Baadhi ya wananchi waliofika katika familia ya Mtuwa kuomboleza kifo cha wanafamilia watano waliofariki katika Uwanja wa Uhuru mkoa wa Dar es Salaam Machi 20, 2021.
Na Mwandishi wetu, Michuzi Tv.
FAMILIA iliyopoteza wanafamilia watano imetoa ratiba ya maziko ya Msiba huo na kwamba miili ya marehemu watano itawasili nyumbani siku ya Jumatano jioni Machi 24, 2021.
Akizungumza na Michuzi Tv mwanafamilia wa Familia ya mzee Mtuwa, Irene Mtuwa amesema kuwa watoto pamoja na mama yao walienda Uwanja wa Uhuru mkoani Dar es Salaam kuaga mwili wa aliyekuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Hayati Dkt. John Pombe Magufuli.
Amesema, ilipofika muda wa saa 10 jioni walipigiwa simu na mtu asiyejulikana akawaambia kuwa mwenye simu hiyo amedondoka katika Uwanja wa uhuru waende Hospitali ya Temeke kuangalia.
Amesema, walitoka mpaka uwanja ya Uhuru ilipokuwa ikifanyika hafla hiyo ya kumuaga Hayati Dkt.Magufuli ambapo walifanikiwa kuliona gari tu ambapo wanafamilia hao wakaamua kutafuta ufunguo wa ziada wa gari wakalichukua na baadae wakaenda hospitali ya rufaa ya Temeke.
Irene amesema kuwa, walipofika hospitalini hapo waliingia katika wodi za majeruhi na kuangalia ndugu zao hawakuona na ndipo walipo ruhusiwa kwenda chumba cha kuhifadhia maiti katika hospitali hiyo na kuwatambua wapendwa wao ambao ni mama pamoja na watoto wanne wa familia hiyo.
Ameeleza kuwa, maandalizi kwa ajili ya kuhifadhi miili yanaendelea hapo nyumbani kwao Kimara, Ubungo kata ya Saranga mtaa wa Matangini Mkoani Dar es Salaam.
Waliofariki dunia ni Susan Mtuwa na watoto wake wawili, Nathan (6) na Natalia (5) pamoja na watoto wengine wawili wa Shemeji zake ambao Michelle (8) na Christian (11) ambao ni watoto wa shemeji zake Susan huku dada wa kazi wa familia hiyo bado hajapatikana mpaka sasa.
Amesema kuwa maziko yatafanyika katika makaburi ya Familia siku ya Alhamis Machi 25, 2021 Mkoani Dar es Salaam.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment