RAIS MAMA SAMIA AWAONYA WENYE HILI NA LILE KUELEKEA 2025 | Tarimo Blog


 Charles James, Michuzi TV

ACHENI hili na lile! Ni kauli ya Rais Mama Samia Suluhu Hassan kwa wanasiasa na viongozi wenye ndoto na uchaguzi wa mwaka 2025 kuacha fikra hizo na badala yake wajielekeze katika utendaji kazi wao na kuwatumikia watanzania.

Kauli hiyo ameitoa Ikulu Chamwino, Dodoma leo alipokua akimuapisha Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Hussein Katanga na Mawaziri Manaibu wapatao nane ambao aliwateua jana.

Rais Mama Samia amesema anafahamu ni desturi kwa nchi yetu na hata nchi nyingine Rais akiwa kwenye kipindi chake cha pili kunakua na hili na lile kwa baadhi ya viongozi hivyo amewaonya kuacha fikra hizo.

" Nafahamu mwaka 2025 ni karibu na mpo ambao mna hili na lile, niwaambie acheni twendeni tukafanye kazi, nawaambia kila mwenye hili na lile kwa mwaka 2025 aache mara moja," Amesema Rais Mama Samia.

Mama Samia amesema katika kufanya mabadiliko katika Wizara hizo amemteua mtu mtaalamu kwenye sekta anayoimudu lengo likiwa ni kwenda kuongeza ufanisi kwenye wizara na kuharakisha maendeleo.

" Kwa Mawaziri mlioapa leo nimechukua wale mabingwa wa sekta nikaona niwarudishe kwenye sekta zao, mfano Prof Palamagamba ni Bingwa wa Sheria nimemrudisha Wizara ya Sheria, Dk Mwigulu ananukianukia Fedha hivyo nimempeleka Wizara ya Fedha na Mipango na hapo umeambiwa na Makamu wa Rais kuwa tufikie lengo la Sh Trilioni 2 kweli tufikie lengo la mapato hayo kwa mwezi.

Sehemu tuliyopata shida na wenzangu wakati wa kuchagua ni kwenye Wizara ya Mambo ya Nje lakini tukatua kwa Balozi Liberata huyu amekua wizara hii anajua vichochoro vyote naamini atatusaidia kunyoosha mahusiano yetu kimataifa," Amesema Rais Samia.

Amesema anafahamu Pauline Gekul aliyekua Naibu Waziri wa Mifugo anaifahamu Mifugo vizuri ila ameona Ampeleke Wizara ya Habari Utamaduni Sanaa na Michezo ili akainue michezo.

" Gekul najua unafahamu Mifugo vizuri lakini nimekupeleka Michezo ukainue michezo kwa Wanawake maana Wanawake tunafanya vizuri sana ila hatusifiwi, wanaume wakifunga goli moja tu hata hawajafika nusu fainali na viwanja wanapewa, nenda kasimamie vizuri," Amesema Rais Samia.

Amewakumbusha mawaziri wote kuwa serikali ni moja wafanye kazi kwa ushirikiano na hatosita kumuondoa yeyote ambaye atainua mabega yake akiwataka kwenda kwa watanzania kutatua changamoto zao.

Mama Samia amesema upo uwezekano  kuwaapisha viongozi wengine Jumanne wiki ijayo baada ya sikukuu ya Pasaka kumalizika.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2