WAZIRI DK NDUMBARO AMSIMAMISHA KAZI MENEJA WA SHAMBA LA HIFADHI YA MISITU LA SILAYO | Tarimo Blog


Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo.


Charles James, Michuzi TV

WAZIRI wa Maliasili na Utalii, Dk Damas Ndumbaro amemsimamisha kazi Meneja wa Shamba la hifadhi ya misitu la Silayo lililopo Bukombe Mkoani Geita.

Dk Ndumbaro amefikia uamuzi huo baada ya kuwepo malalamiko kuwa Meneja huyo, Thadeus Shirima amefanya operesheni ya kuwaondoa watu bila kuwa na kibali Maalum kutoka Wizarani.

Akizungumza na wandishi wa habari jijini Dodoma leo, Waziri Dk Ndumbaro amesema kuwa tayari ameshamuagiza Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii kumsimamisha Meneja huyo huku akiunda Timu ya uchunguzi aliyoipa muda wa wiki mbili.

" Ndugu wanahabari tumewaita hapa kutolea ufafanuzi juu ya malalamiko yaliyotolewa na Mbunge wa Jimbo la Bukombe, Dotto Biteko kuhusu Meneja wetu huyo kufanya operesheni ambayo imewasababishia uharibifu na hasara wananchi wa maeneo hayo.

Hivyo kufuatia malalamiko hayo tunamsimamisha kazi Meneja wa Msitu huo, Thadeus Shirima kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili, na nimuagize Katibu Mkuu kupeleka Meneja mwingine," Amesema Dk Ndumbaro.

Waziri Dk Ndumbaro amesema kitendo kilichofanywa na Meneja huyo kufanya operesheni kinyume na maelekezo ya wizara ni kuchafua sura ya Serikali ya Rais Samia Suluhu Hassan ambayo imejielekeza katika kufanya kazi kwa weledi, sheria na haki.

Ametoa onyo kwa mameneja wengine na watumishi wa Wizara ya Maliasili na Utalii kuacha kufanya operesheni ambazo hazina maelekezo ya wizara na yeyote atakaekiuka atachukuliwa hatua za kinidhamu.


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2