RAIS SAMIA: KUPATA MATANGAZO NI USHINDANI, SIJAONA KATAZO | Tarimo Blog




Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

RAIS wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan amesema taratibu za kupata matangazo katika Vyombo vya Habari ni hali ya ushindani, amewaasa Wamiliki wa Vyombo hivyo kuchangamkia fursa ya matangazo hayo kuyapata na kujiendesha ipasavyo sambamba na kufuata taratibu za nchi katika uendeshaji wake.

Rais Samia amesema hayo alipozungumza na Wahariri wa Vyombo mbalimbali ya Habari kote nchini Ikulu mkoani Dar es Salaam katika Siku 100 tangu kushika madaraka hayo, amesema katazo la kupata matangazo hayo hajalikuta bali upatikanaji wake ni uwezo wa mtu.

Aidha kuhusu ruzuku kwa Baraza la Habari, Rais Samia amesema bado inaangaliwa kutoa ruzuku kwa Tasnia hiyo ili baadae kwenda sawa na Mamlaka za Bunge na Mahakama ambazo zinapata ruzuku Kikatiba. 

Pia, amesema Serikali haitafuta Ada za Leseni za uendeshaji wa Vyombo vya Habari kutokana na Sheria yenyewe inavyosema, ameahidi kukaa na kuziangalia upya Sheria hizo na kupata unafuu katika Ada hizo, “Kutokana na Hali ya Uchumi wa Vyombo vya Habari tunaahidi kulipa madeni kidogo kidogo na kwa awamu ili kuondoa hali hii katika Vyombo mbalimbali vya Habari”, amesema.

Katika hatua nyingine ndani ya Siku 100, Rais Samia amesema kazi ya Urais ni ngumu, ameeleza kuwa Vyombo vilivyochini yake na Wasaidizi wake wanasaidia kufanya kazi hiyo ili kufikia azma katika Mamlaka hayo.

“Nashukuru nina Wasaidizi wangu kadhaa, kazi hii si rahisi kihivyo, mnajua ukiwa na madaraka haya kila kinachotokea kwenye nchi lazima ukijue, Mafaili yote yanayoingia kwa siku lazima uyapitie kazi hii ni ngumu”, amesema Rais Samia.

“Licha ya ugumu mimi pamoja na Wasaidizi wangu tumehimili vishindo, thamani ya Fedha ipo vizuri, Mfumo wa Bei upo vizuri. Hadi sasa tuna akiba ya Fedha ya Dola za Marekeni Bilioni 4 na Milioni 970”, ameeleza Rais Samia.

Awali, Mwenyekiti wa Jukwaa la Wahariri (TEF), Deodatus Balile ameomba kwa Serikali kupunguza Ada za Leseni kwa Vyombo vya Habari, pia ameomba Serikali kuweka nguvu zaidi katika ukombozi wa Vyombo hivyo ili kuvinyanyua Kiuchumi.

Balile ameomba kwa Serikali kufunguliwa kwa baadhi ya Magazeti yaliyofungiwa, kuhusu deni la Bilioni 6.5 hadi 8 ameomba Serikali kusimamia ili tasnia hiyo na Vyombo vya Habari kulipwa kiasi hicho kwa wakati.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2