WAJASIRIAMALI MOROGORO WASITISHA BIASHARA KWA MUDA KUMUENZI JPM | Tarimo Blog




Wajasiriamali wakiwemo wachoma mahindi na wauza Mbogamboga katika Eneo la Feli  Kata ya Magole Wilaya ya Kilosa  Mkoani Morogoro wakisaini Kitabu cha Rambirambi ikiwa ni ishara ya kuungana na Watanzania wengine kufanya maziko ya Hayati Dkt John Pombe Magufuli.

Wajasiriamali wakiwemo wachoma mahindi na wauza Mbogamboga katika Eneo la Feli Kata ya Magole Wilaya ya Kilosa Mkoani Morogoro wakiwa katika Maombi maalumu ya kumuombea Hayati Dkt John Pombe Magufuli.


NA FARIDA SAIDY, MOROGORO

WAJASIRIAMALI wakiwemo wachoma mahindi, wauza mbogamboga, matunda pamoja na mamalishe katika eneo la Feli Kata ya Magole Wilayani Kilosa Mkoani Morogoro wamesitisha kwa saa kadhaa shughuli za biashara zao ili kuungana na Watanzania wote kushiriki mazishi ya Hayati Dokta John Pombe Magufuli wakikumbuka alivyo wajengea vibanda vya kufanyia biashara katika eneo hilo.

Michuzi Tv na Blog imefika katika eneo hilo la Feli na kushuhudia shughuli za biashara zikiwa zimesimama huku wafanyabiashara hao wakiwa wamekusanyika kwa ajili ya kufanya maombi maalumu ikiwa ni ishara ya kushiriki maziko ya mpendwa wao Hayati Dk. Magufuli.

Wakizungumza kwa nyakati tofauti wajasiriamali hao wamesema wanamkumbuka Hayati  Magufuli kwa vitu vingi hususani kwa kuwa na maamuzi magumu katika kuwasaidia wananchi wa hali ya chini kama alivyowafanyia wao katika Kata ya Magole kwa kuwajengea vibanda vya kufanyia biashara eneo la Feli katika Barabara kuu ya Morogoro-Dodoma.

Aidha, wafanyabiashara hao wamesema wataendelea kuchapa kazi ili kumuenzi huku wakimuomba Rais Mama Samia Suluhu Hasan kufuata nyendo za Hayati Dk. Magufuli

Hata hivyo, katika viunga mbalimbali vya mji wa Morogoro  Wananchi walifuatilia moja kwa moja mazishi ya Hayati Dokta Magufuli kupitia Luninga pamoja na mitandao ya kijamii ikiwa ni moja ya njia ya kumuaga Jemedari huyo.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2