UJUMBE WA WAZIRI MKUU KWA WATANZANIA WAKATI HUU KUAGA MWILI WA MPENDWA WETU DK.JOHN MAGUFULI | Tarimo Blog


Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV-Dodoma.

WAKATI Watanzania wakiendelea kuaga na kutoa heshima za mwisho kwa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Hayati Dk.John Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amesema leo Machi 22, mwaka 2021 ni siku ya kitaifa kwa ajili ya shughuli za kumuaga na kutoa heshima za mwisho kwa mpendwa wetu.

Akizungumza katika Uwanja wa Jamhuri Mjini Dodoma, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa amewaambia wananchi waliokuwepo uwanjani hapo wakiongozwa na Rais Mama Samia Saluhu Hassan pamoja na marais wengine tisa kutoka nchi mbalimbali na viongozi wengine waandamizi, amesema anatoa pole kwa Rais Mama Samia, Mjane , watoto, ndugu, jamaa, marafiki pamoja na Watanzania wote.

Pia ametoa pole kwa wale wote ambao wameguswa na msiba huo na kwamba kama wanavyofahamu baada ya kutolewa tangazo la kifo na ratiba kutoka kwa Rais Mama Samia , ratiba ya kuaga ilianza Machi 20 Dar es Salaam na itaendelea hadi Machi 26 mwaka huu kwa kuupumzisha mwili wa mpendwa wetu katika nyumba yake ya milele kijijini kwake Chato.

"Ratiba hii imetoa fursa kwa watanzania kutoa heshima kwa kipenzi chetu, mtetezi wa wanyonge, ambaye anaadoka akiwa ameacha alama.Tangu kutokea kwa msiba huu tumepata ushirikiano mkubwa kutoka kwa watanzania, tumeona makundi mbalimbali yakijitokeza kutoa hisia zao, uchungu wao kwa Dk.Magufuli.

"Wananchi pokeeni shukrani kwa kujitokeza kwa wingi katika kuaga mwili wa Dk.Magufuli, kwa wingi huu wananchi ambao umenekana tangu kuanza kuaga, tumeamua kuongeza fursa ya wengi kumuaga kwa kupita kwenye mitaa na kipenzi chetu.Tulianza Dar es Salaam kwa siku mbili.

"Leo tuko Dodoma tutapita katika mitaa, na kesho tutakuwa Zanzibar na tupita mitaani baada ya kupata dua katika Uwanja wa Abeid Aman Karume, baadae tutakwenda Mwanza , na kisha mwili utapitishwa barabarani kuelekea Geita , kwa kupitia daraja kubwa la Kigongo Busisi,"amesema Waziri Mkuu.

Aidha amesema atakuwa mchoyo wa fadhila kama hatampongeza Rais Samia Suluhu Hassan kwa uimara wake tangu ulipotokea msiba huo wa kuondokewa na mpendwa wetu, kipenzi chetu na aliyekuwa Rais wetu."Tunakushukuru Rais wetu kwa maelekezo yako na ushauri kwa Kamati ya Mazishi ili kufanikisha jambo hili.

"Ndugu wananchi tuendelee kumuenzi kwa vitendo, wengi tulitamani tuwe naye kimwili lakini hatuna budi kumshukuru Mungu kwa kutoa na sasa ametwaa, umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu, hivyo naomba kuungana na kauli ya Rais wetu tuendelee kushirikana, kuvumiliana na kudumisha umoja na mshikamano wetu na tuendelee kumuombea mpendwa wetu apumzike kwa amani,"amesema.

Pia amesema leo wanayo faraja kubwa kwa kukimbiliwa na majirani zetu na kwamba wanawashukuru kwa kujitoa kwao na kuwakimbilia Watanzania katika kuungana nao kwenye kipindi hiki kigumu."Kupata marais tisa si jambo dogo, kupata makamu wa Rais wawili sio jambo dogo, kupata wawakilishi wa marais si jambo dogo, kupata wawakilishi wa nchi mbalimbali nalo si jambo dogo.

"Jambo hili linaonesha upendo mkubwa walionao wenzetu dhidi yetu, nasi tunacho cha kujifunza kutoka kwao.Kwa utambulisho wa ratiba hii na kama nilivyosema tutaendelea kuaga kwenye vituo vingine vilivyobakia, inakamilisha taarifa ambayo nimeona niifikishe kwenu.Niwahakikishie tutaendeleza yale yote aliyotenda na kuanzisha na tubani mengine kwa ajili ya taifa letu".





Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2