Na Said Mwishehe,Michuzi TV
NI maelfu ya wananchi wa Mkoa wa Dar es Salaam ambao wameendelea kujitokeza katika Uwanja wa Uhuru kwa ajili ya kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk.John Magufuli.
Wananchi wa Dar es Salaam walianza kutoa heshima zao za mwisho na kumuaga mpendwa wetu jana Machi 20,2021 na leo wameendelea tena.Hata hivyo kwa siku ya leo idadi ya watu imekuwa kubwa sana ikilinganishwa na jana kiasi cha kusababisha vyombo vya ulinzi na usalama kuongeza umakini kuhakikisha wananchi hao wanakuwa salama.
Ndani ya Uwanja wa Uhuru watu walikuwa wamejaa kila mahali kiasi cha kusababisha mageti kufungwa ili walioko ndani wamalize kutoa heshima zao za mwisho na ndipo walioko nje waruhusiwe.Hakika idadi ya watu uwanja wa Uhuru ni kubwa sana.
Hata hivyo Mkuu wa Wilaya ya Temeke mkoani Dar es Salaam Godwin Gondwe...alilazimika kutoa tangazo kwa wananchi waliokuwa uwanjani hapo kwamba watu ni wengi ambao wamefika kumuaga mpendwa wetu Dk.Magufuli na akatumia nafasi hiyo kuomba watu wote wakae chini ili kuwepo na utaratibu mzuri utakaowezesha wote waliofika kutoa heshima zao.
" Ndugu wananchi wote wa Dar es Salaam, tunawashukuru wote kwa kuja kwa ajili ya kumuaga na kutoa heshima kwa mpendwa wetu Dk.Magufuli, tunawahakikishia wote mtapata nafasi, lakini kwa idadi ya watu walioko hapa naomba walioko majukwaani wasinyanyuke hadi watakaporuhusiwa, walioko nje wasiingie wabakie huko hadi wa ndani wapungue, "amesema Gondwe wakati akitoa utaratibu .
Wakati hayo yakiendelea ,simanzi na majonzi zimetawala uwanjani hapo na kuna baadhi ya watu wameonekana wakianguka baada ya kutoa heshima zao za mwisho kwa Dk.Magufuli, waliokuwa wakitoa huduma ya usaidizi wamekuwa na kazi ya kubeba watu wanaoanguka ili kuwezesha wengine nao kupata nafasi ya kuaga.
Kwa mujibu wa ratiba leo itakuwa siku ya mwisho kwa wananchi wa Dar es Salaam kumuaga Dk.Magufuli kipenzi cha Watanzania, kwani jioni mwili wake utasafirishwa kwa ndege kuelekea Jijini Dodoma ili wananchi wa huko nao wamuage na baadae mwili utakwenda Zanzibar halafu Mwanza na kumalizia Chato mkoani Geita ambako atapumzishwa kwenye nyumba yake ya milele.
Kwa Dar es Salaam , maelfu ya wananchi ambao wamepata nafasi ya kumuelezea Dk.Magufuli, wesema kifo cha mpendwa wao kimewaumiza wengi kwani alikuwa akiwapenda wananchi wote na hasa wanyonge na kubwa zaidi watakumbuka ujasiri na uthubutu wake wa kufanya maamuzi.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment