Meneja wa Mamlaka ya mapato(TRA)Mkoa wa Ruvuma Amina Ndumbogani akionesha Tuzo Maalum waliyokabidhiwa na Mamlaka ya mapato Nchini kutokana na utendaji kazi mzuri wa watumishi wa mamlaka hiyo mkoa wa Ruvuma ambao umewezesha kuvuka lengo la kukusanya shilingi bilioni 8.6 kati ya lengo la kukusanya bilioni 7 katika kipindi cha miezi sita kwa mwaka wa fedha 2020/2021, kushoto ni meneja msaidizi Antipas Mrema.
Na Muhidin Amri, Songea
MAMLAKA ya mapato Nchini (TRA) mkoani Ruvuma, imefanikiwa kukusanya kiasi cha shilingi bilioni 8.442 sawa na asilimia 109 kati ya lengo walilopewa
la kukusanya shilingi bilioni 7.771 katika kipindi cha miezi sita
kutoka mwezi Julai hadi Desemba 2020.
Hayo yamesemwa na Kaimu Meneja wa Mamlaka hiyo mkoani humo Amina
Ndumbogani, wakati akitoa taarifa ya ukusanyaji wa mapato katika
kipindi cha nusu Mwaka wa fedha 2020/2021 kwa waandishi wa habari
ofisini kwake mjini Songea.
Amesema, katika mwaka wa fedha 2020/2021 TRA mkoani Ruvuma
imepewa lengo la kukusanya shilingi bilioni 15.639, lakini kutokana
na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi wa mamlaka hiyo hadi kufika
Desemba 2020 wamefanikiwa kuvuka lengo kwa kukusanya shilingi bilioni
8.4 hivyo kuwa na matumaini ya kufika lengo la kukusanya shilingi
bilioni 15.6
Alisema, mbali na kazi nzuri iliyofanywa na watumishi pia mafanikio
hayo yametokana na ushirikiano waliopata kutoka kwa wadau wengine
wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo Christina Mndeme na wakuu wa Wilaya
tano za mkoa wa Ruvuma pamoja na kamati ya ulinzi na usalama ambayo ni
sehemu ya mafanikio hayo.
Alisema, anajivunia kuona wadau mbalimbali wakiongozwa na Mkuu wa
mkoa wa Ruvuma Chritina Mndeme,Wakuu wa wilaya za mkoa huo na
wafanyabiashara walivyofanikisha malengo ya Mamlaka hiyo kuvuka
malengo katika kipindi cha nusu mwaka kutoka mwezi Julai hadi Desemba
2020.
Aidha alisema, kwa mwaka huu wa fedha wameweka malengo mbalimbali
kama mkakati wa kukusanya shilingi bilioni 15 walizopewa ambayo ni
kupanua wigo kwa kuwatambua na kuwasajili wafanya biashara kwa mfumo
wa mtandao, kupita mlango kwa mlango ili kuwabaini walipa kodi na wale
wanaokwepa kulipa kodi na kuongeza nguvu kwa wafanyabiashara kuhusu
matumizi ya mashine za Efds.
Alisema, mbali na hilo mkakati mwingine ni kuwafuatilia walipa kodi
wenye madeni ili kulipa madeni yao kwa wakati kabla ya hatua za
kisheria hazijachukuliwa dhidi yao.
“kazi ya kukusanya kodi ni ngumu sana, lakini kutokana na jitihada
kubwa zilizofanyika na wadau wengine kwa kweli ndiyo kwa kiasi kikubwa
waliofanikisha malengo hayo.” Alisema Amina.
Alisema, mamlaka ya mapato inaendelea kuwakumbusha wafanya biashara na wananchi wote kwa jumla kuwa msingi wa makadirio ya kodi kwa haki ni
utunzaji sahihi wa kumbukumbu na ni wajibu na kila mwenye sifa kulipa
kodi stahiki za Serikali.
Amina ameonya kuwa, mfanyabiashara yeyote atakayebainika kutotumia
vyema mashine za kielektroniki katika biashara yake au kukaidi
kutimiza wajibu huo wa kisheria atakuwa ametenda kosa na atachukuliwa
hatua kali za kisheria.
Alisema, mfanyabiashara atakayekamatwa kwa kosa la kutotumia mashine
za Efds adhabu yake ni faini kuanzia milioni 3 na isiyozidi milioni
4.5 au kifungo cha miaka mitatu jela au vyote kwa pamoja kwa mujibu
wa sheria za usimamizi wa kodi ya mwaka 2015.
Pia, amewataka wanunuzi wote wa bidhaa mbalimbali kuhakikisha wanadai
risiti pindi wafanyapo manunuzi kwani ni haki ya msingi na kisheria
kwa kila mnunuzi, na kutofanya hivyo ni kosa linaloweza kupelekea
kupata adhabu kali ikiwemo kutozwa faini kati ya shilingi 30,000 hadi
milioni 1.5.
Alisema, TRA inategemea sana ushirikiano kutoka kwa wadau wote katika
suala zima la kukusanya mapato ya Serikali na kusisitiza,ni wajibu wa
kila mwananchi kuonyesha uzalendo kwa kulipa kodi ili kuisaidia
Serikali kutoa huduma bora na haraka zaidi.
Amina amesisitiza kuwa, ni haki na lazima kwa mwananchi kudai risiti
sahihi kila anunuapo bidhaa au huduma pamoja na kutoa taarifa ya
upotevu wa mapato ili kuiwezesha mamlaka hiyo kutekeleza majukumu yake
kwa ufanisi katika kuwahudumia Watanzania.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment