JAMHURI YABADILI HATI YA MASHTAKA DHIDI YA WASHTAKIWA WANNE | Tarimo Blog




JAMHURI imebadilisha hati ya mashtaka dhidi ya washtakiwa wanne akiwemo mke wa marehemu, mtoto wake, wakili wa kujitegemea na mfanyakazi wa benki ta Stanbick ambapo sasa wanadaiwa kuiba na kutakatisha zaidi ya sh. Bilioni moja.

Washtakiwa hao ambao wamebadilishiwa mashtaka leo Julai 21, 2020 ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber Ltd, Khairoon Jandu ambaye ndio mke wa marehemu, Zainabu Tharia binti yake, Wakili Mohamed Majaliwa na Meneja wa benki ya Stanbic Inrahim Sangawe.

Mapema leo asubuhi, washtakiwa hao walifikishwa mbele ya Hakimu Mkazi Casian Matembele lakini upande wa mashtaka aliwasilisha maombi ya kuondoa kesi hiyo mahakama chini ya kifungu cha sheria cha 90 (1) cha CPA kwa kuwa DPP hana nia ya kuendelea na mashtaka dhidi yao(Nolle Prosequi). 

Hata hivyo, washtakiwa hao walikamatwa upya na kusomewa mashtaka mapya.

Akisoma hati ya mashtaka wakili wa serikali, Faraji Ngukah amedai katika muda tofauti kati ya Januari na na Juni 2020 katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja kwa kudhamilia waliunda genge la uhalifu, kwa lengo la kughushi na kuiba fedha.

Katika shtaka la pili imedaiwa, Januari 16, 2017 katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam washtakiwa khairoon Jandu, Majaliwa na Sangawe walighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka zilizoonesha kuwa ni nyaraka halali za kikao cha Kampuni ya Jandu huku wakijua si kweli. 

Aliendelea kudai katika kosa la tatu washtakiwa hao kasoro Zainabu walighushi saini ya Inderjit Jandu katika nyaraka za kampuni zinazoonesha amechaguliwa kuwa Mkurugenzi wa kampuni hiyo akionesha ni nyaraka halali huku akijua si kweli.

Washtakiwa hao pia wanadaiwa Mei 25, 2019 katika jiji na mkoa wa Dar es Salaam wakiwa na nia ya udanganyifu walighushi saini ya Inderjit Jandu wakionesha kuwa amehamishia hisa za kampuni kwa Khairoon huku wakijua si kweli.

Shtaka jingine la kughushi linalomkabili Khairoon ni la nyaraka za wosia ulioandikwa na Inderjit akionesha ni wosia halali huku akijua si kweli.

Ngukah aliendelea kudai kuwa katika shtaka la sita, saba na nane Khairoon alitoa nyaraka za uongo kwa BRELA zilizoonesha kuwa ni nyaraka halali za vikao vya kampuni ya Jandu zilizoonesha kuwa amechaguliwa kuwa Mkurugezi wa kampuni hiyo na pia amehamishiwa hisa za kampuni huku akijua kuwa nyaraka hizo si za kweli.

Aidha katika shtaka la tisa washtakiwa wote wanadaiwa katika tarehe tofauti mwaka 2020 waliiba Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Constructions and Plumber. 

Mshtakiwa Sangawe pia anadaiwa kati ya mwaka 2019 na 2020 akiwa ameajiriwa kama meneja wa benki ya Stanbic alishindwa kutumia mbinu zote kuzuia wizi wa kiasi hicho cha fedha kilichokuwa kimehifadhiwa katika benki hiyo.

Katika kosa la mwisho la utakatishaji inadaiwa katika ya Januari 2019 na Juni 2020 jijini Dar es Salaam washtakiwa wote kwa pamoja walijipatia kiasi cha Sh 1,033,860,100 mali ya Kampuni ya Jandu Construction huku wakijua kuwa fedha ni zao la kosa tangulizi la wizi.

Hata hivyo, washtakiwa hawakuruhusiwa kujibu kitu chochote mahakamani hapo kwa kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza kesi za uhujumu uchumi na kwa mujibu wa upande wa mashtaka upelelezi wa shauri hilo bado haujakamili hivyo aliomba tarehe nyingine ha kutajwa.

Hakimu Matembele ameahirisha kesi hiyo hadi Agosti 4, 2020 itakapopoletwa mahakamani kwa ajili ya kutajwa.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2