BALOZI SEIF ALI IDDI ASHAURI KAMPUNI ZA UWEKEZAJI | Tarimo Blog

Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Royal Group Ndugu Hassan Mohammed Raza Kushoto akimuonyesha Ramani ya Hoteli Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif  alipofanya ziara fupi.
MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi amezishauri Kampuni za Uwekezaji katika Sekta ya Biashara kuangalia uwezekano wa Kujenga Hoteli ya Kitalii katika Uwanja wa Ndege wa Pemba kwa lengo la kutoa huduma kwa wasafiri na hata Wananchi wanaotumia Uwanja huo.
Alisema mfumo wa huduma za Mahoteli unaokuwepo katika Viwanja mbali mbali vya Ndege Duniani hulenga kuwaondoshea usumbufu Wasafiri wa  Anga kuzitafuta huduma hizo maeneo ya Mijini kwa vile baadhi ya Viwanja hivyo huwepo Ng’ambo ya Miji.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa ushauri huo alipofanya ziara fupi ya kukagua Maendeleo ya Mradi wa Ujenzi wa Hoteli ya Kimataifa ya  Golden Tulip Airport Hotel iliyopo pembezoni mwa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume ulio chini ya Kampuni ya Royal Group.
Alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Taasisi zake za Uwekezaji ina nia ya kuona fursa ya ujenzi wa Hoteli ya Kitalii katika Uwanja wa Ndege wa Pemba inachangamkiwa na Wafanyabiashara wenye uwezo kwa kuanzisha Mradi huo muhimu unaoweza kutoa huduma sambamba na ajira kwa Vijana.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliupongeza Uongozi mzima wa Kampuni ya Royal Group kwa uamuzi wake wa kuanzisha Mradi huo Mkubwa utakaosaidia kuongeza Pato la Taifa, huduma kwa Wasafiri na kwa upande mwengine Ajira kwa Wananchi Wazalendo.
Mapema akimkaguza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar katika maeneo mbali mbali ya Jengo hilo, Mkurugenzi Mtendaji wa Makampuni ya Royal Group Ndugu Hassan Mohammed Raza alisema ujenzi huo unaotarajiwa kuchukuwa Miezi 16 utakamilika ifikapo Mwezi Oktoba Mwaka huu.
Ndugu Hassan alisema ujenzi wa jengo hilo litakalokuwa na Vyumba 62 vya kulala, eneo la kuegesha magari 150 kwa wakati Mmoja linatarajiwa kugharimu jumla ya Dola za Kimarekani Milioni 7.5 sawa na fedha za Kitanzania Zaidi ya shilingi Bilioni 17.1.
Mkurugenzi Hassan alimueleza Balozi Seif kwamba pamoja na mambo mengine Uongozi wa Royal group umezingatia huduma za Michezo kwa kuweka Bwawa maalum la kuogelea pamoja na sehemu za mazoezi kwa wale wasafiri wanamichezo.
Alisema Mradi huo utakapokamilika utatoa huduma kwa Wasafiri wa Anga wanaotumia Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar kwa kuzingatia umuhimu wa usalama wa Abiria unaokwenda sambamba na vile vigezo vya Viwanja vya Ndege vya Kimataifa.
Naye Meneja wa Operesheni wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Zanzibar      {AAKIA} Nd. Haji Haji alisema vifaa Maalum vitawekwa katika Hoteli hiyo vitakavyosimamiwa na Watendaji wa Taasisi zote zinazohusika na masuala ya Uwanja wa Ndege katika kuona Msafiri anapata huduma zinazostahiki.
Nd. Haji alisema usafiri wa Mabasi utawekwa kwa ajili ya kuwahudumia abiria wanaokuwemo ndani ya Hoteli hiyo na kuwafikisha kwenye mlango na ndege wanazosafiria.
Othman Khamis Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
21/07/2020.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2