Hakikisheni huduma za kibingwa matibabu ya moyo zinawafikia wananchi walioko vijijini – Mhe. Nyongo | Tarimo Blog

 

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akiwaelezea wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii  huduma za  matibabu ya moyo kwa watoto zinazotolewa  wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo. Kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki Mhe. Stanslaus Nyongo

Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima akisoma risiti ya malipo ya dawa ambayo iliyotolewa kwa mgonjwa anayetibiwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) wakati  Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii  ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. Wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki Mhe. Stanslaus Nyongo.

Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Moyo kutoka Taasisi ya  Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Tulizo Shemu akiwaeleza wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii  namna ambavyo mtambo mpya wa  Cathlab na Carto III utakavyofanya kazi wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. Mwanzoni mwa mwaka jana Serikali ilitoa kiasi cha shilingi bilioni 4.6 kwa ajili ya ununuzi wa mtambo huo ambao utaanza kufanya kazi mwezi ujao.

Msimamizi wa Wodi ya Watoto waliolazwa katika Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Afisa Uuguzi  Theresia Marombe akiwaeleza baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii magonjwa ya moyo yanayowakabili watoto waliolazwa katika wodi hiyo wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana. Watatu kushoto ni Mbunge wa Jimbo la Mchinga ambaye pia ni mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Salma Kikwete.

Mkurugenzi wa Upasuaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Angella Muhozya akiwaelezea baadhi ya wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii jinsi upasuaji wa moyo unavyofanyika wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. Kushoto ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini ambaye pia Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Hassan Kungu.

Wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii wakiwa katika picha ya pamoja na menejimenti ya Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) mara baada ya kumaliza ziara yao ya kutembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa. Katikati mstari wa mbele ni Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dkt. Doroth Gwajima.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi akisoma taarifa ya maendeleo ya Taasisi hiyo kwa wajumbe wa Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya jamii  wakati kamati hiyo ilipotembelea Taasisi hiyo jana kwa ajili ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo.

Picha na JKCI

****************************************

Na Mwandishi Maalum – Dar es Salaam

17/03/2021 Kamati ya kudumu ya Bunge ya huduma na maendeleo ya Jamii imeitaka Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) kuhakikisha huduma za matibabu ya moyo za kibingwa  wanazozitoa zinawafikia wananchi walioko vijijini.

Agizo hilo limetolewa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo Mhe. Stanslaus Nyongo wakati akizungumza na menejimenti ya Taasisi hiyo mara baada ya kumaliza ziara ya kukagua matumizi ya fedha zinazotolewa na  Serikali kama zinatumika ipasavyo pamoja na kuona huduma za matibabu ya moyo zinazotolewa.

Mhe. Nyongo ambaye pia ni Mbunge wa Maswa Mashariki alisema kamati yake  imeridhishwa na huduma zinazotolewa na Taasisi hiyo na kuishukuru Serikali kwa kuanzisha kituo hicho kinachotoa huduma za kimataifa ambacho kimekuwa mkombozi na kuwasaidia  watu wengi wakiwemo watanzania na  wasio watanzania.

Alisema huko vijijini kuna watu wakiwemo watoto wanamatatizo ya moyo ni vyema nao wakapata  huduma za matibabu hayo ambazo hivi sasa zinapatikana hapa nchini. Pia wananchi waelimishwe kuhusu magonjwa hayo  na jinsi gani wanaweza kutibiwa kwa wale ambao wanamatatizo na kwa wale ambao hawana matatizo waelekezwe jinsi ya kuyaepuka.

“Katika ripoti yenu mmesema mmewafundisha madaktari 45 wa watoto kutoka Hospitali za kanda jinsi ya kuwatambua watoto wenye matatizo ya moyo ni vyema sasa mkawafundisha madaktari wa Hospitali za mikoa na wilaya ili nao waweze kuwatambua wagonjwa wa moyo mapema ambao watapata  huduma za matibabu kwa wakati  kwani hivi sasa huduma hizo zinapatikana hapa nchini”, alisema Mhe. Nyongo.

“Pia muwe na vituo vingine vya JKCI katika Hospitali za kanda na mikoa kwa kufanya hivyo kutawasaidia wananchi kutokusafiri umbali mrefu wa kufuata huduma za matibabu ya moyo ya kibingwa ambazo zinapatikana Dar es Salaam”, alisisitiza.

Aliendelea kusema huduma zinazotolewa katika Taasisi hiyo ni za kibingwa na wataalamu waliopo ni wachache  na kuiomba Serikali kuhakikisha wataalamu hao wazalendo hawarubuniwi na kwenda kufanya kazi mahali kwingine pia kwa wataalamu ambao hawana ajira za kudumu waajiriwe ili wawe na uhakika na maisha yao pamoja na moyo wa kufanya kazi.

“Ninaipongeza Compounding Unit ambao wanatengeneza dawa za watoto kutoka kidonge cha mtu mzima hadi kuwa kwenye matumizi ya watoto, hii inasaidia kupatikana kwa dawa za moyo za watoto kwani dawa hizo hazipatikani kwenye soko la dawa nchini kutokana na dawa hizo kutozalishwa viwandani”,.

Kwa upande wake Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Dkt. Doroth Gwajima aliishukuru kamati hiyo kwa kutembelea Taasisi hiyo na kujionea huduma zinazotolewa  na kuahidi kuyafanyia kazi maelekezo yote waliyoyatoa ikiwa ni pamoja na kuhakikisha wataalamu ambao wanafanya kazi za kujitolea wanaajiriwa.

“Kufika kwenu katika Taasisi hii kumewasaidia kufahamu changamoto mbalimbali zinazowakabili, hata Taasisi ambazo hamjazitembelea changamoto zake zinafanana. Ninaamini tukikaa kwa pamoja tutaona ni jinsi gani tutaweza kuzitatua changamoto hizi na kuifanya sekta ya afya iweze kusonga mbele na kutoa huduma bora zaidi kwa wananchi.

Mhe. Dkt. Gwajima alisema Serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika sekta ya afya ni muhimu uwekezaji uliofanyika hapo awali na unaoendelea kufanyika ikiwa ni pamoja na kununua mashine za kisasa za kufanya vipimo pamoja na kutoa tiba ukaendelea kuimarisha huduma ili  wagonjwa wengi waje kutibiwa kutoka nchi za jirani.

Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Moyo Jakaya Kikwete (JKCI) Prof. Mohamed Janabi alisema tangu Taasisi hiyo ianzishwe mwaka 2015 hadi 2020 imeokoa maisha ya watanzania 444,445, kuokoa fedha zaidi ya bilioni 250.7  kwa kufanya upasuaji wa moyo hapa nchini kwa wagonjwa 8009 na kupatikana kwa  dawa muda wote kwa zaidi ya asilimia  95.

Prof. Janabi alisema Taasisi hiyo imesaini mkataba na  Asasi moja ya nchini Marekani  ijulikanayo kwa jina la Childs Heart ambao badala ya kuwapeleka watoto kutibiwa nchini India wanawaleta katika Taasisi hiyo kwa ajili ya matibabu. Hadi sasa  wameshafanya upasuaji wa moyo kwa watoto saba ambapo watatu kutoka nchini  Kenya , wawili kutoka nchini Uganda, wawili kutoka nchini Malawi na Ethiopia.

Naye Mjumbe wa kamati hiyo Mhe. Hassan Kungu ambaye ni Mbunge wa Tunduru Kaskazini alisema ni mara ya kwanza kufika katika Taasisi hiyo amejifunza mambo mengi ikiwa ni pamoja na  wataalamu wa kitanzania kuweza  kutambua mtoto kabla hajazaliwa kama ana matatizo ya moyo au la.

“Nimejifunza Taasisi hii imeweza kununua mitambo mikubwa ya kutibu magonjwa ya moyo bila ya kutumia mikopo au kuwa na madeni ya wazabuni na wataalamu wengi waliopo hapa ni watanzania. Ni jambo la kujivunia tunapata huduma za matibabu hapa nchini bila ya kwenda nje ya nchi, Taasisi zingine za afya ziige mfano kutoka JKCI”, alisema Mhe. Kungu.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2