VIONGOZI KATA YA KIBADA WAHAMASISHA USAFI WA MAZINGIRA,WANANCHI KUJIKINGA NA CORONA | Tarimo Blog


Na Said Mwishehe, Michuzi TV

VIONGOZI wa ngazi mbalimbali katika Kata ya Kibada wilayani Kigamboni mkoani Dar es Salaam wameshiriki kuhamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira pamoja na kuwahimiza kuchukua tahadhari ili kukabiliana na janga la Corona.

Miongoni mwa viongozi walioshiriki kufanya usafi kwa kushirikiana na wananchi wa Kibada ni Ofisa Tarafa wa Somangila Augusta Safari, Diwani wa Kata ya Kibada Amiri Sambo, Mwanasheria wa Manispaa ya Kigamboni Charles Lawiso , maofisa watendaji Kibada pamoja na wenye viti wa mtaa.

Akizungumza na waandishi wa habari ,Diwani wa Kata ya Kibada Amiri Sambo amesema viongozi hao wameamua kuhamasisha usafi na wananchi kuendelea kuchukua tahadhari ya Corona kwa kuvaa barakoa na kunawa maji kwa sabuni na maji tiririka.

"Rais wetu mpendwa Mama Samia Suluhu Hassan ametuhamasisha tuchukue tahahadhari kwa ajili ya Corona, hivyo tumekuja kuwaambia wananchi umuhimu wa kuchukua tahadhari kwa kufuata maelekezo yanayotolewa na Wizara ya Afya na watalaamu wa afya.

"Pia tumekuja kuhamasisha usafi, kwa hiyo leo viongozi wa Kata ya Kibada tukiongozwa na Ofisa Tara wetu tumekutana kufanya safi wa pamoja katika eneo hili.Hali ya usafi Kata ya Kibada sio mbaya lakini ni vema tukaendelea kusimamia kwani tusipoasimamia uchafu utakuwa mwingi na kuhatarisha afya za wananchi.

Aidha wakati wakiendelea kuhamasisha usafi, amefafanua kuna mipango mizuri ya Serikali kwa wafanyabiashara wa wananchi wa Kibada ambapo hivi sasa ujenzi wa soko unaendelea na Oktoba mwaka huu litakuwa limekamilika , litakuwa na vizimba 173.

"Tunaishukuru Serikali ilivyojitoa kwa ajili yetu, kwa hiyo wafanyabiashara wadogo wadogo 173 watapa vizimba ,wenye bucha watapata na hii inakwenda kuondoa kero ya wafanyabishara kupanga biashara kando ya barabara."

Kwa upande wake Ofisa Tarafa Somangila wilayani Kigamboni Augusta Safari amesema wameendelea kuhamasisha usafi katika meneo ya Wilaya hiyo ikiwa ni sehemu ya kipaumbele cha Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Amos Makala.Pia Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni Fatma Nyangasa amekuwa akiwahimiza viongozi kusimamia usafi kwenye maeneo yao.

"Kwa hiyo sisi viongozi ambao ni wasadizi wa Mkuu wa Wilaya ya Kigamboni leo tumekuja Kibada kuhamasisha usafi kwa kuwashirikisha viongozi wa kata na mitaa. Lakini lengo letu kubwa ni kukumbusha wananchi lazima tushirki kufanya usafi katika maeneo yetu kwani tunakinga afya zetu, pia tunapofanya usafi tutajikinga na magonjwa yakiwemo ya mlipuko.

"Tumepita kwenye hospitali, vituo vya afya, maeneo ya sokoni na kwa wananchi ambako kote huko tumeshiriki kufanya usafi na kuhamasisha wananchi kuweka mazingira yao katika usafi.Pia wakati tukiendelea kufanya yote haya Rais wetu ameendelea kusisitiza tuendelee kujenga uchumi lakini tusisahau kuchukua tahadhari dhidi ya Corona,"amesema Safari.

Wakati huo huo Mwanasheria wa Wilaya ya Kigamboni Charles Lawiso amewakumbusha wananchi hasa wafanyabiashara kwamba kufanya usafi kila Jumamosi ya mwisho wa mwezi ni jambo ambalo lipo kwa mujibu wa sheria, hivyo wafanyabiashara wanatakiwa kufanya usafi bila kushurutishwa na watakaokaidi kuna faini inayoanzia Sh.50,000 hadi Sh.300,000.

"Hivyo kila ifikapo Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi wafanyabiashara wanatakiwa kufanya usafi kuanzia saa 12 asubuhi hadi saa tatu asubuhi na baada ya hapo ndipo watafungua maeneo yao ya biashara, hivyo tumendelea kuhamasisha na kutoa elimu katika Kata mbalimbali na leo tuko Kata ya Kibada , tumetoa elimu kwa baadhi ya wananchi ambao wamefungua maduka yao bila kufanya usafi lakini na adhabu ambazo wanaweza kuzipata iwapo watakaidi kwa miezi inayokuja,"amesema.

Amesema siku ya usafi imewekea sheria, hiyo kwa watakaokiuka watatozwa faini,lakini kikubwa wamewaelimisha wananchi hakuna sababu ya kusubiria faini."Hapo baadae tutaanza kutoza faini kwa watakaoshindwa kufanya usafi."

Ofisa Tarafa wa Somangila Augusta Safari(kulia) akiwa na Diwani wa Kata ya Kibada wilayani Kigamboni Amiri Sambo(kushoto)wakiwa wamebeba tenga lenye uchafu kwa ajili ya kupeleka kwenye gari la kubeba taka wakati viongozi wa ngazi mbalimbali walipokuwa wakihamasisha usafi wa mazingira ndani ya Kata hiyo na Wilaya kwa ujumla.
Diwani Kata ya Kibada Amiri Sambo(katikati) akiwa kwenye kijiwe cha bodaboda akihamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira na kuwakumbusha kuvaa barakoa na kunawa maji kwa sababu na maji tiririka ili kujikinga na Corona.
Mwanasheria wa Manispaa ya Wilaya ya Kigamboni mkoani Dar es Salaam Charles Lawiso(wa pili kulia) akizungumzia umuhimu wa wananchi kufanya usafi yakiwemo ya biashara kila ifikapo Jumamosi ya mwisho ya kila mwezi na wale ambao watakaidi watatozwa faini ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.
Ofisa Tarafa wa Somangila wilayani Kigamboni Augusta Safari (wa pili kushoto) akisisitiza jambo wakati wa kampeni hiyo ya kuhamasisha wananchi kufanya usafi na kuendelea kuchukua tahadhari ya Corona.Wa kwanza kulia ni Ofisa Afya Kata ya Kibada Yusar Aboubakari na wa pili kulia ni Ofisa Mtendaji Kata Kibada Salome Nyoni.
Diwani wa Kata ya Kibada wilayani Kigamboni Amiri Sambo(kushoto) akiwa na mmoja watendaji katika kata ya Kibada wakiweka maji kwa ajili ya kuwezesha wananchi kunawa mikono kama sehemu ya jitihada za kukabiliana na Corona.
Ofisa Tarafa wa Somangila wilayani Kigamboni Augusta Safari (kulia) akiwa na viongozi wengine wa Kata ya Kibada wakizoa taka wakati wa kampeni ya kuhamasisha usafi wa mazingira ndani ya Kata hiyo.
Diwani wa Kata ya Kibada Amiri Sambo(kulia) akisisitiza jambo.Kushoto ni Ofisa Tarafa wa Somangila Augusta Safari.
Kazi ya uzoaji taka ikiendelea kufanywa na viongozi wa ngazi mbalimbali walioshiriki kufanya usafi wa mazingira Kata ya Kibada wilayani Kigamboni.
Mwanasheria wa Manispaa ya Kigamboni Charles Lawiso (kushoto) akishiriki kufanya usafi baada ya kuwahamasisha wafanyabiashara kushiriki usafi na hasa kila ifikapo Jumamosi ya kila mwisho wa mwezi ambayo ipo kwa mujibu wa sheria.Kulia ni Augusta Safari ambaye ni Ofisa Tarafa wa Somangila.
Viongozi wa Kata ya Kibada wakisafisha tenki la kuweka wakati walipokuwa eneo la Kibada Centre kuhamasisha usafi wa mazingira na wananchi kuchukua tahadhari ya Corona.


Matukio mbalimbali katika picha wakati wa kampeni ya viongozi wa Kata ya Kibada wakihamasisha wananchi kufanya usafi wa mazingira.
 

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2