VIONGOZI WA DINI WAMSHUKURU MUNGU KUIFANYA TANZANIA KWA MARA YA KWANZA KUWA NA RAIS MWANAMKE, NCHI KUWA SALAMA | Tarimo Blog

 Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

VIONGOZI wa dini nchini wamekutana kwa ajili ya kuzungumza masuala mbalimbali yanayohusu mustakali wa Taifa la Tanzania huku wakitumia nafasi hiyo kumshukuru Mungu neema yake ya kuifanya nchi kwa mara ya kwanza kuwa na Rais mwanamke.

Aidha wamesema wanamshukuru Mungu kwa jinsi ambavyo Katiba ya Tanzania imetekelezwa bila kuwepo na uvunjifu wa amani baada ya aliyekuwa Rais Dk.John Magufuli kufariki dunia akiwa madarakani na hivyo ikalazimika Makamu wa Rais Samia Suluhu Hassan kushika nchi kwa amani na utulivu mkubwa, kitu ambacho kwa nchi nyingine kisingewezekana.

Akizungumza mbele ya waandishi wa habari, Askofu Nelson Kisare ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu ,Kanisa la Mennonite Tanzania amesema pamoja na mambo mengine ambayo wameyajadili kwenye kikao hicho, kuna kila sababu ya kumshukuru Mungu kwa kufanya mambo makubwa mawili ndani ya nchi yetu na Watanzania wamebakia salama.

"Katika siku za karibuni, ni mara ya kwanza katika Taifa letu Katiba yetu imeonesha kama inafanya kazi au haifanyi kazi.Rais wetu alitwalia na Mungu akiwa madarakani, tumeona Katiba yetu imefanya kazi, tumetoka kwenye utawala mmoja kwenda mwingine kwa amani na utulivu.

"Tunayo kila sababu kumshukuru Mungu na kuliombea Taifa na viongozi kwa yale ambayo yametokea, katika nchi nyingine za wenzetu ikitokea kitu kama kilichotokea kwetu, Rais aliyekuwa madarakani ametwaliwa na Bwana inaweza kutoa vurugu lakini kwetu Tanzania hakuna vurugu iliyotokea.

"Hivyo tuna kila sababu ya kumshukuru Mungu na sisi mahusiano yetu na Mungu ni ya kila siku , kila wakati na muda wote.Pia ni jambo la kumshukuru Mungu kwani ni kwa mara ya Kwanza kuwa na Rais mwanamke jambo ambalo halijawahi kutokea kwenye nchi yetu,"amesema Askofu Kisare

Ameongeza ndio sababu ya wao viongozi wa dini wamekutana na kufanya dua na sala kwa ajili ya kushukuru kwa mambo makubwa mawili ambayo yametokea kwenye nchi yetu.

Akizungumza sababu za kukutana kwa viongozi hao wa dini na kufanya kikao hicho, Mwenyekiti wa kikao hicho, Sheikh Mkuu wa Tanzania Aboubakari Zubeir amesema wamekuwa na kawaida ya kukutana na kujadiliana mambo yanayohusu dini zao , waumini wao na mustakali wa nchi kwa ujumla.

"Viongozi wa dini tunakawaida ya kukutana kuzungumza masuala yanayohusu dini zetu, kama vile kujenga mahusiano mema,kuzungumzia amani ,kujenga maadili kwenye jamii na wakati mwingine kutoa muelekeo wa waumini wetu katika mambo yanayohusu waumini wetu na Taifa letu.

"Wakati mwingine tunazungumza mambo yenye mahusiano kama wana dini lakini na Serikali vile vile , kwasababu dini ni kitu kikubwa , kimechukua jamii kubwa sana na karibu watu woote atakuwepo mmoja kwenye upande mmojawapo wa dini , kwa hiyo tabia hii ya kukutana mara kwa mara haikuanza sasa imeanza miaka mingi huko nyuma.

Wakati huo huo Askofu Alex Malasusa amesema wanashukuru ushirikiano uliopo kwenye dini na madhehebu mbalimbali katika Taifa hili."Ushirikiano huu umekuwa ukituletea sifa sio tu kwa Bara letu la Afrika, bali duniani, kwamba viongozi wa dini wanaweza kukaa pamoja.

"Ni jukumu la vyombo vya habari kusaidia kueleza kuwa watu wanaweza kuwa na dini tofauti, madhehebu tofauti na bado wakakaa pamoja, kwababu yako mambo yanatuunganisha moja kwa moja.

"Unapozungumzia suala la amani , sisi sote tunatamani kuwa na amani kama watanzania, sisi sote tunalo jukumu la kuhakikisha tunakuwa na amani, tunapozungumzia uchumi wote tunahitaji kuwa na uchumi ili kila mtu aweze kuona hii ni nchi nzuri.

"Kila mtu apate chakula cha kila siku, tunajua tuna dini tofauti lakini kuna mambo yale yanayotuunganisha, tunapozungumzia maji tena maji safi na salama, hayahusiani na dini lakini yanatukusanya pamoja , tunapozungumzia afya , miundombinu, vitu kama hivyo lazima tuendelee kuvizungumza.Ni vikao vyetu vya kawaida,"amesema Askofu Malasusa.
Sheikh Mkuu wa Tanzania Aboubakari Zubeir akizungumza jambo na viongozi wenzake wa Dini wakati wakielekea kuzungumza na Waandishi wa Habari kuhusu mambo mbalimbali leo mkoani Dar es Salaam.
Sheikh Mkuu wa Tanzania Aboubakari Zubeir  akifafanua jambo mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) leo mkoani Dar es Salaam
Baadhi ya Waandishi wa Habari wakiwasikiliza Viongozi vya Dini walipokuwa wakizungumza mambo mbalimbali leo mkoani Dar es Salaam.
Mwenyekiti wa baraza la Makanisa ya Kipentekoste Tanzania (CPCT) Askofu Peter Konki (wa pili kushoto) akizungumza mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) akifafanua umuhimu wa kuwalinda viongozi wetu Wastaafu na hata walioko madarakani kwa wale wanaosambaza maneno mabaya kwa viongozi wa Kitaifa katika maeneo mbalimbali ikiwemo kwenye mitandao ya kijamii.
Askofu Alex Malasusa akifafanua jambo kwa Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu unyanyasaji na ukatili kwa Watoto ambao umekuwa ukiendelea kufanyika katika jamii
Askofu Nelson Kisare ambaye ni Mwenyekiti wa Baraza la Maaskofu ,Kanisa la Mennonite Tanzania akifafanua kwa ufupi mbele ya Waandishi wa Habari (hawapo pichani) kuhusu mambo mbalimbali waliyoyajadili kwenye kikao chao cha pamoja walichokifanya kabla ya kuzungumza na Vyombo vya Habari leo mkoani Dar es Salaam.PICHA NA MICHUZI JR-MMG.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2