TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI HAIJAMWADHIBU LISSU-NEC | Tarimo Blog

 

*Atakiwa kutofanya Kampeni yake au kwa ajili ya mgombea mwingine kwa siku 7


Na Leandra Gabriel, Michuzi TV


TUME ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imetoa ufafanuzi kuhusu adhabu ya mgombea wa Urais kwa tiketi ya chama cha  CHADEMA, Tundu Antiphas Lissu na hiyo ni baada ya baadhi ya watu kutaka kuaminisha umma wa watanzania kuwa mgombea huyo ameadhibiwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi, jambo ambalo si kweli.


Akizungumza na waandishi wa habari leo jijini Dar es Salaam Katibu wa kamati ya maadili ya kitaifa Emmanuel Kawishe amesema kuwa, kumekuwa na tafsiri isiyo sahihi kuhusu adhabu iliyotolewa na kamati ya maadili ya kitaifa jana Oktoba 2 dhidi ya mgombea huyo, ukweli ni kwamba;


"Lissu ameadhibiwa na kamati ambayo inajumuisha wawakilishi wa vyama vyote vya siasa vinavyoshiriki uchaguzi wa kiti cha Rais, wajumbe 15 kutoka vyama vya ADA-TADEA, CUF, SAU, UPDP, CHADEMA, CHAUMA, CCM, NCCR-Mageuzi, DP, UMD, ACT-Wazalendo, NRA, Demokrasia Makini, ADC, na AAFP hawa ndio waliotoa adhabu kwa bw.Lissu na kamati hiyo pia ina mjumbe kutoka Serikalini na kutoka Tume ambaye kwa muundo wa kamati yeye ndio alikua Mwenyekiti... na ikumbukwe kuwa katika kikao hicho kulikuwa na mawakili wawili kutoka CHADEMA waliosimama na kutetea hoja ya bw.Lissu mbele ya kamati" amesema.


Aidha amesema kuwa kwa kuzingatia adhabu zilizoainishwa katika kanuni ya 5.11 ya uchaguzi wa Rais, wabunge na madiwani ya mwaka 2020 mgombea huyo amepewa adhabu ya kutofanya kampeni kwa siku saba kuanzia Oktoba 3 hadi Oktoba 9, 2020.


"Hii ina maana kuwa haruhusiwi kufanya kampeni yake au kwa ajili ya mgombea mwingine" amesema Kawishe.


Pia amesema kuwa endapo mgombea huyo atadharau uamuzi huo na kufanya kampeni, kamati imepewa Mamlaka ya kuelekeza makosa mengine kwenye vyombo vingine kadri itakavyoona inafaa kama ilivyoainishwa kwenye kanuni ya 5.7(1) ya maadili ya uchaguzi wa Rais, Wabunge na Madiwani ya mwaka 2020 na kufafanua kuwa katika kipindi hiki cha uchaguzi sheria nyingine za nchi zinaendelea kufanya kazi.


Awali amesema kuwa kama ilivyoelekezwa jana katika taarifa ya kamati , malalamiko dhidi ya mgombea yalipokelewa, na Katibu Mkuu wa CHADEMA alipewa taarifa kwa maandishi kwa kuzingatia utaratibu ambao vyama vya siasa na Tume walikubaliana tangu awali.


"Inashangaza kusikia Bw. Lissu akidai taarifa apelekewe yeye mwenyewe kinyume na utaratibu uliowekwa, huku akisahau kuwa tarehe 24 Septemba, 2020 alilalamikiwa na Chama cha SAU kuhusu ukiukwaji wa maadili ambapo barua ilitumwa kwa katibu mkuu wa CHADEMA na walijibu kama kawaida" ameeleza.


Amesema kuwa Tume haipeleki taarifa kwa mgombea mmoja mmoja bali kwa wagombea kupitia makatibu wakuu wa vyama vyao.


"Tume haina na si mtunzaji wa anuani binafsi za wagombea wa nafasi mbalimbali katika chaguzi, Tume inawasiliana na Katibu mkuu na si vinginevyo, hivyo madai ya Bw. Lissu kuwa hajapokea taarifa ya malalamiko hadi leo ni uongo, Chama chake kilipokea taarifa na barua za malalamiko zimemtaja kwa jina." ameeleza.


Mwisho amesema kuwa suala la mgombea huyo limetangazwa kwa sababu ni sehemu ya adhabu aliyopewa na kamati, na kamati hiyo si Tume ya Taifa ya Uchaguzi bali ni chombo kinachoundwa na vyama vyote vyenye wagombea wa kiti cha Urais ikiwemo CHADEMA.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2