WADAU WA USAFIRISHAJI NCHINI WATOA NENO SHERIA UBEBAJI MIZIGO ZAMBIA KATIKA BANDARI YA DAR | Tarimo Blog


*Waiomba Serikali kuchukua hatua haraka, kwani inaonesha ukandamizaji
 

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV

WADAU wa usafirishaji katika bandari ya Dar es Salaam ukiwemo Uwakilishi wa Vyama vya usafirishaji na Chama cha Wakala wa Bandari wametoa pongezi kwa Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imekuwa ikitatua changamoto zao kwa spidi ya kuridhisha.

Mbali ya pongezi hizo, wadau hao wametoa ombi kwa Serikali kuhakikisha inashughulikia changamoto ambayo imejitokeza baada ya wadau wenzao wa Zambia kuwa na sheria ambayo inaeleza wasifirishaji wa mizigo kutoka nchini Zambia ndio wanaotakiwa kusafirisha mizigo ya bandari ya Dar es Salaam inayokwenda nchini kwao kwa asilimia 50.

Wamesema ni vema Serikali ikatoa utatuzi wa changamoto hiyo huku wakiweka wazi , Watanzania wako tayari kushindana na majirani zao wa Zambia kwa ushindani wa bei, ubora wa huduma na usawa lakini sio kushindana kwa kutumia sheria inayokandamiza upande mmoja kwani hata Jumuiya ya SADC imeruhusu ushindani unaozingatia usawa katika kufanya biashara huru kwa nchi wanachama wa jumuiya hiyo.

Akizungumza leo Juni 24,2021 jijini Dar es Salaam, Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Bw.Elias Lukumay   amesema wadau hao wanapongeza hatua ya Serikali kuboresha bandari hiyo ili iweze kubeba mizigo tani milioni 30 na spidi ambayo Rais Samia anakwenda nayo wanaamini hilo linawezekana.

Pamoja na mafanikio yaliyopo amesema  wadau hao wameona haja ya kuzungumzia mjadala unaondelea wa suala la SI ambalo haliko ndani ya Serikali ya Tanzania bali liko nje ya Serikali."Ni jambo ambalo limezungumzwa kwenye vyombo vya habari, hivyo nasi tunaona tuzungumze kidogo, wenzetu wa kule Zambia ni wadau wakubwa wa bandari ya Dar es Salaam, mizigo mingi inakwenda Congo na Zambia ambayo ni mtumiaji wa pili wa bandari yetu.

"Kwa hiyo ni mdau muhimu sana,lakini upande wa Zambia tumeona changamoto moja ambayo ni lazima kuisemea kwasababu ni ya kitaifa, Zambia ni wanachama wa jumuiya ya SADC na jumuiya hiyo ina taratibu zake,inataka kuwe na ufanyaji wa biashara wa soko huria, tushinde kwa huduma bora, bei nzuri, tusishindane kwa hila.

"Tunachokiona kwa wenzetu ni jambo ambalo linahitaji kutolewa ufafanuzi kidogo .Kitu kinachoitwa SI maana yake ni nini? Wazambia wanataka jinsi ya kubeba mzigo ya Zambia katika bandari ya Dar es Salaam kwenda Zambia na mzigo wa zambia kuja Dar. Wanasema mizigo ya Wazambia ambayo mingi ni mafuta na Copa asilimia 50 ibebebwe  na wao.

"Hii maana yake ni nini?Mzambia kwa maana ya ni Mzambia kwa uraia, awe amezaliwa kule au ameoa, hivyo ukienda kule huwezi kupata nafasi hiyo, asilimia 30 ya mizigo  ndio ibebwe na TAZARA na asilimia 20 iliyobakia ibebwe na wengine, kumbukeni hapa nyumbani kuna wasafirishaji ambao wamekuwa kwenye biashara hiyo  kwa muda mrefu,"amesema 

Ameongeza wadau hao waliopo nchni wamekopa fedha na wamewekeza kwenye biashara hiyo."Leo tukifika tunagawana biashara hii kwa asilimia maana yeke watanzania waliowekeza watafilisika na watakosa mizigo lakini Mungu aliyetupa bandari hii tutaona kama urembo, tutakuwa tunaona magari ya wenzetu tu yanapita. 

"Sisi hatupingani na mtu yoyote anayetaka kufanya biashara kwa soko hurua, tuko tayari kushinda kwa ubora wa huduma kwa bei lakini hatuko tayari kuona tunashinda kwa watu kutumia sheria kukandamiza wengine, kwa hiyo tukasema katika kuboresha huduma zetu ni vizuri tukaona Serikali inachukua hili jambo kama changamoto.

"Wasafirishaji wa tanzania wanatumia lita za mafuta milioni mbili wakiweka Zambia na kurudi na wanaporudi wanachukua mizigo ya nafaka kwa ajili ya kuleta Dar es Salaam na hivyo bei ya mazao ya nafaka kuwa chini kutokana na kusafirishwa na usafiri wa malori,hivyo tunahitaji kufanya biashara na wenzetu wa Zambia kwa ushindani wa kibiashara sio kutumia sheria kushindana kibiashara.

"Na hii tunaisema kwa nia njema tukiamini sisi kama nchi hatuwezi kuruhusu utaratibu huo lakini pia hatutaki kuwanyima Wazambia stahili yao ya msingi ya kuja kuchukua mzigo, tunachosema tushindane kwa huduma na hizi huduma ndizo zitakazoamua nani atafanya zaidi lakini sio kutumia sheria,"amesema.

 Kwa upande wake Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Forodha Elitunu Maramia amesema wao kama wadau wa usafirishiji ambao wanahusika na uchakati wa kuondosha mizigo inayoingia Tanzania na ile inayoondoka, wamekaa na wadau wenzao wa uchukuzi, usafirishaji na wamiliki wa malori na Chama cha Wamiliki wa usafirishaji (TOT) na wameamua kufanya tathimini ya sekta inavyokwenda.

Amesema wameona kuna mambo ambayo Serikali inapaswa kutekelezwa kwa spidi kubwa ambayo ndani ya miezi mitatu ya awamu ya sita wameiona na kikubwa wamekiona na kuthaminiwa, Serikali katika kipindi hicho imesogea karibu na wadau hao na kusikiliza changamoto walizonazo na kuzipatia ufumbuzi kwa spidi.

Pia amesema wameona jinsi Serikali imewekeza kwa kiwango kikubwa kwenye miundombinu ikiwemo upanuzi wa bandari , kuongeza kina cha bandari , ujenzi wa mindombinu ya barabara na reli."Tunamshukuru Rais Samia amejipanga kuindeleza sekta hii na kuikuza, sekta ya uchukuzi ni sekta wezeshi kwenye uchumi na inachangia kwa asilimia nane.

"Sasa kwenye uchumi na vile vile inasadia sekta nyingine ziweze kukua kwa kasi, tunavchokiona pia sisi kama nchi sio tu tunahudumia soko la ndani bali tunahudumia na soko la nchi jirani kam Zambia, Congo na nyinginezo na kwenye hili tunaona Serikali inatakiwa kama ambavyo tunashauri inapaswa kuiona sekta binafsi kama mbia.

"Sekta ya umma na sekta binafsi zinatakiwa kushirikiana kutatua changamoto na kupanga mipango ya pamoja, tani milioni 30 kupitia Bandari ya Dar es Salaam inawezekana na mambo ambayo tunashauri ili kufikia tani hizo milioni 30 za mizigo ni pamoja na kushirikiana na sekta binafsi,"amesema.

Pia amesema kuna haja ya Serikali kuiangalia kwa kina na kuifafanua sheria inayozungumzwa nchini Zambia kwani kama ikiachwa iendelee ilivyo inaweza kuathiri nchi yetu kwa maana ya kubeba mizigo inayopita hapa nchini.

Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Malori Tanzania (TATOA), Bw.Elias Lukumay akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam

Katibu Mtendaji wa Chama cha Mawakala wa Forodha Tanzania (TAFFA), Bw. Elitunu Mallamia akizungumza na waandishi wa habari leo Jijini Dar es Salaam.



Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2