RUFAA YA DC CHEMBA, YATUPWA AAMRIWA KUTOA MATUNZO YA MTOTO | Tarimo Blog

Na Karama Kenyunko, Michuzi TV
MAHAKAMA ya Wilaya ya Ilala jijini Dar es Salaam, Imetupilia mbali rufaa iliyokatwa na Mkuu wa wilaya ya Chemba Simon Odunga kupinga hukumu ya Mahakama ya Mwanzo Ukonga iliyoamuru Odunga kutoa Sh. Milioni saba kama sehemu ya gharama ya matunzo ya kumsomesha mtoto wake.

Uamuzi huo umetolewa leo Aprili 29, 2020 na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Wilaya ya Ilala, Glory Nkwera ambaye amekazia hukumu hiyo na kumtaka Odunga kutoa kiasi hicho cha fedha Kama ilivyoamuliwa na mahakama ya mwanzo ya Ukonga ambapo fedha hizo ni nusu ya gharama za matunzo aliyotumia mkewe Madelina Mbuwuli  kumsomesha mtoto wao kuanzia darasa la kwanza hadi kidato cha sita.

Pia mahakama imesema ndoa baina ya wawili hao itabaki kama ilivyo sasa kwa sababu haijaona mahali ambapo mkatiwa rufaa Madelina alikosea bali mrufani  Odunga ndiye alikosea kwa kumtelekeza mwenzake na kuondoka nyumbani hivyo Ndoa ibaki kama ilivyo. 

Ameongeza kuwa mrufani Odunga alitakiwa kuonesha sababu za msingi ambapo angeonyesha Medelina alikosea na aliweza kufanya makosa yaliyokinyume cha sheria, hivyo mahakama imeona ndoa yao haijavunjika na hakuna sababu za kusema ndoa imevunjika na haiwezi kurekebishika. 

Aidha mahakama imemuamuru Odunga kutoa kiasi cha Sh. 100,000 kila mwezi ikiwa ni gharama za matunzo ya mtoto wao. 

Hata hivyo Hakimu Nkwera amesema iwapo kuna mtu hajaridhika na hukumu hiyo haki ya kukata rufaa ipo wazi

Awali Mkuu huyo wa Wilaya, Odunga alifungua kesi ya talaka namba 181 ya mwaka 2019 katika mahakama ya mwanzo Ukonga  ili waweze kumtaliki mkewe Madelina lakini mahakama ya Mwanzo ya Ukonga katika hukumu yake ilikataa ombi hilo badala yake ikamtaka alipe kiasi hicho cha fedha ikiwa ni sehemu ya gharama za ada alizoutumia mkewe huyo zaidi ya Sh milioni 13 kwa kumsomesha mtoto wao.

Kufuatia hukumu hiyo, Novemba 5, mwaka jana Medelina alifika Mahakama  Ukonga ili kuweza kujua utekelezaji wa hukumu hiyo ndipo alipokumbana na rufaa ya Odunga ambayo hata hivyo mahakama imeitupilia mbali.

Katika hukumu ya Ukonga  Odunga pia alitakiwa kutoa Sh 100,000 kila mwezi kwa ajili ya matunzo ya mwanaye na pia iliamuru mtoto huyo  kwa kuwa ana umri wa zaidi ya miaka 18 ana haki ya kukaa mahali anapotaka.

Odunga na Mbuwuli walifunga ndoa kanisani na kupata cheti cha ndoa.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2