TAMKO LA KILELE CHA MAADHIMISHO YA SIKU YA HOMA YA INI DUNIANI | Tarimo Blog

Mratibu wa Ugonjwa wa Homa ya ini kutoka Wizara ya Afya Dkt. Baraka Nzobo akizungumza na Waandishi wa habari (Hawapo Pichani) wakati akisoma Tamko la SIku ya Maadhimisho ya ya Siku ya Homa ya Ini Duniani kwa niaba ya Waziri wa Afya Dkt. Dorothy Gwajima.

 


TAREHE 28 JULAI, 2021

 

Ndugu Wanahabari

Tarehe 28 Julai ya kila mwaka, ni siku iliyoteuliwa na Shirika la Afya Duniani (WHO) kama siku ya Homa ya Ini (World Hepatitis Day). Lengo kuu la maadhimisho haya ni kuielimisha na kuikumbusha jamii kutambua athari za ugonjwa wa Homa ya Ini, jinsi ugonjwa huu unavyoambukizwa, na namna ya kujikinga na ugonjwa huu. Ni jambo muhimu kwa nchi zote duniani kushirikiana katika kupambana na ugonjwa huu.

 Ndugu Wanahabari

Katika kuadhimisha Siku hii, kila mwaka Shirika la Afya Duniani hutoa kauli mbiu yenye ujumbe maalum, unaolenga kuhamasisha na kuelimisha jamii kuhusu madhara yanayotokana na ugonjwa huu. Kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Homa ya Ini Duniani kwa mwaka huu wa 2021 ni: - Tusisubiri “Kupima, Kuanza Matibabu na kupata Chanjo ya Homa ya Ini” (“Hepatitis Can’t Wait).

Kauli mbiu hii inatulazimu sisi kama Serikali kuweka mikakati ya pamoja na wananchi ili kuweza kudhibiti ugonjwa huu nchini na hatimaye kuweza kuutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.

 

Ndugu Wanahabari

Maadhimisho haya pia yanatoa fursa ya nchi yetu kuongeza juhudi

za kutekeleza Mpango Mkakati wa kwanza wa Tanzania wa Homa ya Ini (National Strategic Plan for the Control of Viral Hepatitis) kwa mwaka 2018-2023, ambao tuliutengeneza ukiwa na lengo la kuwezesha nchi kuudhibiti Ugonjwa wa Homa ya Ini,hadi kufikia kiwango ambacho itakuwa si tatizo kubwa la kiafya katika Jamii.

 

Ndugu Wanahabari

Ugonjwa wa Homa ya Ini ni tatizo linalohitaji juhudi za dhati kupambana nalo. Ugonjwa huu umetajwa kuwa wa hatari na unaoua idadi kubwa ya watu pole pole. Kati ya watu 100, watu 8 wanaweza kuwa na maambukizi sugu ya ugonjwa huu na wanaweza wasioneshe dalili zozote na kwamba asilimia kubwa ya wagonjwa huugundua ugonjwa huu kwenye hatua za mwisho na hivyo kushindwa kupata matibabu mapema na kupelekea mgonjwa kupoteza maisha.

 

Ndugu Wanahabari,

Maambukizi ya Homa ya Ini husababishwa na virusi ambavyo vinapoingia mwilini mwa binadamu, hushambulia ini na hivyo kulifanya wakati mwingine lisinyae na kushindwa kufanya kazi vizuri. Katika hatua za mwishoni mwathirika wa ugonjwa huu anaweza kupata saratani ya ini. Ugonjwa huu unaenezwa kwa njia mbalimbali kulingana na kundi la virusi hivi. Virusi vya homa ya ini vipo katika makundi matano, yaani A, B, C, D na E.

Uhakika wa mgonjwa kuwa na maambukizi haya hupatikana kwa kufanyiwa vipimo maalum vya kimaabara.

 

Ndugu Wanahabari

Takwimu za Shirika la Afya Duniani zinaonesha kuwa, watu 884,000 hufariki kila mwaka kutokana na matatizo yanayotokana na Homa ya Ini hasa saratani ya Ini. Inakadiriwa kuwa kila baada ya dakika mbili watu wawili hufariki kutokana na homa ya ini duniani

 

Ndugu Wanahabari,

Kwa Tanzania, takwimu kutoka Mpango wa Taifa wa Damu Salama (NBTS) zinaonesha kuwa maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B kwa wachangiaji damu kwa miaka mitatu mfululizo yalikuwa kama ifuatavyo:

·        Mwaka 2018, kati ya wachangiaji damu 307,835, takribani watu 13,613 (asilimia 4.4) walikuwa na maambukizi.

·        Mwaka 2019, kati ya wachangiaji damu 258,779, takribani watu 14,123 (asilimia 5.5) walikuwa na maambukizi.

·        Mwaka 2020, kati ya wachangiaji damu 263,119, takribani watu 15,923 (asilimia 6.1) walikuwa na maambukizi.

Mikoa iliyokuwa na maambukizi makubwa ya Homa ya Ini kwa mwaka 2020 kwenye kundi la watu wanaochangia damu ni; Mara asilimia 9.3, Geita asilimia 8.7, Morogoro asilimia 7.7, Rukwa asilimia 7.6 na Shinyanga asilimia 7.4.

Kwa upande wa Homa ya Ini inayosababishwa na virusi aina ya C maambukizi yalikuwa kama ifuatavyo:

·        Mwaka 2019 kati ya wachangiaji wa damu 258,779, takribani watu 5,344 (asilimia 2.1) walikuwa na maambukizi.

·         Mwaka 2020, kati ya wachangiaji damu 263,119, takribani watu 6,914 (asilimia 2.6) walikuwa na maambukizi.

Mikoa iliyoongoza kwa maambukizi ya Homa ya Ini aina ya C kwa mwaka 2020 kwenye kundi la wachangiaji damuni: Mtwara asilimia 5.5, Ruvuma asilimia 4.6, Kilimanjaro, Geita asilimia 4.6 na Lindi asilimia 4.5.

Aidha, utafiti mahususi ujulikanao kama “THIS”, unaoratibiwa na Ofisi ya Taifa ya Takwimu, umeonesha kuwa maambukizi ya Homa ya Ini aina ya B ni asilimia 4.0 miongoni mwa watanzania wenye umri kati ya miaka 15-49, kwa mwaka 2017.

 

Ndugu Wanahabari

Matibabu ya Homa ya Ini ni ya gharama kubwa na ndio maana tunasema kinga ni bora kuliko Tiba. Tiba kwa Wagonjwa waliopata kirusi aina ya A na E,mara nyingi hutolewa kutokana na dalili zinazoambatana na ugonjwa huu. Kwa wagonjwa waliogundulika kuwa na Hepatitis B au C, matibabu hutegemea hatua mgonjwa aliyofikia. Wakati mwingine hulazimika kupewa dawa za kupunguza makali ya virusi vya ugonjwa huo kwa kipindi chote cha uhai wake. Gharama za dawa hizi ni kubwa sana. Kwa mgonjwa aliyepata maambukizi ya Homa ya Ini kupitia Virusi aina ya C, gharama ya dawa ni kati ya shilingi Milioni Tatu hadi Tano kulingana na muda wa tiba. Kupitia mradi maalum wa awali (“Hepatitis B Pilot project”), matibabu kwa wagonjwa walioathirika yanatolewa bila malipo katika hospitali ya Taifa Muhimbili.

 

Ndugu Wanahabari

Ugonjwa huu unaweza kukingwa kwa kutumia chanjo ambayo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo. Kwa maambukizi ya kirusi aina ya B, chanjo ya ugonjwa huo hutolewa kwa mtu asiye na maambukizi ya virusi hivyo na hutoa kinga kwa kipindi chote cha maisha yake. Hivyo, ninawasisitiza wananchi kwenda kufanyiwa uchunguzi wa homa ya Ini, na kwa wale ambao hawatakutwa na maambukizi ya virusi vya hepatitis B watapatiwa chanjo hiyo kwa gharama nafuu katika hospitali za serikali. Chanjo hii hutolewa katika Hospitali 28 za Rufaa za Mikoa, Hospital za Rufaa za Kanda pamoja na vituo 21 vilivyopo maeneo ya mipakani. Huduma hii ya chanjo kwa watu wazima inatolewa kwa bei elekezi ya serikali, ambapo gharama ya kipimo ni shilingi 10,000, na kila dozi inagharimu shilingi 10,000, kufikia jumla ya dozi tatu. Aidha, Hospitali za Ocean Road, Benjamin Mkapa, Muhimbili Orthopaedic Institute, Hospitali ya KCMC na Hospitali ya Bugando, pia zinatoa chanjo ya Homa ya Ini aina ya B kwa watu wazima kwa utaratibu wa kuchangia gharama.  Naziagiza hospitali binafsi na za mashirika ya kidini, kushusha gharama za upimaji na utoaji wa chanjo ya homa ya Ini ili huduma hii iweze kuwafikia wananchi wote.

Ni matarajio yangu kuwa gharama hizi zitapungua kwa kiasi kikubwa na kuwezesha chanjo kupatikana katika vituo vingi vya kutolea tiba hasa vya umma baada ya uamuzi wa serikali kununua dawa moja kwa moja kutoka kwa wazalishaji ambapo bei ya chanjo ya Homa ya Ini katika bohari ya dawa (MSD) sasa inauzwa shillingi 5,300 kutoka shilingi 22,000.

Hapa nchini chanjo ya homa ya ini hutolewa kwa watoto wachanga bila malipo. Chanjo hii ambayo ilianza kutolewa kwa watoto wachanga nchini waliozaliwa kuanzia mwaka 2002 ipo kwenye mchanganyiko wa Pentavalenti. Hadi kufikia mwaka 2021, inakadiriwa kuwa asilimia 98% ya watoto walipata chanjo hiyo ya Pentavalent. Chanjo ya Hepatitis A ipo na inatumika kwa baadhi ya nchi lakini hapa nchini kwetu hatujaanza utaratibu wa kutoa chanjo hiyo kwa sabau tatizo kubwa zaidi linalotukabili kwa sasa ni Hepatitis B. Hakuna chanjo dhidi ya Hepatitis C, D na E. Hata hivyo, ugonjwa wa Hepatitis D unaweza kuzuilika kwa kuwachanja watu dhidi ya Hepatitis B.

 

 

Ndugu Wanahabari,

Kama wajibu wa waajiri kuwakinga watumishi wao sehemu za kazi, chanjo ya kuzuia maambukizi ya Hepatitis B hutolewa kwa watumishi wa sekta ya Afya kwa gharama ya serikali. Wizara imekuwa ikiratibu utoaji wa chanjo ya homa ya ini kwa watoa huduma za afya kwa lengo la kuwakinga watumishi wa afya ambao wana hatari mara mbili ya kupata ugonjwa huu. Kwanza kwa kupata maambukizi wawapo kazini katika kutekeleza majukumu yao ya kila siku ya kutoa huduma za afya na pili wanapokuwa katika jamii kama sehemu ya jamii. Kwa upande mwingine, sekta binafsi zina utaratibu wao wa kugharamia chanjo kwa ajili ya kuwakinga watumishi wao sehemu za kazi. 

 

Ndugu Wanahabari

Makundi hatarishi kwenye maambukizi ya Homa ya Ini aina B na C ni kama yafuatayo: Watumishi wa afya, Wanaume wanaofanya ngono na Wanaume wenzao, Watu wanaojidunga madawa ya kulevya, Watu wenye wapenzi wengi, watu wenye magonjwa sugu ya ini na figo, Wazee kuanzia miaka 60 wenye kisukari na watu wanaosafiri kwenda kwenye nchi ze maambukizi makubwa ya Hepatitis B.

Makundi haya yanatakiwa kujikinga na maambukizi ya Hepatitis B kwa kufanya yafuatayo.

1. Kupima na kujua hali ya maambukizi, kisha kupata chanjo ya Hepatitis B

2. Kufanya ngono salama kwa kutumia Kondomu

3. Kupunguza idadi kubwa ya wapenzi wengi

4. Kuacha kujidunga Madawa ya kulevya, kwani wengi hushirikiana kutumia sindano moja kwenye kitendo cha kujidunga madawa ya kulevya.

 

Ndugu Wanahabari

Hatua zinazofanyika na Wizara katika kudhibiti Homa ya Ini ni pamoja na  

1. Kusimamia Mpango Mkakati wa Taifa wa Kudhibiti na Kutokomeza Ugonjwa wa Homa ya Ini nchini wa mwaka 2018-2023. Wizara pia inakamilisha Muongozo wa matibabu ya Homa ya Ini ambao utatumika kutoa maelekezo ya tiba hiyo nchi nzima ili kumpunguzia mwananchi gharama ya kusafiri umbali mrefu kwenda kupata tiba hiyo katka Hospitali ya Taifa Muhimbili.

2. Kuandaa vielelezo vinavyohusu ugonjwa wa Homa ya Ini (Viral Hepatitis), ili kuuelimisha umma juu ya ugonjwa huu na namna gani maambukizi yanaweza kuzuiwa.

 

3. Kuendelea kutoa chanjo ya hepatitis B kwa watumishi wa afya walio katika mazingira hatarishi.

4.  Aidha, Wizara inakamilisha mipango ya uwezekano wa kuhakikisha chanjo hii ya Hepatitis B inapatikana kwa watu wote wanaohitaji na kwa gharama nafuu.

5. Kuanzisha huduma ya kinga ya maambukizi ya homa ya Ini kutoka kwa mama mjamzito kwenda kwa mtoto.

 

Ndugu Wanahabari,

Kwa sasa hakuna ushahidi wa mlipuko wa Homa ya Ini nchini. Hata hivyo, wananchi wa Tanzania na Afrika Mashariki wapo katika hatari ya kupata maambukizi ya ugonjwa huu, hususan Hepatitis B na C, kuliko aina nyingine, yaani A, D na E kutokana na kuwa njia za maambukizi ya Virusi hivi vya aina ya B na C hufanana kwa kiasi kikubwa na zile za maambukizi ya VVU.

 

Leo tunapoadhimisha Siku ya Homa ya Ini, na ili tuweze kwenda sambamba na mataifa mengine duniani, katika kufanikisha Ajenda ya Maendeleo Endelevu ifikapo mwaka 2030, Msisitizo wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto ni kwa wananchi na wadau wote kuendelea kuona umuhimu na kutoa kipaumbele katika mapambano dhidi ya ugonjwa wa Homa ya Ini  hususan kwa kutumia fursa zilizopo na  kuwekeza katika mapambano dhidi ya ugonjwa huu.

 

aomba nihitimishe kwa kuwataka wafanyakazi wa Mpango wa Damu Salama kuendelea na kazi nzuri ya kupima damu zote za wachangiaji, kuwaomba wafanyakazi wa sekta ya afya kuzingatia kanuni za usalama, kuwashauri jamii kuepuka na kujidunga madawa ya kulevya, kuepuka ngono zembe, na mwisho kabisa kuwaomba wadau wote kushirikiana na Serikali katika juhudi za kuondoa ugonjwa wa Homa ya Ini hapa nchini ifikapo mwaka 2030.

Asanteni kwa kunisikiliza

 

Dkt. Dorothy Gwajima (Mb)

WAZIRI WA AFYA, MAENDELEO YA JAMII, JINSIA, WAZEE NA WATOTO


Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2