DODOMA WAMPOKEA HAYATI DK MAGUFULI KISHUJAA, WANANCHI WAMSINDIKIZA KUTOKA 'AIRPORT' HADI IKULU CHAMWINO | Tarimo Blog


Charles James, Michuzi TV

VILIO, huzuni na machozi kila kona ya Jiji la Dodoma. Hii ni baada ya mwili wa aliyekua Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dk John Magufuli aliyefariki Machi 17 mwaka huu kutua jijini Dodoma.

Mwili wa Dk Magufuli umetua katika uwanja wa Ndege wa Dodoma majira ya saa 12:54 za jioni na kupokelewa na Rais Mama Samia Suluhu Hassan, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa pamoja na viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama.

Wananchi wa Jiji la Dodoma ambao licha ya mwili wa Hayati Dk Magufuli kuchelewa kufika bado walizidi kujipanga barabarani bila kuchoka wakiimba nyimbo za mapambio.

Wingi wa wananchi waliojumuika kwenye barabara za jiji la Dodoma wakiimba 'Jeshi Jeshi Jeshi, Rais Rais Rais, Baba Baba Baba, Magu Magu Magu huku wengine wakilia ni uthibitisho tosha kwamba Dk Magufuli alikua kipenzi cha watanzania na wana-Dodoma.

Wananchi wa Dodoma wameusindikiza mwili wa Dk Magufuli kutokea Uwanja wa Ndege kupitia mitaa ya Chako Ni Chako kuelekea Bunge hadi Ikulu Chamwino ambapo Dk Magufuli atapumzishwa kwa usiku wa leo.

Kesho wananchi wa Jiji la Dodoma watapata fursa ya kushiriki shughuli ya kumuaga Dk Magufuli ambapo tukio hilo litafanyika kitaifa katika uwanja wa Jamhuri na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa ndani na nje ya nchi.














 
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2