Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo.
Simu: 0766054094/0718878887
NIKICHEKA, UTALIA!! Ni simulizi iliyojaa visa, mikasa na matukio mengi, yaliyokuwa yanatokea katika Chuo Kikuu cha Mtakatifu Agustino Tanzania.
simulizi Hii iliyotungwa na Mtunzi mahiri ELIGI GASTO TARIMO inaelezea jinsi ambavyo Riziki anaamua kulipiza kisasi baada ya kufanyiwa ukatili wa ajabu
simulizi Hii iliyotungwa na Mtunzi mahiri ELIGI GASTO TARIMO inaelezea jinsi ambavyo Riziki anaamua kulipiza kisasi baada ya kufanyiwa ukatili wa ajabu
Endelea...........................
Msako mkali unafanyika ndani ya chuo
kikuu cha Mtakatifu Augustino(SAUT) kilichopo jijini Mwanza. Ni msako
unaofanyika kumsaka anaesababisha hali ya taharuki kwa matukio ya ajabu. Msako
wa kumsaka aidha watu, kikundi au mtu asiejulikana anayefanya matukio ya
kustaajabisha. Haijulikani ni mtu au kikundi cha watu lakini ni msako
unafanyika na polisi wenye sare na wasio na sare walitanda kila kona kuondoa
taharuki hiyo.
Asubuhi
hii tukio jipya la kushangaza linaibuka tena. Askari polisi aliyekua analinda
doria anakutwa amefungwa kwenye mti ulio karibu na chuo huku amekatwa masikio
yote mawili na kufungwa mtini akiwa bado hai lakini amepoteza fahamu. Hali ya
taharuki inazidi kulikumba eneo la chuo. Wanafunzi wengine wanaamua kurudi
kwenye vyumba vyao (hosteli) hawana hamu ya kuingia madarasani. Wenye kiu ya
elimu wanaendelea na masomo, wenye roho ngumu wanaingia madarasani lakini kwa
tahadhari na woga ukitanda mioyoni mwao.
Chuo
kikuu cha Mtakatifu Augustino kimekua kikikumbwa na mikasa ya kustaajabisha.
Wanachuo wanateswa, wengine kuuwawa wengine wanapotea bila kuonekana. Wahadhiri
nao wamo lakini si wengi kama wanachuo. Isitoshe matukio mengi yanalikumba
darasa (kozi) moja. Japokuwa kozi nyingine zinahusika lakini kozi moja inakuwa
na matukio mengi zaidi. Chanzo cha matukio yote hakikua kikieleweka.
Haijulikani kama ni kikundi cha watu fulani au mtu mmoja wengi wanabaki kizani.
XXXXXX
Nje
ya darasa wanachuo wa kozi ya uandishi wa habari na mawasiliano ya umma
(Bachelor of Arts in Mass Communications) wengi hufupisha na kuita BAMC walikua
wamekusanyika vikundi vikundi baada ya Mkufunzi kuaihirisha kipindi. Katika
kikundi kimojawapo kilichoongozwa na kiongozi wa zamani wa darasa hili aitwae
Kaida Bakari na kiongozi wa sasa wa darasa kwa vyuoni hufupishwa na husemwa CR
(Class Representative). CR wa sasa wa kiume alikua Zawadi Chama.
“mimi kuna mida nafkiria niombe
likizo ya dharura maana hali inatisha maze” Alisema Zawadi.
“we kama msomi kukimbia tatizo sio
solution tafuta njia ya kutatua tatizo” Kaida akamjibu.
“Acheni ujinga hii sio ishu ya
kuchezea watu na akili zao wanachemka, hii ishu hakuna cha usomi wala nini”
Rwachi mwenye maneno mengi aliongeza
“Mwenzenu usiku sitoki kabisa
rum(Chumbani) hata vipindi vya asubuh kuja mwenyewe sithubutu” Gloria
alichangia.
“jamani sasa tutafanyaje, tukimbie
chuo?” Baraka aliuliza.
“mimi ndio mnazidi kunichanganya”
Alisema clara.
Majadiliano
na mabishano yaliendelea kwenye vikundi vikundi hivi. Wengne hawakua na la
kusema walikaa kwenye viti vya kusomea na kutafakari kimya kimya. Hakuna
aliyekua na amani. Kila mtu alikua na woga kwa hali inayoendelea.
Kipindi
kilichofuata muda wake uliwadia na hivyo
waliingia darasani na mkufunzi aliingia. Ni kipindi cha uandishi na matumizi ya
kamera (Photo Journalism). Mkufunzi huyu alikua mwembamba na mfupi kwa jina ni
Proches Rugabwa. Wengi walimchukia kwa sababu ya kazi nyingi za darasani
alizozitoa na hata ukifanya kwa ufanisi kiasi gani ni vigumu kupata maksi za
juu. Ingawa somo alilofundisha lilikua si gumu lakini waliofaulu ni wachache.
Wanachuo wengi husema ukimzoea mkufunzi huyu somo lake utafeli.
Kwa
siku ya leo ilikua ni siku ya kuwasilisha (Presentation) kwa kawaida mkufunzi
alitoa kazi wiki mbili kabla wanachuo hufanya kwa vikundi halafu huja
kuwasilisha darasani kwa wenzao, yaani kuwafundisha kile walichofanya. Vikundi
vingi vilikua havijajiandaa kikamilifu hivyo uwasilishwaji ulikua ni kwa
kiwango cha chini. Vikundi vilikuwa na watu si chini ya kumi na tano. Vikundi
viliwasilisha kutegemea na jinsi walivyojiandaa na kutegemea na uwezo binafsi
wa wanachuo wenyewe.
Ilikua
ni zamu ya kikundi cha kumi na tatu kuwasilisha kazi yao. Kikundi hiki
kilishangaza kidogo sababu kilikua na watu wachache, badala ya kuwa na watu
kumi na tano kilikua na watu wanne tu. Walikua wavulana wawili na wasichana
wawili. Wakiwa mbele ya darasa wanadarasa wengine walicheka wengine
wakawahurumia.
“Where are the others?”(“wenzenu wako
wapi?”). hakuna aliyejibu wote walibabaika kwa sababu hawakua na taarifa yoyote
na wenzao.
“Anyway, may you Proceed.”(Mnaweza
kuendelea). Walianza kubabaika na kuangaliana. Hawakua na budi kufanya hivyo.
Katika vikundi vingi wengi wanaotegemewa ni wale wenye akili, ujasiri wa
kuongea, ujasiri wa kuwasilisha mbele za watu na katika kikundi hiki namba kumi
na tatu hawa watu hawakuepo. Kwa lugha ya vijana husema “majembe” hayapo.
Jeni
Ngete alijitutumua na kuanza kuwasilisha, akawasilisha kwa kubabaika lakini alijitahidi sana. Akachukua Benjamin
Lemnat akatumia dakika moja akamwachia Doris mwanjale. Riziki Tagea alikua
amejitenga mbali kama sio mmojawapo wa kikundi. Ilipowadia zamu yake alijifanya
amezama kwenye tafakari. Darasa likacheka. Riziki akashtuka.
“Bwana mdogo vipi” Mkufunzi Proches
Rugabwa akamsaili.
“Nilikua napanga pointi” Akajibu na
darasa likacheka tena
Mhadhiri, “endelea tunakuskiliza”
Riziki
akawasilisha lakini utulivu ukaondoka darasani. Ni kama alikua anachekesha darasa.
Aliendelea kuwasilisha vitu visivyoeleweka.
Mhadhiri Rugabwa akamkatisha
akamwambia;
“Kati ya maboga wewe ni boga ambalo
haliivi, yaani kichwa boga umekuja chuoni kujaza nafasi. Chuoni wanakuja wenye
akili sio boga kama wewe” Wanadarasa hawakupendezwa na maneno ya mhadhiri,
huyu. Wanajua ni ugumu kiasi gani wa kuwasilisha mbele ya darasa, kuna wengine
walikwepa hata kuja darasani kuhofia hii kazi ngumu.
Wengi
walitarajia Riziki angejiskia vibaya na roho ingemsuta, ajabu alimtazama
mkufunzi Rugabwa kisha akaangua kicheko cha nguvu.
“Yani unatudhihirishia ulivyo boga”
Rugabwa akanena. Riziki alimtazama akacheka tena.
“Nyie wenzake hebu lisaidieni hili
boga” Rugabwa akaongea kwa hasira kiasi. Benjamini akaendelea kuwasilisha mpaka
mwisho. Ikafika muda wa maswali ambayo yalitakiwa kujibiwa na kikundi
kilichowasilisha kazi. Ni utaratibu kila baada ya kikundi kumaliza kuwasilisha
kazi maswali huulizwa na wanadarasa.
Gloria
Ndeema akanyoosha mkono na mhadhiri akamruhusu kuuliza.
“I have a question and I need Riziki
to answ……..” (Nina swali na nataka Riziki aji…….)
Riziki akamkatisha “ask us as a group
not a single person” ( tuulize kama kikundi sio mtu binafsi
Mhadhiri akaingilia “You are among of
the group, don’t regard” (Usijali na wewe ni mmoja wa kikundi) Riziki
akamtazama Mhadhiri Rugabwa na Gloria kisha akacheka. Darasa likastaajabu.
Gloria akauliza swali, hakika lilikua swali gumu sana kwa riziki akafikiri
akakosa jibu akaomba mwingine amsaidie.
“I asked you Riziki to answer”(
nilisema Riziki ndio ujibu) Gloria akasisitiza. Riziki akatazama chini kisha
akainua uso wake akamtazama sana Gloria kisha akacheka. Kisha akageuka
kumtazama mhadhiri akacheka pia. Darasa likafurahi. Wenzake wakamsaidia kujibu.
Mwisho wa kipindi ukafika, wakatawanyika kujiandaa na vipindi vingine.
XXXXXX
Ni asubuhi nyingine ndani ya chuo
kikuu St Augustine jijini Mwanza habari zinasambaa chini chini juu ya mwanachuo
kujinyonga. Ni habari iliyoanza kuvuma taratibu nyakati za asubuhi na kuenea
kwenye masikio ya wanachuo wengi chuoni hapa. Ni minong’ono iliyokua inaendelea
kuzagaa lakini bila uthibitisho. Ni mwanafunzi wa kozi ya Mawasiliano ya umma
(BAMC).
Kipindi
cha somo la uandishi wa kitangazaji (Writing for broadcasting) kilikua
kinaendelea katika darasa lililohudhuriwa na wanachuo wa kozi husika. Karibu
wanakozi wote walihudhuria kipindi lakini kuna baadhi ya wenzao hawakuepo. Hii
ilizidisha wasiwasi katika darasa hili lakini bado hakuna aliyekua na hakika na
habari iliyokua inazagaa asubuhi hii. Mkufunzi Madam Herrieth alikua anaendelea
kutoa mafunzo lakini wanakozi wengi walikua mbali. Mawazo yalikua mbali
kufikiri taarifa zinazozagaa kuhusu mwenzao. Wenye namba za anaedaiwa
“kufariki” walijaribu kumtafuta bila mafanikio. Simu yake iliita bila
kupatikana. Meseji nazo zilitumwa pasipo kujibiwa!
Ilikuwa ni wasiwasi!
Madam
Herrieth akiwa anaendelea kutoa mawaidha mara mwalimu mlezi wa darasa na mkuu
wa idara ya mawasiliano ya umma Madam Peace Wedu aliingia katika darasa hili.
Aliingia kupitia mlango wa mbele ya ukumbi huu wa darasa na kumkabili moja kwa
moja Madam Herrieth kisha wakateta jambo Fulani. Wanakozi walimtazama kwa
makini wakijaribu kusoma jambo Fulani bila mafanikio. Kisha Madam Wedu
akasimama mbele ya darasa akatazama darasa zima. Usoni alionekana dhahiri ana huzuni.
Kuna jambo limemsibu!
Tena si jambo dogo!
“Habarini za asubuhi?” Madam Wedu
alisaili.
Wanakozi wakajibu “Nzuri shikamoo
Madam”
“Marahaba” Madam akaitika kisha
akasita kidogo. Alipoipata vyema kauli yake akaendelea.
“Sijui nianzie wapi lakini nimepokea
taarifa ambayo si nzuri, ni habari ya kusikitisha na imenitia majonzi” Akasita
kidogo. Darasa likatulia likaweka umakini wote kumsikiliza. Akaendelea;
“Nimepata taarifa mwanachuo mwenzenu,
ameaga dunia” Darasa likataharuki, wenye
mioyo isiyo na uvumilivu machozi yakaanza kutiririka. Madam akaendelea;
“Ni mwanafunzi mwenzetu, dada yetu
wote tulimpenda sana lakini kilichotokea hatuna jinsi. Amekutwa amejinyonga
chumbani kwake. Ni mwenzetu nadhani wote tunamfahamu GLORIA NDEEM……………?
Lahaula!!! Kabla madam hajamaliza darasa lililipuka kwa kilio kikubwa. Wenye
ujasiri walibaki kupigwa na butwaa. Darasa likaangua kilio. Wanachuo wa kozi
nyingine waliokuwa nje waliingia katika darasa hili kujua kulikoni. Madam
hakuweza kuendelea kuelezea na aliyekua anafundisha hakuendelea kufundisha.
Hakukua na namna ya kipindi kuendelea. Kunguru mwoga hukimbiza mbawa zake.
Wenye mioyo laini walikwishafika kwenye vyumba vyao wakilia.
XXX
Gloria
Ndeema alikua ni mwanachuo wa mwaka wa kwanza katika chuo cha Mt Augustino
(SAUT) tawi la Mwanza. Ni miongoni mwa wanakozi wanaosomea shahada ya
mawasiliano ya umma (BAMC). Alipendwa sana na wahadhiri wengi kwa sababu alikua
miongoni mwa wanafunzi wenye upeo na wadadisi sana. Akiwa darasani asipoelewa
aliuliza sana maswali. Daima alipenda kukaa nafasi za mbele na kamwe humkuti
nafasi za nyuma. Ilifika mazoea hadi akichelewa kidogo aliachiwa nafasi katika
viti vya mbele. Kwenye kuwasilisha kazi za vikundi alikua machachari na
anayejiamini hivyo alipendwa na wakufunzi wengi. Pia wakati wenzake
wanawasilisha kazi zao mbele ya darasa aliwasikiliza kwa makini na kuuliza
maswali. Wanachuo wenzake wengi walimhofia wakati wa maswali na wengine walimchukia
kwa maswali yake. Japo si sahihi lakini penye wengi pana mengi.
Ni
asubuhi mwenzake aliesoma kozi tofauti alipompitia waende chuoni pamoja kwakua
walikua na vipindi vya asubuhi wote. Gloria aliishi maeneo ya Sweya karibu na
chuo na aliishi chumba cha peke yake kwene jumba hili lililokua na vyumba vingi
ambavyo vilikodishwa kwa wanachuo. Aisha Aboubakar alimgongea Gloria lakini hakufungua!
Hakuitika!
Haikua mazoea yake!
Aisha
aliwaza huenda amekwisha kutangulia chuo lakini nafsi ilikataa sababu jana
alimwambia asubuhi ampitie, pia simu akipiga inaita ndani ya chumba na vile
vile ni mapema sana hawezi kuwahi chuo hivyo. Aisha alisubiri pale nje,
alitamani kugonga vyumba vya wanachuo walioishi jirani aulize lakini aliachana
na wazo hilo aliona ni usumbufu kuwapa bugudha wengine asubuhi hivyo kwa kuwa
wengi hawapendi kusumbuliwa asubuhi. Usingizi wa asubuhi mtamu sana. Akiwa
katika kufikiri hili na lile alisogea lilipo dirisha la chumba anacholala
Gloria kama atawezakuona ndani. Aliufuata upenyo uliionekana katika dirisha
kisha akasogea kupenyeza jicho. Alitazama na kuweza kuona sehemu ya kitanda.
Ilikua tupu!
Kitandani Gloria hakuwepo!
Aliwaza huenda alikua bafuni lakini
hakukumbuka kusikia mtiririko wa maji. Au chooni lakini mbona katumia muda sana
kuita na kugonga bila kuitikiwa? Aliendelea kusogeza jicho lake kupenya pembe
mbalimbali za chumba. Mara aliona miguu ya mtu ikining’inia hewani. Aisha
akapatwa hofu akainama chini kisha akapandisha jicho juu zaidi ili aweze kuona
mtu aliyening’inia anafanya nini.
Maaamaaaaaaaaaaaaaaaaaa………………Lilimtoka
yowe kubwa kisha akaanguka na kuzirai. Vyumba vya jirani wanachuo walishtushwa
na ukulele ule. Walitoka nje haraka wengine hawakua wamejiandaa walikua wamevaa
hovyo baada ya mkurupusho wa ukulele ule. Walimkuta Aisha amezimia chini ya
dirisha hakuna aliyeelewa nini kimemzimisha na sababu ya kelele ile. Wengine
walimpepea, wakambeba kumwingiza ndani kumpatia huduma.
Mmoja aliamua kuchungulia kwenye lile
dirisha!
Mtumeee!!!!!!!!! Alitokwa na yowe
dogo la woga.
Wenzake walikuja pale dirishani
wakasukumana kuchungulia ndani. Asalaaalee!!! Ni mwili wa Gloria ulikua
unaning’inia bila uhai. Wengi wakaingia katika hali ya taharuki, wengine
waliokua wakicheka nae jana walibaki kustaajabu zaidi. Gloria hakua na huzuni
au kitu kilichomwonesha yupo katika hali yoyote ya huzuni au hasira iweje
ajiue. Wenye mchecheto walianza kufahamishana kwa simu. Watu walianza kujaa. Mwenye
busara aliinua simu yake na kutoa taarifa polisi.
Muda
mfupi baadae polisi waliwasili na gari lao eneo la tukio. Walifanya mahojiano
kidogo na wenyeji kisha mmojawao akajaribu kufungua mlango. Mlango ulikua
umefungwa vyema kwa ndani na walipochungulia funguo zilionekana. Hakukua na
njia ya ziada ilibidi mlango uvunjwe. Kabla ya maiti kushushwa kwenye kitanzi
uliponing’inia askari walikagua chumba kwa makini. Mezani kilionekana kipande
cha karatasi kimeshikiliwa vyema na kalamu kikiwa na maandishi machache.
Kiongozi wa msafara wa askari hawa alikiokota akakisoma, kiliandikwa hivi;
MAPENZI NI SUMU MBAYA TENA MBAYA
SANA. SIKUTEGEMEA KAMA UTAKUJA KUNISALITI. NILIKUAMINI SANA NA KUKUDHIHIRISHIA
KAMA NAKUPENDA NATANGULIA NIKATOE MASHTAKA YANGU HUKO. KWAHERI.
Askari
alipomaliza kukisoma aliwapa wenzake nao wakasoma.
“dada mzima na akili zake anajiua
kisa mapenzi huu si ulimbukeni”? Askari mmoja akaropoka.
“yanasoma lakini hayaelimiki, jamani
hapa tusipoteze muda tumjue kwanza huyo mwanaume wake twende nae” Mwingne
akachangia. Mwili wa Gloria ukashushwa ukaingizwa ndani ya gari la polisi
likatimua vumbi kuondoka eneo lile.
XXXXXX
Kituo
kidogo cha polisi Nyegezi, Kelvin Tibaaccra alikua katika mahojiano maalum. Ni
muda kidogo umepita tangu akamatwe kwa tuhuma za kusababisha kifo cha mpenzi
wake Gloria aliyefariki baada ya kujinyonga. Kelvin alipatwa na kigugumizi
hakuweza kuongea. Tangu apate taarifa za kifo cha mpenzi wake akili zilimruka
na hata askari walipokuja kumtafuta walimkuta chumbani kwake hajielewi. Kelvin
alikumbuka majira ya jioni siku iliyopita ndipo aliongea na Gloria
hawakugombana waliagana kwa furaha.
Tangu
waingie kwenye uhusiano Kelvin na Gloria walipendana sana. Hakuwai kumsaliti na
wote waliaminiana. Ingawa waliwai kukwaruzana siku za nyuma lakini ilikua ni
hali ya kawaida kabisa na walimaliza wakaelewana maisha yakaendelea. Hakuwai
kumsaliti kabisa na hakuwai kujihusisha na msichana mwingne tofauti. Pia
hajawai kugombana na Gloria siku za karibuni bali walikua na maelewano mazuri
sana. Sasa iweje Gloria ajinyonge tena kwa ajili yake. Aliwaza labda Gloria
alikua na mtu tofauti na yeye na ndie aliemsaliti. Haikumwingia akilini eti
Gloria alijiua kwa sababu yeye alimsaliti.
“Haiwezekaniiiiiiiiiii………..”
Alipayuka kwa nguvu.
XXX
Majira
ya saa 9:45 alasiri wanakozi wa BAMC walikua darasani wakiendelea na kipindi
cha uchumi (Economics). Ingawa walikua na msiba wa kuondokewa na mwanadarasa
mwenzao ratiba ya chuo ilibidi iendelee. Ratiba ya chuo hupangwa mwanzoni
kabisa mwa muhula na hupangwa ratiba ya nusu mhula na masomo yote hupangwa
idadi sawa ya vipindi hivyo ni lazima izingatiwe bila kujali nini kitatokea
mbele. Darasa lilikua nusu wengi walishindwa kuja darasani na waliokuemo
walipunguza ufanisi wa kusikiliza kwa mawazo ya msiba wa mwenzao. Mhadhiri Dk
Zakulala alikua mbele ya darasa akifundisha somo la uchumi.
Mara
aliingia mwanazuoni ambae si muhusika wa darasa akanong’ona kidogo na mhadhiri
Dk Zakulala kisha akatoka nje.
“CR ukaonane na mwalimu mlezi wa
darasa mara moja” Aliongea Dk Zakulala kisha akaendelea na kipindi. Somo la
uchumi ni moja ya masomo magumu kidogo hasa kwa kozi za sanaa sababu inahusisha
mambo ya biashara na hesabu hivyo inampasa msomaji awe na msingi kidogo wa
hesabu.
Riziki
Tagea nae alikua darasani akamnong’oneza mwenzake.
“Hizi equilibrium zake ngumu kweli,
hili somo nisiposupp nachinja kakondoo” Tagea alinong’ona kwa sauti ya chini.
“Tulia dogo udongo uwahi ungali maji
ukikubali likushinde utajibeba” alijibu wa pembeni Aron Mkombe.
Dr
Zakulala aliendelea kufundisha na mara CR akarudi kisha akamjongelea mhadhiri
na kumnong’oneza jambo kisha kwa ishara akamruhusu kama kuteta jambo Fulani.
Akakohoa kidogo kisha akasema;
“Jamani
nimeitwa na madam mlezi wa darasa madam Wedu namenituma nije niwape taarifa
mwalimu wa Photo Journalism mr Rugabwa amepata ajali mbaya amelazwa Bugando”
alisema CR
“Oooooh……….mama yangu………..eeeeeehhh”
wanachuo waligwaya, majadiliano ya sauti kubwa yakaendelea. Mhadhiri aliwasihi
watulie waendelee na kipindi lakini hakuna aliyemsikiliza ni kama alikua
anapiga ngoma ya bugudha.
XXXXXXX
“Afande
tangu niingie kwenye mahusiano na Gloria sijawahi kumdanganya wala sijawahi
kuwa na mwingine tofauti na yeye” Kelvin alijibu
“kijana mbona ameacha ujumbe ambao
unakutaja wewe” askari akaongeza swali
“afande kwa kweli inaniwia vigumu
sana hata jana tumeagana vizuri tu na hatujawai kuwa na ugomvi wowote siku za
karibuni nipo gizani afande sielewi chochote” Kelvin aliendelea kujibu kwa
msisitizo.
Baada
ya kuhojiwa vya kutosha na uchunguzi uliofanywa kwenye simu ya Kelvin na ya
marehemu Gloria na pia uchunguzi wa watu mbali mbali Kelvin aliachiwa na kupewa
miadi ya kuripoti mara kwa mara kituoni kuendelea na uchunguzi.
Mwili
wa marehemu Gloria ulisafirishwa kwa maziko nyumbani kwao mkoani kagera baada
ya michango kutoka kwa wanachuo na familia iliyokuja kuratibu mpangilio wa
kuusafirisha mwili.
XXXXXXX
Riziki
Tagea alikua amejipumzisha kwenye bustani za chuo mkononi akiwa na kijitabu
kidogo na spika ndogo za masikioni zikiwa zimechomekwa vyema kwenye simu yake
aina ya TECNO aliburudika vyema na mziki mwororo uliokua unamliwaza. Kwa umbo
ni mwembamba mrefu si mrefu na mfupi si mfupi. Sura ya maji ya kunde mara
nyingi hupendelea suruali za jinsi na mashati ya kisasa. Popote atembeapo
Riziki huwa na spika za masikioni akisikiliza mziki. Ni miongoni mwa wanafunzi
wa BAMC na mara nyingi hupenda kutembea na gari ndogo ya aina ya Corolla ya
kizamani. Ni miongoni mwa wanachuo wachache wanaokuja chuoni na magari binafsi
kwani wengi hupanda dala dala.
Akiwa
amejipumzisha bustanini jua lilikikimbiza kivuli kilichomkinga na kupenya moja
kwa moja kwenye ngozi yake. Alivuka kiuzio kilichokuepo na kuingia ndani zaidi
ya kibustani. Mara alikuja mlinzi akamkemea kwa kuharibu bustani. Mlinzi alikua
nyuma ya Riziki akiongea kwa ghadhabu na wakati huo Riziki alitingisha kichwa
kufuatia mapigo ya mziki uliovuma masikioni mwake. Mlinzi kwa ghadhabu
alimwinamia na kumtandika kofi kali. Kwa mshtuko Riziki aligeuza shingo na
kushikilia shavu kwa kofi lililotua shavuni mwake.
“Nakusemesha una dharau sio wote
wakudharaulika dogo hata kama ni mlinzi niheshimu elimu yako isikufanye
unidharau” alibwata mlinzi. Loooh! Hakujua kama Riziki hakua anamsikia kutokana
na mziki mkubwa uliokua unavuma masikioni mwake. Wanachuo watatu waliokua
jirani wakijadili hili na lile walishuhudia tukio lile. Wakati Riziki anapokea
kibao waliangua kicheko cha nguvu Riziki akawageukia kwa ghadhabu.
Nae akacheka!!
Kisha akamgeukia mlinzi.
Riziki akacheka tena!! Mlinzi alighadhibika
zaidi baada ya mwanachuo huyu aliyeonekana ana dharau kumcheka akamzabua kibao
kingine cha nguvu.
Riziki akamtazama kisha akacheka!!
Wanachuo watatu waliokua karibu
walivunjika mbavu kwa kucheka, walicheka sana, hakika lilikua tukio la
kushangaza. Riziki akanyanyuka akawafuata pale walipo, walikua ni wasichana
wawili na wa kiume mmoja. Alipowafikia aliketi kama kujiunga nao akawatazama
kisha akacheka!!
“Mnajua nilikua nacheka nini” Riziki
akahoji.
Wakamcheka kisha wakamjibu kwa
pamoja. “unacheka nini”?
Riziki akawatazama kisha akacheka
akawaambia “NIKICHEKA UTALIA, nitawaambia kwenye simu nilichokua nacheka, haya
hebu andikeni namba zenu za simu na majina yenu halafu mtalia,” Riziki akasema
kisha akacheka. Bila hiyana wakaandika namba za simu kwenye kijidaftari cha
Riziki huku wakicheka. Riziki akaondoka zake akiwaacha wakicheka.
ITAENDELEA..................................
Unaweza kutoa maoni pamoja na ushauri katika kuwezesha ubora na mafanikio ya blog hii.
Asante
Post a Comment