JPM AKASIRISHWA NA KITENDO CHA WANAFUNZI BARANGO, UBUNGO KUKAA CHINI ATOA MAAGIZO MAZITO | Tarimo Blog






* Asema ni dhambi kubwa

Na Said Mwishehe, Michuzi TV

KITENDO cha wanafunzi wengi wa Shule ya Msingi Barango iliyopo wilayani Ubungo katika Mkoa wa Dar es Salaam kukaa chini kutokana uhaba wa madawati kimemkasirisha na kusababisha Rais Dk.John Magufuli kutoa maagizo na maelekezo kwa viongozi wa mkoa huo.

Dk.Magufuli amesema haiwezekani katika Mkoa wa  wenye viongozi wa ngazi mbalimbali akiwemo Mbunge wa Ubungo Profesa Kitila Mkumbo ambaye ni mwalimu lakini wanafunzi wanakaa chini.

Akizungumza leo wakati akizindua Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo iliyopo mkoani Kagera, Rais Magufuli ametumia nafasi hiyo kuizungumzia shule ya Barango ambayo ina wanafunzi wengi ambao wanakaa chini kwa kukosa madawati lakini pia kuna madarasa mengine yamebomoka.

"Madarasa mengine yamebomoka, madawati mengine yamevunjika yameachwa bure, Mkuu wa Wilaya yupo, Mkuu wa Mkoa yupo, Mkurugenzi wa Ubungo yupo na bado anakusanya kodi, na Mbunge wa Ubungo yupo tena yuko hapa na ni Profesa tena wa elimu.'' Amesema JPM.

"Simama Profesa (Kitila) wakuone kwenye Jimbo lako, simama hapo mbele wakuone kabisa na ni Profesa wa elimu, anafundisha elimu, mimi napenda kusema ukweli, kaa sasa wameshakuona lakini hiyo shule ya Barangu wanafunzi wanakaa chini.

"Ninamshukuru huyo muandishi ambaye ameitoa kwenye mitandao, viongozi wa kule wakasema ni masuala ya kisiasa, hayo sio masuala ya kisiasa, bali ndio mambo ninayopenda kuyajua, ninazungumza nikiwa Kagera lakini nikienda Dar es Salaam niyakute yamekamilika na wanafunzi hawakai chini.

"Nitaenda kuitembelea mimi hiyo shule, kwa hiyo kama wananisikia wa Dar es salaam meseji sent and delivary. Haiwezekani ndugu zangu wana Kagera, uwe umechaguliwa na wananchi unaitwa Rais halafu ukawapa watu madaraka, ukawapa uwaziri, ukawapa ukuu wa mkoa , ukawapa ukurugenzi na wanakusanya kodi na bajeti zipo, na wanazunguka kwenye maeneo hayo wanakuta wanafunzi wanakaa chini"Amesema Rais Magufuli.

Amesisitiza hiyo ni dhambi kwake na kwamba alikosea kuchagua baadhi ya viongozi."Ndio maana nilipofika hapa nilizungukia madarasa, sikusubiri madarasa niliyoandaliwa, nikawa navamia madarasa nikakuta madawati yapo nikafurahi sana nikasema Haleluya...hongereni sana ninyi lakini ile shule iliyopo Ubungo maneno haya wakayasikie na mawaziri mko hapa". Amesema.

Aidha amesema ana uhakika kuna maeneo watu wanafanya kazi vizuri sana lakini kuna maeneo mengine bado wamelala."Na ndio maana Mkurugenzi wa Geita niliamua nimfukuze kazi, yeye ananunua gari la Sh.milioni 400 huku wananchi wanachangishwa kwa ajili ya kununua madawati, zinatolewa fedha na mgodi wa wa GGM kwa ajili ya kuchangia maendeleo ya wananchi yeye anakwenda kununua magari.'' 

"Anakwenda kununulia mpaka mabasi ya kusafirisha wafayakazi, yupo Geita Mjini, utakuwa unasafirisha walimu kwenda kwenye shule kufundisha. Kwa hiyo nitoe mwito kwa viongozi wenzangu, tuzitumie fedha hizi vizuri ili zilete matokeo kwa wananchi,"amesema.

Ameongeza, "Na hizi Sh.bilioni bilioni sita zilizotolewa na Serikali ya Uingereza na Sh.bilioni tano zilizotolewa na Serikali ya Tanzania zisingetumika vizuri leo tusingeona mfano huu(Shule), nilipokuja hapa Kagera walitaka fedha hizi nizigawe nikanunue ndizi, nikanunue mahindi.

"Nikasema sitoi kitu, najua nilioekana wa ovyo kwa baadhi ya wanasiasa, huwezi ukawagawia watu wote wa Kagera chakula, nilitaka niwaambie ukweli na ukweli unakuweka huru." Amesema JPM.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2