Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV - Dodoma
Marais wa Mataifa mbalimbali ya Afrika leo wamejitokeza kuomboleza na kutoa heshima zao za mwisho kwa Aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Joseph Magufuli aliyeagwa Kitaifa katika Uwanja wa Jamhuri jijini Dodoma baada ya kifo chake kilichotokea Machi 17, 2021.
Marais waliojumuika na Rais wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan na Watanzania wote kwa pamoja walikuwa ni Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU), Mhe. Félix Tshisekedi, Rais wa Msumbiji na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Mhe. Filipe Nyusi, Rais wa Kenya na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Afrika Mashariki (EAC), Mhe. Uhuru Kenyatta.
Wengine ni Rais wa Afrika Kusini, Mhe. Cyril Ramaphosa, Rais wa Comoro, Azali Assoumani, Rais wa Botswana, Mokgweetsi Masisi, Rais wa Zambia, Mhe. Edgar Lungu, Rais wa Zimbabwe, Mhe. Emmerson Mnangagwa, Mataifa ya Rwanda, Uganda na Burundi yakituma Wawakilishi kutoa salamu za rambirambi na pole kwa Rais Samia na Wananchi wa Tanzania kwa ujumla.
Kwa nyakati tofauti Marais hao wamemuelezea Hayati Dkt. Magafuli kuwa alikuwa Kiongozi muadilifu, mwenye uthubutu, mpenda amani na mtumishi mwadilifu kwa Wananchi wenye kipato cha chini katika Taifa la Tanzania.
Pia Viongozi hao wa Afrika wameeleza kuwa walishirikiana na Hayati Dkt. Magufuli katika shida na raha, usiku na mchana ili kutatua changamoto za Wananchi mbalimbali wa ndani ya Tanzania na bara la Afrika kwa ujumla.
Viongozi hao pia wameahidi kushirikiana kwa hali na mali na Rais wa sasa wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan ili kutekeleza majukumu yake yaliyoachwa na mtangulizi wake, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli aliyefariki.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment