Walioweka fedha zao kwenye Benki zilizofilisiwa wakazichukue-BoT | Tarimo Blog


Bodi ya Bima za Amana imewataka Wananchi walioweka fedha zao kwenye Benki zilizofilisiwa na Benki Kuu ya Tanzania- BoT, kwenda katika matawi ya Benki ya Posta yaliyopo popote nchini, kuchukua amana zao ikiwa ni sehemu ya fidia kwa wateja waliowekeza kwenye benki hizo.

Jumla ya benki 7 zilifilisiwa katika kipindi cha Mwezi Mei 2017 na Januari 2018 baada ya kuonesha mashaka katika uendeshaji wake, ambapo amana na mali za benki hizo zilichukuliwa na kuwa chini ya ufilisi wa BoT.

Akizungumza katika semina ya Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na Biashara Mkoani Mtwara, Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bima za Amana iliyo chini ya BoT Bw. Richard Malisa, amesema ni asilimia 39 tu ya watu  walioweka fedha zao kwenye Benki hizo ndio waliofika kuzichukua na wengine hawajaonekana mpaka sasa.

"Baada ya ufilisi wa benki sisi kama bodi ya bima ya amana tunatakiwa kutoa fidia kwa walioweka fedha zao katika benki husika, na hilo ndio lengo kubwa la bodi hii, ikitokea benki imefutiwa Leseni na BoT sisi wajibu wetu kisheria ni  kutoa fidia ambayo ina ukomo, na kiasi cha juu cha fidia hiyo ni shilingi milioni moja na nusu" amesema.

Malisa amesema mara baada ya kufungiwa kwa benki hizo bodi hiyo walitoa matangazo kwa wananchi ambao walikuwa na fedha zao waende kuzichukua lakini mpaka kufikia Desemba 2020, ni watu 25,050 tu walioenda kuzichukua fedha zao zaidi ya bilioni 7.3 kati ya watu 63,704 ambao wanadai zaidi ya bilioni 3.6 walizoweka huku sababu zikitajwa kuwa ni kutokuwa na taarifa, wengine kuwa na fedha ndogo na hivyo kuepuka gharama ya nauli ya kuzifuatilia fedha zao kwa waliopo mbali na maeneo wanayoishi.

Benki saba zilizofungiwa na kufutiwa leseni na BoT katika kipindi cha mwaka 2017-2018 ni pamoja na Benki ya FBME, Benki ya Efatha, Benki ya Convenant na Benki za Kijamii za  Njombe, Mbinga, Kagera na Meru.

Kaimu Mkurugenzi wa Bodi ya Bima za Amana iliyo chini ya BoT Bw. Richard Malisa akizungumza katika semina ya Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na Biashara Mkoani Mtwara wakati akiwasilisha mada iliyohusu masuala ya Bodi ya Bima za Amana.

Mmoja wa Washiriki wa Semina hiyo akiuliza swali
Waandishi wa Habari za Fedha, Uchumi na Biashara Mkoani Mtwara wakati wakifuatilia mada zilizokuwa zikijadiliwa ukumbini humo


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2