DC CHONGOLO ARIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA MADARASA KINONDONI | Tarimo Blog







Muonekano wa vyumba vya madarasa vilivyojengwa.
Mkuu wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo akipata
maelezo kutoka kwa Afisa Elimu Sekondari wa Manispaa hiyo Joseph
Kapere wakati wa ziara ya ukaguzi wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya
madarasa.


MKUU wa Wilaya ya Kinondoni, Daniel Chongolo ameipongeza Manispaa ya Kinondoni kwa kufanikisha kwa asilimia kubwa mpango wa utekelezaji wa miradi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa 110 ikiwa ni katika kuhakikisha kwamba wanafunzi walio ongezeka mwaka huu wanapata madarasa ya kusomea.

Pongezi hizo zimetolewa jana wakati wa ziara yake ya kukagua miradi
hiyo ambayo inatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi huu ambapo
pamoja na mambo mengine amesema kuwa Manispaa chini ya Mkurugenzi wake Aron Kagurumjuli wametekeleza adhma hiyo kwa vitendo.

 Chongolo ameongeza kuwa madarasa hayo yatazinduliwa Februari tano
mwaka huu ikiwa ni siku muhimu ya kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Chama cha Mapinduzi CCM  na hivyo kuanza kutumika.

Ameongeza kuwa Manispaa ya Kinondoni inazitendea haki pesa
zinazotokana na mapato ya ndani jambo linalopelekea kuwepo na
mafanikio makubwa ya miradi inayoanzishwa kwani imekuwa ikikamilika
pasipokuwa na changamoto yoyote.

“ Kwa hili nikupongeze Mkurugenzi pamoja na timu yako, kuna watu
katika Halmashauri nyingine unafanya ziara ya kukagua mradi fulani
lakini ukifika hakuna hata tofali ambalo linaweza kukupa moyo kwamba
kunakitu ambacho kinaendelea, ila hapa Kinondoni leo nimeshuhudia
kuona madarasa ambayo tulikubaliana yanajengwa na kweli yapo na
mengine wanafunzi wanatumia.” Amesema  Chongolo.

Awali Kaimu Mkurugenzi Maduhu Kazi alimueleza Mkuu wa Wilaya Chongolo
kuwa Manispaa inajenga madarasa 110 yenye thamani ya shilingi zaidi ya
Bilioni mbili ambapo kati yake madarasa 46 ni ya shule ya msingi na
madarasa 64 ni ya Sekondari ambayo yote yatakamilika mwisho mwa mwezi
huu na hivyo kuanza kutumika na wanafunzi.

Mstahiki Meya wa Manispaa hiyo Mhe. Songoro Mnyonge amesema kuwa
mafanikio hayo yanatokana na kuwepo kwa uongozi imara wa Mkurugenzi
Kagurumjuli kwani amekuwa akitumia fedha za makusanyo ya ndani kwa
ajili ya kufanikisha miradi ya maendeleo kwa umaridadi mkubwa.

Ziara hiyo ilihuisha kamati ya ulinzi na usalama ya Wilaya, viongozi
wa Chama Cha Mapinduzi ngazi ya Wilaya, mstahiki Meya, Kaimu
Mkurugenzi, Wakuu wa Idara pamoja na wataalamu mbalimbali.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2