ASKARI WANYAMA PORI WATAKIWA KUJIEPUSHA NA VITENDO VYA RUSHWA HIFADHINI Inbox | Tarimo Blog

KAMANDA wa Polisi mkoa wa Ruvuma kamishina msaidizi wa Polisi Simon Maigwa, amewataka maafisa na askari wa jeshi la Uhifadhi wa Wanyamapori nchini kujiepusha na vitendo vya rushwa kwa kutoruhusu wafugaji kuingiza mifugo katika mapori na hifadhi zetu za Taifa.

Kamanda Maigwa amesema hayo jana wakati wa hafla fupi kuwavisha vyeo maafisa 10 na askari 5 wa kikosi dhidi ya ujangili na wa pori la akiba Liparamba iliyofanyika katika ofisi za kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kusini Songea.

Amewataka maafisa na askari hao, kutumia weledi,moyo wa kujituma na kutanguliza uzalendo katika kupambana na waharifu mbalimbali wakiwemo majangili ambao wanaingia katika hifadhi na kuuwa wanyama ambao ni urithi na rasilimali kubwa za Taifa.

“nawaomba sana maafisa na askari msijihusishe na vitendo vya rushwa kuruhusu wafugaji na majangili kuingia katika hifadhi zetu,nendeni mkapambane bila kuchoka ili kuhakikisha hifadhi zetu zinabaki salama kwa ajili ya maslahi ya taifa”alisema Kamanda Maigwa.

Pia amewataka watumishi hao kuendelea kuwatumikia watanzania kwa uadilifu na uaminifu ili kujenga taifa na kutokata tamaa katika majukumu yao ya kila siku.

Alisema, moja ya sifa ya askari ni uvumilifu kwa hiyo ni lazima askari atambue pindi adui anapovamia pori anatahitajika kwenda mstari wa mbele kupambana bila kuchoka kwa kuwa wapo baadhi ya maadui waliopitia mafunzo ya jeshi na wengine hata kupata mafunzo ya ugaidi.

Amewakumbusha kuheshimiana kuanzi askari wa cheo cha chini hadi afisa na kufuata maadili ya jeshi wakiwa kazini na nje ya kazi na kushirikiana na vyombo vingine vya ulinzi na usalama kwa maslahi ya taifa.

Kwa upande wake meneja wa Pori la Liparamba wilaya ya Mbinga Nollasco Ngowe alisema, jeshi Ussu limeanzishwa kwa sheria namba 2 ya mwaka 2020 ambayo imeziunganisha taasisi za uhifadhi wa wanyamapori kuwa jeshi moja la wanyamapori na misitu.

Ngowe alitaja taasisi hizo ji Tanapa,Tawa,Tfs na Ncaa ambapo utaratibu unafanyika utakaotoa mwongozo kwa taasisi zote za za uhifadhi, na utaratibu wa mafunzo ya kijeshi utaendelea kuboreshwa ili ili kuongeza uweledi na uwajibikaji kwa watumishi.

Alisema, suala la nidhamu ni nguzo kubwa kwa jeshi lolote,hivyo amewataka kuzingatia sheria na taratibu katika utendaji wa kazi zao za kila siku na amewataka maafisa waliovishwa vyeo kuhakikisha wanawajibika kutoa maelekezo kwa askari,kuwarekebisha tabia na kuwachukulia hatua za kinidhamu kwa askari wanaokiuka maadili ya kazi.

Ngowe alisema, maafisa na askari wanatakiwa kufuata na kuishi mfumo wa taratibu za kijeshi kwa kuwajibika kutekeleza na usimamizi wa kijeshi kama ulivyotolewa na mamlaka ya Tawa.

 Kamanda wa Polisi mkoa wa Ruvuma Simon Maigwa Marwa akikagua gwaride rasmi  katika hafla fupi ya kuwavisha vyeo maafisa 10 na askari 5 wa kikosi dhidi ya ujangili na wa pori la akiba la Liparamba wilayani Mbinga hafla iliyofanyika katika ofisi ya kikosi cha kuzui ujangili kanda ya Kusini Songea,kushoto mkuu wa gwaride hilo mhifadhi mwandamizi Joseph Ruben.

Meneja wa pori la akiba Liparamba wilayani Mbinga Nollasco Ngowe kushoto, akimvisha cheo kipya mhifadhi mwandamizi wa mamlaka ya Uhifadhi Wanyamapori Tanzania(TAWA)Joseph Ruben jana, ambapo maafisa 10 na askari 5 kikosi cha dhidi ya ujangili na pori la akiba Liparamba walivishwa vyeo mbalimbali hafla iliyofanyika katika ofisi za kikosi cha kuzuia ujangili kanda ya kusini Songea.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2