SERIKALI YAPIGA VITA UNYANYAPAA DHIDI YA WATU WENYE VVU | Tarimo Blog



Na Bakari Madjeshi, Michuzi TV

SERIKALI imeendelea kupiga vita vitendo vya unyanyapaa, unyanyasaji, ubaguzi na ukatili kwa Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi nchini huku ikiahidi kuendelea kutoa elimu kwa Watu wa kada zote kuhakikisha jamii inatokomeza Virusi hivyo na kuwa na afya bora na salama.

Hayo yameelezwa na Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera ,Uratibu na Bunge), Kaspar Mmuya wakati akizungumza na Makundi, Konga, Mitandao kutoka sehemu mbalimbali nchini zilizo chini ya Baraza la Taifa la Watu Waishio na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) Ofisini kwao jijini Dar es Salaam.

Mmuya ametoa hamasa kwa Watanzania kujua hali zao kiafya bila kujali jinsia na umri, pia amepongeza juhudi za NACOPHA katika mapambano dhidi ya Virusi vya Ukimwi nchini huku akitoa wito kwa Serikali kuangalia vizuri mifumo iliyopo sasa ili kufikia watu wengi zaidi.

“Hata mimi nimesikia tukio la kule mkoani Shinyanga la Mwanamme mmoja kuua Mke wake kwa kumkata Mapanga kwa kile kilichoelezwa kuwa alibaini Mke huyo anatumia Dawa za kufubaza VVU (ARV) kwa siri, nasema poleni sana NACOPHA”.

“Huyu Mwanamme hakujua kama na yeye alikuwa analindwa kwa huyo Mke kuanza kutumia hizo Dawa, NACOPHA endeleeni kutoa elimu kuhusu VVU”, ameeleza Mmuya.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Waishio na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA), Bi. Leticia Mourice ameipongeza Serikali kupitia Mamlaka zake husika kutoa huduma za mapambano dhidi ya VVU bila malipo kutokana na hali ya uchumi wa Wananchi wengi.

Bi. Leticia amesema NACOPHA itaendelea kupiga vita unyanyapaa, ukatili na ubaguzi dhidi ya Watu wenye VVU ili kulinda upendo, amani na mshikamano kwa jamii na kuepuka uvunjifu wa amani na haki za binadamu kutokana na matendo hayo.

Pia Bi. Leticia ameomba kwa Serikali kutoa adhabu kali na fundisho kwa jamii kwa wale wanaofanya mauaji dhidi ya Watu wanaoishi na Virusi vya Ukimwi akitolea tukio la mauaji lilitokea mkoani Shinyanga.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera ,Uratibu na Bunge), Kaspar Mmuya akizungumza na Makundi, Konga, Mitandao mbalimbali nchini zilizo chini ya Baraza la Taifa la Watu Waishio na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA) Ofisini kwao jijini Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa Baraza la Taifa la Watu Waishio na Virusi vya Ukimwi (NACOPHA), Bi. Leticia Mourice akizungumza kabla ya kumkaribisha Mgeni rasmi katika Mkutano na Makundi, Konga, Mitandao mbalimbali nchini zilizo chini ya NACOPHA.

Bi. Leticia ametoa ushuhuda wa tukio la mauaji yaliyotolea mkoani Shinyanga kwa Mwanamme mmoja kumuua Mkewe baada ya kubaini alikuwa akitumia Dawa za Kufubaza VVU (ARV).
Baadhi ya Wawakilishi wa Konga, Vikundi, Mitandao mbalimbali nchini wakifuatilia Mkutano uliofanyika Ofisi za NACOPHA jijini Dar es Salaam.
Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera ,Uratibu na Bunge), Kaspar Mmuya akipata maelekezo kwa baadhi ya Wanavikundi ambao ni Wajasiriamali waliokuwa wakionyesha bidhaa zao katika Mkutano huo uliofanyika Ofisi za NACOPHA jijini Dar es Salaam.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2