WAZIRI JAFO AWATAKA WASHAURI ELEKEZI WA MAZINGIRA KUFANYA KAZI ZAO KWA UFANISI | Tarimo Blog

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (katikati), akionyesha zawadi aliyopewa na Chama cha Wataalamu wa Mazingira Tanzania (TEEA), baada ya ufunguzi wa mkutano huo uliofanyika Millenium Tower Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Mwenyekiti wa TEEA Prof. Hussein Sosovere pamoja na mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. Esnat Chaggu (kushoto).

 Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (katikati), akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa Mkutano wa Wataalam Elekezi wa Mazingira Tanzania (TEEA). Wa pili kulia ni Mwenyekiti wa Chama cha Wataalamu wa Mazingira Tanzania Prof. Hussein Sosovere, Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. Esnat chaggu (wa pili kushoto) pamoja na Mkurugenzi Mkuu wa NEMC Dkt. Samuel Gwamaka (wa tatu kushoto).
 Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka, akizungumza na wadau wa mazingira katika Mkutano wa Chama cha Wataalam Elekezi wa Mazingira Tanzania, uliofanyika katika ukumbi wa Millenium Tower Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo, akifungua mkutano wa Wataalam Elekezi wa Mazingira, uliofanyika Millenium Tower Kijitonyama Jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya Washiriki wa Mkutano wa Chama cha Wataalam Elekezi wa Mazingira wakisikiliza kwa makini hotuba inayotolewa na Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Selemani Jafo (hayupo pichani).

WAZIRI wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais Muungano na Mazingira Mhe. Selemani Jafo, amewataka washauri elekezi wa Mazingira kufanya kazi zao kwa ufanisi na kwa kufata sheria ya mazingira, kwani Taifa linawategemea katika kuhakikisha mazingira yanakuwa salama kutokana na utaalam walionao.

Ameyasema hayo alipokuwa akizungumza katika mkutano wa Wataalamu Elekezi wa Mazingira Tanzania, uliofanyika Millenium Tower, ukumbi wa LAPF, Kijitonyama Jijini Dar es Salaam. Amesema kuwa wataalam wa mazingira wana kazi kubwa sana kama tunavyofahamu ajenda kubwa ya Taifa ni kuvutia wawekezaji lakini katika uwekezaji huo kama wataalam hawatafanya kazi zao kisanifu basi uwekezaji huo utasuasua na kupelekea athari kubwa katika taifa letu upande wa mazingira.

Aidha Mhe. Jafo amewataka wataalamu hao kuwa kinara katika kutoa ushauri wa mazingira kwa wawekezaji ili tuwe na uwekezaji wenye tija na manufaa katika jamii yetu. Ameendelea kusema lengo kubwa la mkutano huu ni kuweza kujengea uwezo na kupitishana katika kanuni mpya iliyoundwa ya washauri elekezi, lakini pia kupitia mfumo wa namna ya kusajili miradi kwa mtandao, hivyo kupitia mkutano huu wataalam wa mazingira watakuwa mahiri katika utendaji wao.

“Naamini kupitia Mkutano huu mtakuwa mmejifunza vitu vikubwa sana, kwa wataalam hawa na ambao hawapo hapa watakuwa wamekosa kitu kikubwa sana siku ya leo. Mfumo wa kielektroniki ni mzuri sana hii itasaidia kuepusha malalamiko kutoka pande zote tatu kwa mtaalam, NEMC na muwekezaji mwenyewe. Napenda niwaambie wawekezaji kuwa suala la kufanya Tathmini ya Athari kwa Mazingira (TAM) ni jambo muhimu sana hii ni kwa ajili ya manufaa ya muwekezaji pamoja na Mazingira yetu.”

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) Dkt. Samuel Gwamaka amesema kuwa, hapo awali kulikuwa na kanuni za wataalam elekezi wa mazingira za mwaka 2005 ambazo zimefutwa kwa sasa na kuundwa kanuni mpya ambazo zimeanza rasmi tarehe 19/3/2021. Kutokana na majukumu ya Baraza tumetumia fursa hii kushirikiana na Chama cha Wataalam wa Mazingira Tanzania (TEEA) kuweza kupeana ushauri na maelekezo ili kuweza kuhakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa weledi na kwa mujibu wa sheria.

Vile vile Mwenyekiti wa Bodi ya NEMC Prof. Esnat Chaggu amesema kuwa, mkutano huu una faida kubwa katika Taifa letu hivyo amewaomba wataalamu hao kuzingatia maelekezo watakayopewa ili kuweza kufanya kazi zao kwa umahiri na uadilifu ili kuweza kuongeza uaminifu katika jamii yetu na kuhakikisha mazingira yetu yanalindwa.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa TEEA Prof. Hussein Sosovele amesema, NEMC ishirikiane kwa karibu na chama cha wataalam wa Mazingira Tanzania ili kuweza kutekeleza kanuni hizo mpya ambazo zimepitishwa kwani kanuni hizo zinawahusu wataalam hao na pia ni chanzo cha mapato kwa Taifa. Ameendelea kusema kuwa lengo la Kanuni hizo mpya ni kwaajili ya namna ya kuwasajili na kutoa mafunzo kwa wataalam hao, kwani hii ni kuweza kuwasaidia wataalam kujirekebisha na kujisahihisha pale panapokuwa na makosa ya kiutendaji.

Mwisho Mhe. Jafo amesema kuwa wataalam wa Mazingira wanatakiwa kuhakikisha mazingira yetu hayaharibiki kutokana na shughuli za kijamii, hivyo amewataka wataalamu hao kuzingatia kanuni hiyo kwa kuandika andiko lililo sahihi kwani unapoandaa andiko ambalo haliko vizuri husababisha tasnia hii ambayo ni muhimu kwa Taifa kushuka hadhi yake na kupelekea kukosa wataalam elekezi wa Mazingira mahiri. Vile vile Mhe. Jafo amewataka wawekezaji wote kusajili miradi yao ili kufanya Tathmini ya Mazingira bila kushurutishwa kwani hili ni takwa la kisheria.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2