katika Makao Mkuu ya ofisi ya Chama cha ACT Wazalendo alitoa maneno ya uchochezi yenye kuleta hisia ya hofu na chuki.

Inadaiwa kuwa mshitakiwa alitamka kuwa ‘’…watu ambao walikuwa ni majeruhi katika tukio la mapambano baina ya wananchi na Polisi wakiwa wamekwenda hospitali kupata matibabu katika kituo cha afya Nguruka, Polisi wakapata taarifa kuwa kuna watu wanne wamekwenda hospitali kituo cha afya Nguruka kupata matibabu wakawafuata kule wakawaua..’’

Katika shitaka la pili ilidaiwa Oktoba 28, mwaka huu maeneo ya Kijitonyama katika makao makuu ya chama hicho, jijini Dar es Salaam, alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’…lakini tumefuatilia kwa kina jambo hili, taarifa ambazo tumezipata kutoka kijijini Mpeta-Nguruka, Uvinza ni mbaya, ni taarifa ambazo zinaonesha wananchi wengi sana wameuawa na jeshi la Polisi pamoja na kwamba afande Sirro amekwenda kule, haijatoa taarifa yoyote kuhusu wananchi…kama hawa wanyantuzu walivamia eneo la Ranchi kuna taratibu za kisheria za kuchukua na sio kuwauwa, wananchi wengi sana wamekufa…’’

Ilidaiwa kuwa katika tarehe hiyo hiyo, Zitto alitoa maneno ya uchochezi dhidi ya Jeshi la Polisi akisema ‘’… Tumekuwa tukifuatilia kwa kia yanayojiri yote huko Uvinza tunasikitika kusema kuwa taarifa tunazozipata kutoka Uvinza zinaogofya mno, kwani tunaambiwa kuwa wananchi zaidi ya 100 wa kabila la Wanyantuzu wamepoteza maisha kwa kupigwa risasi na Polisi, wengine wakisema kuuawa hata wakiwa kwenye matibabu hospitalini baada ya kujeruhiwa kwenye purukushani na jeshi la polisi…’’
Mhe.Zitto Kabwe.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2