UGONJWA WA CORONA (Covid-19) WAIHIRISHA SHEREHE ZA MEI MOSI 2020 ZANZIBAR | Tarimo Blog



TAMKO LA SHIRIKISHO LA VYAMA VYA WAFANYAKAZI ZANZIBAR KUPITIA VYOMBO VYA HABARI  KATIKA KUADHIMISHA SIKU SIKU YA WAFANYAKAZI DUNIANI 2020
Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi  

Kama wengi wetu tunavyoelewa kwamba  leo ni  tarehe 01-05-2020 ambayo pia hujulikana kama Siku ya Mei Mosi. Siku ambayo Wafanyakazi wa Zanzibar kila Mwaka hushirikiana na Wafanyakazi wenzao Duniani kuadhimisha Siku ya Wafanyakazi Duniani

Kwa msingi huo hatunabudi  kumshukuru Mwenyezi Mungu mwingi wa Rehema na Mwenye kurehemu kwa kutufikisha siku ya leo tukiwa wazima na amani ya nchi yetu. Aidha tunawapongeza Viongozi wetu wa Serikali hususan Mhe. Rais kwa uongozi wake uliobora , Waajiri na wananchi kwa kushirikiana nasi katika maadhimisho haya 

Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi  
Siku hii ni miongoni mwa Siku maarufu Duniani ambayo kihistoria inaadhimishwa kutokana na tukio lililotokea huko Marekani siku nyingi zilizopita ambako Wafanyakazi waliandamana kwa amani kwa Madhumuni ya  kupinga madhila waliyokuwa wakifanyiwa katika sehemu zao za kazi.

Kama sote tunavyokumbuka  kwamba, Maadhimisho haya kila mwaka huadhimishwa kwa ratiba ndefu inayojumuisha shughuli mbali mbali, hata hivyo kwa mwaka huu tumelazimika kuakhirisha Ratiba yote kutokana na Mripuko ya Maradhi ya CORONA yaliyoingia nchini mwetu katikati ya Mwezi wa Tatu.

Badala yake tumeamua kutowa tamko hili la wafanyakazi kwa lengo kuadhimisha tukio hilo na kutathmini haki na mazingira ya kazi kwa kipindi cha Mwaka mmoja uliopita kama ilivyo lengo kuu la Maadhimisho ya Mei Mosi kila mwaka.

Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi  
Kwa vile Mwaka huu 2020 unatarajiwa kuwa wa mwisho wa Uongozi wa Awamu ya Saba (07) inayoongozwa na Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Shirikisho limekusudia kufanya tathmini kwa uchache juu ya uongozi wa Awamu hii ili kutambua mchango wake katika maendeleo ya sekta ya ajira pamoja na changamoto zilizojitokeza ambazo  kwa maoni yetu zinahitaji kufanyiwa kazi
Kwa msingi huo, na kwa niaba ya Wafanyakazi wa Zanzibar nachukuwa fursa hii kuainisha baadhi ya mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya ajira kwa kipindi cha Awamu ya Saba ya Uongozi wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar  ambayo miongoni mwa mengine ni

1.      Kutunza amani na utulivu wa nchi na kuwawezesha wananchi kufanya shughuli zao za kawaida
2.      Kuimarika kwa fursa za ajira nchini ambapo zaidi ya vijana 11, 000 wameajiriwa katika Wizara na taasisi za Serikali katika kipindi hicho
3.      Kuundwa kwa Sheria ya Utumishi na ya Mwaka 2011 na Kanuni za Utumishi za 2014 kwa lengo la kuweka mifumo bora ya utumishi Nchini pamoja na kuundwa kwa Wizara na taasisi maalum zinayoshughulikia Utumishi wa Umma
4.      Kuimarishwa kwa maslahi ya wafanyakazi katika sekta ya umma, binafsi na Sekta isiyo rasmi hasa mishahara pamoja na kurekebishwa mifumo ya utumishi na uwajiri
5.      Kuimarishwa kwa Miundombinu ya Nchi na sehemu za kazi hasa za utowaji wa huduma kulikozingatia afya na usalama sehemu za kazi na utowaji wa huduma bora nchini
6.      Serikali kuendelea kuimarisha mifumo ya hifadhi ya jamii kwa wananchi hasa wazee kwa kutunga Sheria na Sera za kuwalinda na kuimarishwa, kutoa pencheni na kuimarisha viwango vya chini vya pensheni za wastaafu.
7.      Utayari wa Serikali kuzungumza na wafanyakazi na viogozi wa Vyama vya wafanyakazi yanapotokea matatizo ya kikazi au mambo yanayohusu haki za wafanyakazi
8.      Kuondoa michango katika  huduma za afya kwa wajawazito na watoto wadogo na katika sekta  za elimu kuanzia Msingi hadi sekondari ili kupunguza mzigo kwa wafanyakazi na wananchi
Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi  
Kama tunavyoelewa kwamba kama ilivyo mifumo ya maisha kila ambapo kunamafanikio hapakosi changamoto kwa hivyo baadhi ya changamoto ambazo kwa maoni yetu zikifanyiwa kazi mafanikio zaidi yatapatikana ni kama ifuatavyo
1.      Kuwepo kwa Uwakilishi wa wafanyakazi katika vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria ya utumishi kama vile Kamisheni na Tume za Utumishi
2.      Vyombo vilivyoundwa kwa mujibu wa sheria za kazi na Utumishi wa umma vifanyekazi zake vilivyopangiwa kikamilifu  ikiwemo kukutana kama vile Bodi ya Ushauri ya mambo ya kazi, bodi ya mishahara, kamati za DHU  na OSH pamoja na Chombo cha Majadiliano cha Kitaifa
3.      Kuchukuliwa hatua kwa Waajiri wasilipa  mishahara kwa mujibu wa amri ya Serikali au kulipa kinyume na kima cha chini kilichoamriwa na serikali
4.      Kulipwa kwa Malimbikizo makubwa ya madeni ya haki za wafanyakazi ikiwemo tofauti za Mishahara ya mishahara na stahiki nyengine na wafanyakazi wa Serikali na taasisi za Serikali
5.      Kufanyiwa kazi Changamoto za marekebisho ya mishahara katika mashirikika ya umma na taasisi zinazojitegemea ambazo hadi sasa zinaendeleza manung’guniko kwa baadhi ya wafanyakazi wa Taasisi hizo
6.      Kurejeshwa kwa Kikokotoo cha mishahara ya Watumishi wa Umma kilichowekwa 2012 ambacho kiliondoa kabisa malalamiko ya wafanyakazi katika mishahara yao na kuweka uwazi katika malipo ya Mishahara
7.      Taasisi za serikali kuajiri kampuni za utowaji wa huduma (outsourcing) zenye uwezo , viwango na zenyekuzingatia sheria za kazi na za nchi katika haki na maslahi ya wafanyakazi
8.      Serikali za mitaa kuwa na watumishi wenye kujali taaluma za wafanyakazi zao kitaaluma (Walimu, madaktari) na kutoruhusu kuwepo wafanyakazi wengi wa muda  (part time ) kinyume na miongozo ya Serikali

Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi 
Kauli mbiu ya maadhimisho ya Mei Mosi kwa mwaka huu ni kama ifuatavyo
“WAFANYAKAZI TUNAWAJIBU KUPAMBANA NA JANGA LA KORONA NA KUSHIRIKI KATIKA UCHAGUZI MKUU KWA AMANI”

Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar (ZATUC) kwa niaba ya  wafanyakazi limeamua kuweka ujumbe huu kutokana na hali halisi iliyopo hapa nchini juu ya mripuko wa maradhi hatari ya CORONA ambayo hadi sasa imeonekana kwamba hayana Kinga wala dawa

Kwa upande wa wafanyakazi kupitia Shirika la kazi duniani linahesabu maradhi haya kama ni maradhi ya sehemu za kazi yaani “Occupational disease” kwa vile limeathiri zaidi wafanyakazi katika sehemu zao za kazi na athari  kubwa ya maradhi haya ni kwa ajira, uchumi na ustawi wa wafanyakakazi  na vipato vyao

Hivyo basi, ujumbe una lengo la kuwakumbusha wananchi hasa wafanyakazi kuchukuwa kila aina ya hatua kuhakikisha janga hili linaondoka nchini kwa kufuata maelekezo yote yanayotolewa na viongozi na wataalamu wa afya juu ya namna ya kujikinga na kuwakinga wenzetu makazini na majumbani juu ya janga hili kwa vile ni hatari kwa Ajira zetu, fursa za ajira za vijana wetu, kipato chetu, haki na maslahi yetu pamoja uchumi na ustawu wa taifa letu

Kwa upande mwengine Taifa letu mwaka huu linakabiliwa na Uchaguzi mkuu ambapo tukichukulia uzowefu wa siku zilizopita inapofika muda kama huu kunajitokeza baadhi ya Viongozi wa kisiasa, na kidini na wafuasi wao kupandikiza chuki na kushajiisha uvunjifu wa amani. Jambo ambalo huvuruga mifumo ya maisha ya wafanyakazi, kuathiri tija na kuzorotesha utowaji wa huduma

Kwa msingi huo na kwa kupitia ujumbe huu tunakusudia kuwakumbusha wananchi hasa wafanyakazi kwamba tunawajibika kikamilifu katika kuilinda amani ya nchi yetu kwa kupiga kura kwa amani, kwani huo ndio msingi wa utawala bora katika jamii. Kinyume chake tunaweza kuvuruga maendeleo mengi yaliyopatikana nchini kwetu kwa kufanya mzaha na amani

Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi 
Kwa kumalizia tumapenda kutoa maoni yetu katika siku hii muhimu kwetu kwa wadau kutokana na hali inavyoendelea katika sekta ya ajira nchini kwetu kama ifuatavyo:-

1.      Serikali
Tunaipongeza sana Serikali kwa namna ya hatua ilizochukuwa kupambana na janga la Corona hata hivyo tunaelewa kwamba sio rahisi kuhibiti ugonjwa huu ambao hauna kinga. Hata hivyo pamoja na hali iliyojitokeza tunaiomba Serikali yetu kuyafanyia kazi mambo yafuatayo :

a)       Kuendelea na jitihada  kutimiza ahadi za Mhe.Rais ya kuongezwa kwa Mishahara na mafao mengine inatekelezwa kabla ya kuondoka kwake madarakani yanafanyiwa kazi
b)       Kuendelea kuhakikisha watumishi wa afya, wanaotoa huduma kwa wagonjwa na waandishi wa habari ambao wapo katika mstari wa mbele kupambana na janga la  CORONA wanapatiwa kinga, motisha na bima ya maisha kutokana na mazingira wanayofanyia kazi
c)        Kuendelea kufanya udhibiti wa maeneo ambayo bado inaonekana hayajadhibitiwa ya uingiaji wa watu kutoka nje na kuwachukulia hatua bila ya muhali wanaokiuka taratibu zilizowekwa na Serikali
d)       Kuendelea kuhakikisha kwamba maeneo ya kazi ya umma yanawekewa hatua za tahadhari ikiwemo vifaa vya usafi,  vipima joto, uvaaji wa barkoa na kuondoa mkusajiko sehemu za huduma
e)       Kuendelea kuhakikisha kwamba waajiri wanapohitaji kufanya hatua zozote za kiajira kwa wafanyakazi ambao ajira zao zimeathirika na janga hili, ni lazima wapitie taratibu za kisheria ikiwemo majadiliano na mashauriano ya pamoja na wafanyakazi kwa mujibu wa Sheria katika hatua wanazochukuwa
f)          Serikali ifanye utafiti wa kiwango cha wafanyakazi walioathirika na janga hili kwa kupoteza kazi kupitia au kupunguwa kwa kipato chao ili iwasaidie kupitia mifumo ya hifadhi ya jamii
g)       Kwa vile janga hili kwa kiasi kikubwa linaathiri ajira na mazingira yake, Serikali ihakikishe inazishirikisha Jumuiya za ajira ikiwemo Vyama vya Wafanyakazi katika mapambano haya ikiwemo kamati za Kitaifa

2.      Waajiri

a)     Kuhakikisha kwamba maeneo yao ya  kazi yanawekewa hatua zote za  tahadhari ikiwemo vifaa vya usafi na  vipima joto ili kudhibiti maambukizi zaidi ya COVID-19
b)     Kuhakikisha watumishi wao wanapata huduma za dharura na sehemu za dharura endapo kutajitokeza wanaoshukiwa kuwa na dadili za maradhi yenye ishara zinazolingana na maradhi ya CORONA
c)      Kuhakikisha kwamba hakuna mfanyakazi atakaekosa haki yake na maslahi yake kwa kisingizio cha CORONA bali wafuate Sheria katika kuchukuwa hatua yoyote kwa wafanyakazi ikiwemo kuwasiliana na ofisi ya Kamishna wa kazi kabla hawajachukua hatua yoyote
d)     Kuhakikisha kwamba wafanyakazi wao wanajikinga na maradhi hayo kwa kuepuka mikusanyiko kazini na wanachukua hatua zote za tahadhari ya maradhi hayo

3.      Wananchi

a)     Kukubaliana na kufuata maagizo ya Serikali na wataalamu wa afya kuhusu  kujikinga sisi wenyewe na na familia zetu na janga hili
b)     Kushirikiana na Serikali na wadau wengine katika kuhakikisha janga hilo linaondoka nchini iwe kwa kujitolea hali zao na mali zao kuongezea nguvu za serikali katika mapambano hayo
Ndugu Viongozi, Wafanyakazi na Wananchi 
Mwisho kabisa Kwa kumalizia tunapenda kutoa shukurani za dhati kwa uongozi wa Serikali kuu hususan Mhe. Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa uongozi wake ulio mwema ambao umeleta maendeleo mengi nchini na manufaa kwa wafanyakazi ,
Aidha tunawapongeza viongozi wa wizara ya kazi hususan Mhe. Waziri, katibu Mkuu na Kamishna wa Kazi kwa mashirikiano yao kwa Vyama vya Wafanyakazi. Kwa uzito huo huo tunawapongeza waajiri na wafanyakazi wote kwa ujumla kwa mashirikiano wanayotoa kwa wafanyakazi na vyama vya wafanyakazi katika  kufanikisha shughuli zatu
Tunaomba tushirikiane kumuomba Mwenyezi Mungu atuondoshee janga hili ili tuweze kurudi katika mfumo wa maisha yetu ya kawaida huku tukichukua tahadhari zinazotolewa na Viongozi wa Serikali na wataalamu wa Afya juu ya kujuikinga sisi binafsi na kuwakinga wengine dhidi wa janga hili la CORONA

Kwa niaba ya Shirikisho la vyama vya wafanyakazi Zanzibar Nawashukuru sana kwa kunisikiliza

KWA MSHIKAMANO TUTASHINDA
SOLIDARITY FOR EVER -Mshikamano Daima

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2