SERIKALI KUFUNGA KAMERA ZA USALAMA JIJINI DODOMA | Tarimo Blog

Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka(wapili kushoto), akisikiliza maelezo ya Mradi wa Ujenzi wa Kituo cha Polisi Chang’ombe kutoka kwa Mrakibu Mwandamizi wa Polisi, Zakaria Senso baada ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi wa Ujenzi wa kituo hicho leo, kinachojengwa katika Kata ya Chang’ombe, jijini Dodoma.Wapili kulia ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Ramadhani Kailima.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi



Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde (wapili kulia), akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka mifuko ya saruji ikiwa ni mchango wake katika Ujenzi wa Kituo Kipya cha Polisi Chang’ombe lengo ikiwa kudhibiti uhalifu katika maeneo ya Changombe.Wapili kushoto ni Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi,Ramadhani Kailima.Picha na Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi.

*************************

Abubakari Akida, Dodoma

Serikali imedhamiria kufunga kamera za usalama katika maeneo mbalimbali ya Jiji la Dodoma kwa lengo la kupunguza uhalifu ambao umeanza kushamiri katika maeneo ya jiji hilo baada ya Serikali kuhamia Dodoma huku wimbi la watu likichagiza hali hiyo ya uhalifu.

Hayo yamesemwa leo na Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Anthony Mtaka wakati wa Hafla ya kuweka Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Kituo cha Polisi Chang’ombe kinachojengwa katika eneo la Chang’ombe, jijini Dodoma.

Adhma hiyo ya kujenga kituo imekuja baada ya matendo ya uhalifu ikiwemo uporaji, ubakaji, udhalilishaji, matumizi ya dawa za kulevya kushamiri katika maeneo ya Chang’ombe hali inayopelekea wananchi wa maeneo hayo kuishi kwa wasiwasi wakihofia matendo hayo ya uhalifu.

“Maeneo mengi ya jiji la Dodoma tutafunga kamera za usalama barabarani, hatuwezi kuwa na jiji ambalo polisi wetu wanakimbizana na wahalifu muda wote, tutatumia teknolojia hiyo kudhibiti uhalifu wa aina mbalimbali, Dodoma ni Makao Makuu ya nchi lazima pawe salama nawashauri wahalifu watafute shughuli nyingine ya kufanya hapa si salama tena kwa kazi zao” alisema Mtaka

Akizungumzia Ujenzi wa Kituo hicho cha Polisi, Mkuu wa Mkoa huyo aliwataka wananchi kushirikiana na serikali kuhakikisha kituo hicho ujenzi wake unakamilika mapema ili kianze kutoa huduma za kiusalama katika maeneo hayo.

“Chang’ombe inakua inahitaji kituo kikubwa kitakachofanya kazi saa ishirini na nne ili wafanyabiashara na wananchi wafanye shughuli zao kwa muda wote na sio biashara zifungwe kwa kuhofia uhalifu, sasa kazi ya serikali sio kukwambia ufunge biashara yako muda gani kazi ya serikali ni kukulinda ili kuwepo na uhuru wa kutoa huduma, kwahiyo wananchi tushirikiane ili kituo kimalizike haraka” alisema Mtaka

Akizungumza kwa niaba ya Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Naibu Katibu Mkuu Ramadhani Kailima alisema wizara imetoa kiasi cha shilingi milioni 10/= kama mchango wake katika ujenzi wa kituo hicho na kikikamilika kitaweza kutoa huduma mbalimbali ikiwemo upelelezi wa matukio, upelekaji wa majarada ya kesi kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mashtaka ambayo yatapelekwa mahakamani kwa hatua za kisheria.

Katika hafla hiyo Mbunge wa Jimbo la Dodoma Mjini, Anthony Mavunde alichangia papo hapo mifuko hamsini ya sementi kwa ajili ya ujenzi wa kituo hicho na kumkabidhi Mkuu wa Mkoa Anthony Mtaka.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2