WAWILI WAFARIKI DUNIA ARUMERU KUFUATIA MVUA ZINAZOENDELEA KUNYESHA | Tarimo Blog

Na Woinde Shizza, Arusha
WATU wawili wamefariki dunia kufuatia mvua zinazoendelea kunyesha kwa siku tatu mfululizo katika wilaya ya Arumeru huku nyumba zaidi ya 50 kuharibika kutokana na mvua hizo.

Akitoa taarifa za hali ya mwendendo wa mvua hizo mara baada ya kufanya ziara na kushiriki shughuli za uokoaji, Mkuu wa wilaya ya Arumeru  Jery Muro amesema kuwa mvua hizo  zimeleta madhara makubwa kwani zimesababisha vifo vya watu wawili ambao wamefariki dunia leo Alhamisi   April 23 Katika Halmashauri ya Meru mkoani Arusha.

Muro amewataja waliofariki dunia kutokana na mvua hizo  kuwa ni  Terevaeli Mirisho Nasari Mwenye umri wa  miaka 65 Mkazi wa kitongoji cha meto kijiji cha mulala kata ya songoro, ambapo amefariki dunia Asubuhi baada ya maporomoko ya Udongo kutoka mlimani kuvunja ukuta wa chumba alichokuwa amelala na tayari mwili wake umepatikana na kupelekwa katika hospitali ya Mount Meru.

Aidha ametaja kifo  kingine cha mtoto alietambuliwa kwa jina la  Tumaini Simon Mwenye umri wa miaka 3 wa kijiji cha Valeska Kitongoji cha Mwamko, ambae amesombwa na mafuriko ya maji wakati akiwa katika harakati za kuokolewa na Mzazi wake ambapo Mzee simon alifanikiwa kuokoa mtoto mmoja na mwingine kufariki dunia na mwili wa mtoto tumaini umepatikana na taratibu za mazishi zinaendelea.

Amebainisha Katika Mvua hizo  Nyumba zaidi 50 zimeharibiwa huku zingine zikianguka kutokana na maji kuwa mengi.

Ameongeza kuwa tayari ameshaziagiza kamati za maafa zinazoongozwa na wakurugenzi wa Halmashauri za Meru na Arusha kushirikiana na wananchi katika kutoa misaada ya haraka katika familia hizo.

Amesema hiyo yote ni njia ya kuweza   kunusuru familia hizo ikiwemo kuwatafuta makazi ya muda 

 Alitumia muda huo kutoa  tahadhari ya wananchi waliojenga pembezoni mwa milima na miinuko mikubwa pamoja na wale waliojenga Katika maeneo yanayokumbwa na mafuriko kuondoka katika maeneo hayo  haraka kabla ya madhara zaidi maana mvua bado zinaendelea kunyesha.
 Wananchi wakiangalia nyumba iliyobomoka.
 Mkuu wa wilaya ya Arumeru  Jery Muro akiangalia madhara yaliyojitokeza mara baada ya mvua kunyesha na kudondosha baadhi ya nyumba katika wilaya ya Arumeru.
Wananchi wa Maeneo ambayo yameathirika na mvua zinazoendelea kunyesha wilaya ya Arumeru mkoani Arusha wakiwa katika moja ya nyumba zilizopata madhara baada ya  mvua kunyesha na kuleta madhara ya kuangusha nyumba. 
Picha na Woinde Shizza, Arusha.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2