Baada ya kushuhudia Mwili wa Dkt. John Pombe Magufuli akiwa amelala,Sasa nimeamini Jabali lenye Moyo wa Simba na akili ya Duma amelala Usingizi wa Mauti.
Usiku ule wa tarehe 17 Machi, ni usiku Mgumu kuwahi kutokea katika Maisha yangu, Nilimfikiria Baba, Mwalimu,mtu mwenye huruma,ambaye kabla ya "kukuhukumu" atataka akusikilize na wewe, Na siku zote akisema USIOGOPE,Mtu asiyejua UNAFIKI wa kupikwa ila aliyezingatia zaidi matokeo ya kazi aliyokupa, na aliyeamini sana katika nafasi ya pili,Anayesikiliza sana tena kwa Upendo.
Kuondoka kwake kwa wakati huu kuliniingiza Ganzi nisiyowahi kuiona Maishani, Ninajua Mama Janeth amempoteza Mume, Taifa limempoteza Baba na Rais, Africa Imempoteza Mwana mapinduzi Jasiri,Lakini Mbingu imempokea shujaa wa Imani, Aliyevipiga vita bila Kujali maumivu ya Moyo aliyoyapitia, akailinda imani kwa kulitambulisha jina la MUNGU aponyaye kwa mataifa, Na sasa amemaliza mwendo na amepumzika Miguuni kwa bwana wa vita. MATENDO uliyoyatenda kwa Gharama ya maisha yako, yamekutangulia.
Nenda Baba Nenda, matendo yako, kazi zako,na kujitoa kwako kumeandikwa kwa wino wa dhahabu kwenye moyo wangu na katika mioyo ya watanzania wa kweli umeandika Dibaji mpya.
Hadithi za kazi ulizowatendea wana wa Taifa hili zitasimuliwa na vizazi, kwangu umenipa sababu ya kuamka tena, kutenda kwa Ujasiri bila woga wala Hofu,Nikiona Fahari sana Kwamba nimejifunza na Kuwa Mwanafunzi wako na uwe na Uhakika kwamba sasa Nitatenda kwa ujasiri zaidi bila kutokuonea wala kupendelea na niikijua ipo siku MUNGU mwenyewe, katika ukamilifu wake, atatuita kutoa hesabu ya matendo yetu na Sio Maneno yetu.
Tukutane baadae Nyumbani kwa baba, kusiko na Kuomboleza, kilio wala maumivu,Tutakapohesabiwa haki na Bwana Mwenyewe.
Imenyamaza sauti dhabiti ya wanyonge, imenyamaza kimya kiranja mkuu na mkufunzi wapigania usawa kwa vitendo, Amelala Mjamaa Asiyetishika,Ardhi imemeza shujaa na kaka wa Taifa,Bwana Ataitia Nguvu Mioyo iliyosinyaa, wala Hataacha Taifa Lililolitetea Jina Lake liaibike kamwe.
Umetufunza ushupavu na misimamo imara,Nyayo na Kumbukumbu zako vitatupa hasira za kufanya kwa ajili ya Taifa na vizazi tutakavyoviacha.Vilio vya wanyonge na wasio na sauti vimefika kwenye kiti cha Enzi. Rest in power John, Tutakutana Baadae.Bado ni salama Rohoni mwangu.
Nenda Baba, nyuma yako kila tukitaka kulia tunakumbuka umetuachia Mama Samia. Kila tukitaka kukata Tamaa tunamwona mama akiwa jasiri na kutupa tumaini jipya la Mapambano.
Tanzania inakulilia pumzika kwa amani Jembe.
Ole Sabaya.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment