POLISI WATOA TAMKO KUELEKEA MECHI YA WATANI WA JADI SIMBA NA YANGA, LAONYA WARUSHA CHUPA | Tarimo Blog

Na Mwandishi Wetu, Michuzi TV
WAKATI mashabiki na wapenzi wa soka nchini Tanzania wakisubiri mechi ya watani wa jadi Simba na Yanga zitakazoingia dimbani kesho Aprili 16,2023 , Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam limesema ulinzi umeimarishwa na marufuku mashabiki kwenda na silaya ya aina yoyote uwanjani.

Mchezo huo utachezwa kuanzia saa 11 jioni katika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam huku mashabiki wakiwa na hamu kubwa ya kuushuhudia mchezo huo ambao umesubiriwa kwa muda mrefu.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam Jumanne Muliro amesema kwamba Jeshi hilo limekuwa likichukua tahadhari zote za kiusalama kabla, wakati na baada ya mchezo. Hivyo amewatoa hofu mashabiki watakaofika kushuhudia mchezo huo kuwa usalama utakuwa umeimarishwa kwa kiwango cha juu maeneo yote kuzunguka uwanja huo, ndani, nje na barabarani.

"Ni marufuku kwa mtu yeyote kwenda na silaha uwanjani isipokuwa vyombo vya dola vyenye jukumu la usalama eneo hilo.Jeshi la Polisi Kanda maalum ya Dar es salaam linatoa tahadhari na onyo kali kwa baadhi ya tabia za mashabiki kuwashambulia waaamuzi wasaidizi kwa chupa za maji au chupa zenye vimiminika ambavyo vinadhaniwa kuwa na haja ndogo.

"Wakati ambao huwa hawakubaliani na baadhi ya maamuzi, pia Jeshi la Polisi halitavumilia tabia za baadhi ya mashabiki kuharibu miundombinu ya uwanja kama kuharibu mabomba ya vyoo na bafu pamoja na viti, tabia hizi ni chafu na hazikubaliki na watakofanya vitendo hivyo watakamatwa wakati huo huo au baada ya mchezo kutegemea mazingira ya eneo mtuhumiwa huyo atakapokuwa,"amesema Kamanda Muliro.

Aidha amesema Jeshi la Polisi Kanda Maalum ya Dar es Salaam linashauri pia katika mchezo wa soka au mpira wa miguu hasa kwenye timu zenye upinzani na uwezo unaoonekana kulingana, si vema kwa mashabiki au wapenzi wa timu hizi kwenda uwanjani na matokeo mfukoni kwani matokea yoyote yatakayotokea lazima yakubaliwe na watu waondoke bila vurugu, fujo au kufanya vitendo vya kihalifu.

Mafunzo ya Ufugaji Bora na Matibabu, Jiunge sasa kwa KUBOFYA HAPA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2