Charles James, Michuzi TV
WAZIRI wa Elimu Sayansi na Teknolojia, Prof Joyce Ndalichako amemtaka Mkurugenzi wa Udhibiti Bora Elimu nchini kusimamia idara hiyo vizuri kabla ya kumuagiza Katibu Mkuu wa Wizara hiyo kutatufuta mdhibiti ambaye ataenda na kasi inayotakiwa.
Waziri Ndalichako ametoa kauli hiyo jijini Dodoma leo wakati akikabidhi magari 38 ya wadhibiti ubora elimu kwenye Halmashauri za Wilaya 27 na kanda 10 na gari moja litabaki wizarani kwa ajili ya kuratibu na kufuatilia Udhibiti ubora wa elimu.
Akizungumza wakati wa kukabidhi magari hayo, Prof Ndalichako amemtaka mdhibiti ubora kuhakikisha anawasimamia wadhibiti ubora wa halmashauri ili waweze kufanya ukaguzi hadi kwenye shule za Sekondari na vyuo vya ufundi na siyo kuishia shule ya msingi pekee.
Amesema imekuepo tabia ya wadhibiti ubora wa halmashauri kufanya ziara ya kukagua shule za msingi lakini wanaziacha shule za sekondari zilizopo karibu hadi zije kukaguliwa na wadhibiti ubora wa kanda jambo ambalo amelipiga marufuku.
" Tunatoa magari haya kwenu muende mkafanye kazi, haiwezekani mtu anatumia gari la serikali kwenda kukagua shule ya msingi ambayo jirani yake kuna sekondari anaacha kuikagua eti kwa sababu mdhibiti ubora wa kanda atakuja, huo ni ubadhirifu wa fedha za Umma unatumia gari la serikali bure.
Elimu ya mdhibiti ubora wa halmashauri na kanda ni sawa, nikutake Mkurugenzi wa Udhibiti kusimamia hili usiruhusu hii hali ya matabaka ni ikiendelea tena nitamuagiza Katibu Mkuu atafute Mkurugenzi mpya," Amesema Prof Ndalichako.
Waziri Ndalichako amesema serikali kupitia Wizara ya Elimu itaendelea kupunguza changamoto za wadhibiti ubora kama ambavyo imekua ikifanya ambapo licha ya magari hayo 38 kugaiwa magari mengine 12 yameshaagizwa yapo njiani yanakuja.
Amesema magari hayo 38 yamegharimu kiasi cha Sh Milioni Sita huku akiwataka watumiaji wake kuyatunza magari hayo ili yaweze kudumu kwa muda mrefu na kutatua changamoto ya usafiri kwenye idara hiyo.
Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA
Post a Comment