WASTAAFU WAASWA KUWA MAKINI NA WIZI WA MITANDAONI | Tarimo Blog

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, mahakama ya Tanzania, Edward J.K Nkembo akifungua rasmi mafunzo ya kujiandaa kustaafu kwa watumishi wa Mahakama ya Tanzania ambao hawapo pichani.
Picha mbalimbali za washiriki wa mafunzo ya kujiandaa kustaafu wakifuatilia ufunguzi wa mafunzo hayo yaliyofanyika katika ukumbi wa Magadu mkoani Morogoro.

Mkurugenzi wa Utawala na Rasilimaliwatu, mahakama ya Tanzania, Edward J.K Nkembo aliyeketi katikati kulia ni mtendaji wa mahakama ya hakimu mkazi morogoro Nestory Mujunangoma na kushoto ni Mhadhiri wa chuo cha Uongozi wa mahakama Lushoto, Nuhu Mtekele na Mratibu wa Mafunzo wakiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mafunzo yaliyofanyika Morogoro.

MKURUGENZI wa Utawala na Rasilimaliwatu wa Mahakama ya Tanzania Bwana Edward J.K. Nkembo amefungua rasmi mafunzo ya kujiandaa kustaafu kwa Watumishi wapatao 84 wa Mahakama ya Tanzania kutoka kwenye kanda mbalimbali za Mahakama ya Tanzania. Mafunzo haya yanafanyika katika ukumbi wa Magadu uliopo mkoani Morogoro kwa muda wa siku tano kuanzia tarehe 26 mpaka 30 Julai, 2021.

Bwana Nkembo, alipokuwa akifungua mafunzo hayo aliwapongeza washiriki hao kwa kuwa watumishi bora kwa muda wote waliotumikia Mahakama ya Tanzania mpaka utumishi wao unapokoma. Pia aliendelea kwa kuwasisitiza washiriki hao kuwa makini na wizi wa mitandaoni na kwamba utapeli na rushwa ni matukio mabaya ambayo wastaafu wengi wamekutana nayo na kuwataka kuchukua tahadhari zote za kukabiliana nayo.

Kwa upande wake, Mtendaji wa Mahakama ya Tanzania, mkoa wa Morogoro ndugu Nestory Mujunangoma amewataka washiriki hao kufanya maandalizi ya kustaafu mapema na kuchukua maamuzi sahihi ambayo hayataathiri maisha yao baada ya kustaafu huku akilinganisha kustaafu kama kubadili gia kwenye gari na kwamba maisha yanaendelea hata baada ya kustaafu kama ambavyo gari huendelea hata baada ya kubadili gia.

Naye Mratibu wa Mafunzo hayo Ndugu Nuhu Mtekele, Mhadhiri wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto aliewaeleza washiriki hao kuwa mafunzo hayo ni mpango wa utekelezaji wa Sera ya Mafunzo ya Utumishi wa Umma ya Mwaka 2013, Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania, Sera ya Mafunzo ya Mahakama ya Tanzania ya mwaka 2019 pamoja Mpango Mkakati wa Chuo wa miaka mitano wa mwaka 2018/19-2022/23.

Ndugu Mtekele aliendelea kwa kusema kuwa pamoja na mafunzo ya darasani, washiriki watapata fursa ya kutembelea Chuo Kikuu cha kilimo cha Sokoine (SUA) kilichopo mkoani Morogoro ili kujionea kwa vitendo miradi na shughuli za ujasiriamali na uwekezaji katika nyanja za kilimo na ufugaji na zile ambazo wanaweza kupenda kuzifanya na hatimaye kuwasaidia kimaendeleo baada ya kustaafu.

Mafunzo hayo yameratibiwa na kuendeshwa na Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto. Mafunzo hayo yamejumuisha washiriki wa kada mbalimbali wakiwepo mahakimu, wasaidizi wa kumbukumbu, makatibu mahususi, walinzi n.k.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2