WAHUKUMIWA SIMANJIRO KWA KUGAWA EKARI 413 ZA KIJIJI | Tarimo Blog

 Na Mwandishi wetu, Simanjiro

MAHAKAMA ya Wilaya ya Simanjiro Mkoani Manyara, imetoa adhabu ya kwenda jela miaka mitatu au kulipa faini ya shilingi 100,000 kwa wanakamati wa ardhi ya Kijiji cha Kilombero baada ya kukiri kosa la kutumia madaraka yao vibaya na kugawana ekari 413.

 

Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu amesema wanakamati hao walifanya kosa hilo kinyume na kifungu cha 31 cha sheria ya kuzuia na kupambana na rushwa namba 11/2007.

 

Makungu amesema adhabu hiyo imetolewa na Hakimu mfawidhi wa mahakama ya wilaya ya Simanjiro, Charles Owisso katika kesi hiyo namba CC 12 ya mwaka 2021.

 

Amesema adhabu hiyo imewapata waliokuwa wanakamati ya kijiji cha Kilombero, Habibu Juma Dumbui, Robert Msengi Matua, Hatibu Abdalah Rajabu na Salah Isack Maula.

 

Amesema awali, mawakili wa TAKUKURU, Martin Makani na Evaline Onditi, waliwafikisha Mahakamani washtakiwa sita katika kesi hiyo akiwemo Jamhuri Hamis Muna aliyepewa ekari 413 za ardhi ya kijiji na kamati hiyo kwa kushirikiana na Ofisa Mtendaji wa Kijiji hicho Emmanuel Gabriel Komba bila kibali cha mkutano mkuu wa kijiji, kinyume na kifungu cha 8 (5) cha Sheria ya Ardhi ya Vijiji Cap 114 (R:E 2002).  

 

Amesema katika kesi hiyo Jamhuri Hamis Muna alikana makosa ya kujipatia jumla ya shilingi 114, 850,000 kwa njia ya udanganyifu toka kwa watu mbalimbali kutokana na mauzo ya ekari hizo 413 na alipelekwa mahabusu baada ya kushindwa kutimiza masharti ya dhamana.

 

Ametoa rai kwa kamati za ardhi za vijiji na watendaji wa vijiji kuzingatia Sheria ya Ardhi ya Vijiji Cap 114 (R:E 2002) katika utekelezaji wa majukumu yao na wale wenye uelewa mdogo kuhusu sheria hiyo ni vyema wakaomba ufafanuzi kutoka kwa wanasheria ambao kwa sasa wapo kwenye kila Halmashauri.   

 

Mkuu wa TAKUKURU Mkoani Manyara, Holle Joseph Makungu akizungumza na waandishi wa habari ofisini kwake Mjini Babati.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2