NIKICHEKA, UTALIA!!!! SEHEMU YA 02



Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo.   
Simu: 0766054094/0718878887
Kifo cha mlinzi mmojawapo wa chuo kilishuhudiwa na baadhi ya wanachuo na wafanyakazi waliokua wakijishughulisha na shughuli za usafi wa mazingira.
Siku ya jumamosi chuoni hapa ni siku yenye vipindi vichache. Vipindi vingi huwa kati ya jumatatu mpaka ijumaa. Kwa siku kama hii ambayo ni wikiend kuna baadhi ya madarasa huwa na ratiba ya vipindi jumamosi ambavyo mara nyingi si vingi. Wanachuo wengi wanakua chuoni kufanya mazoezi ya makundi hivyo kama katikati ya wiki hawajapata muda hutumia siku ya jumamosi pengine hata jumapili kukamilisha  kazi za darasani.
          Walioshuhudia walishika kichwa, wengine waliduwaa, wengine akili ziliruka kwa muda wengine hata walikimbia wasishuhudie kuona mwili wa huyu binadamu utakua katika hali gani. Madarasa maarufu kwa jina la Mwanjonde. Mwanjonde ni jengo la ghorofa tatu lililopo katika chuo kikuu cha mtakatifu Augustino.
          Baadhi ya wanachuo waliketi chini ya mwembe mkubwa uliotazamana na jengo hili lenye urefu si sana. Walikua wakijadili hili na lile pengine wakivuta muda kusubiri kipindi au aidha wakiwasubiri wenzao kwa kazi za makundi (Discussion). Ni asubuhi majira ya saa mbili hivi wanashuhudia jambo la kushangaza.
Ni jambo lisilotarajiwa!!
          Kilichosikika kelele iliyofuatiwa na kishindo. Wakati ukulele ule unatoka ndio uliowashtua waliozama kwenye stori za hapa na pale na waliokua wanafagia wakashuhudia mwili wa mtu unashuka chini na kutua kwa kichwa.
Loooh, hali ititisha.

          Umbali wa mita kama 12 kutoka ghorofa ya 3 mlinzi huyu alianguka na kutua chini kwa kichwa. Ni ukelele uliosikika na kishindo cha kutua chini, mwili ulipotua chini walishuhudia mtu akijinyoosha labda ndio alikua anaipigania pumzi kwa mara ya mwisho lakini hakuna aliyekua na hakika. Ni kawaida ya watanzania linapotokea tukio la kushtukiza jambo la kwanza ni kuduwaa badala ya kutafuta msaada wa haraka. Wengine wenye nafsi katili walisogea kupiga picha kutumia simu zao. Sijui ni roho mbaya au ukatili eti mtu badala ya kumpa msaada unapiga picha, sielewi picha ndio mwokozi wa uhai au uokozi ni kumsaidia mwathirika. Ndio watanzania walivyo.
          Gari la wagonjwa liliwasili eneo la tukio na kuupakia mwili wa mlinzi moja kwa moja kuwahi hospitalini Bugando. Ukiutazama mwili ulivyo hata kichaa angekiri kuwa hauna uhai lakini ilipaswa ufike hospitali daktari athibitishe.
          Baadae habari zilithibitika mlinzi alikua amefariki. Alifariki kwa kifo kibaya sana. Kifo cha kuanguka ghorofani, tena kifo cha kugundua sekunde chache zijazo utakua marehemu.
          Wikiendi hii ilikua ya kustaajabisha kabisa haikuishia kwa kifo cha mlinzi pekee. Jambo jingine la kushtua lilitokea, hakika kila mwanachuo ilimshtua. Kifo kingine kilitokea.
Kifo cha kushangaza!
Mambo yalitisha!!
Ni hali ya kusisimua!!
          Mwanachuo anaesoma kozi ya sayansi ya jamii (Bachelor of Sociology) wengi huita kwa kifupi BASO. Msichana Mwanaidi Mfinga aliripotiwa kufariki.
Alifariki baada ya kushambuliwa na nyuki!!
Hakika ni jambo la kushangaza, wengi walijiuliza hao nyuki walitoka wapi mpaka wamshambulie mtu apoteze uhai? Alikua anafanya nini mpaka kushambuliwa na hao  nyuki? Hakuna aliyekua na jibu sahihi. Majibu angekua nayo mwathirika mwenyewe ambaye sasa ni marehemu. Alifariki muda mfupi baada ya kukimbizwa hospitali akiwa na hali mbaya. Alikutwa na hali mbaya mwili mzima umevimba na waliobahatika kumuwahi alikua ndio sekunde ya mwisho anapoteza fahamu. Fahamu hazikumrudia angalau aeleza madhila yaliyompata. Alipitiliza katika usingizi uliochukua uhai wake.
                                                XXXXXX
          Riziki Tagea baada ya kuondoka bustanini pale alikwenda moja kwa moja katika kantini moja iliyopo chuoni maarufu kwa jina la Salma Cone kisha akaagiza juisi ya embe. Alikunywa taratibu akiwa anafikiri hili na lile.
“lazima walie” Aliongea kwa  Sauti ndogo. Aliendelea kufikiri, akazama kwenye tafakari ya kina.
“Roho yangu inauma, nafsi inanisuta nimedhalilishwa sana, lakini lazima walie, nani wa kuwasaidia. Ole wenu mnaocheka sasa maana maana baadae mtaomboleza na kulia” alikumbuka maneno ya kitabu cha Biblia injili ya Luka sura ya 6 mstari wa 25. Riziki akatabasamu. Akaingiza mkono mfukoni akachomoa simu yake akaangalia muda ulikaribia wa kipindi, akaamua kujisogeza darasani.
          Ni kati kati ya kipindi mkufunzi wa somo la Filosofia (Philosophy) Madam Kiprop anafundisha na wanakozi wakimsikiliza kwa makini. Hakika somo la leo liliwagusa na liliwaingia kila mmoja alitega sikio kwa makini kumsikiliza.
“Wengi tunajiuliza kuhusu nafsi, nafsi ni kitu gani. Je ni kweli nafsi inahusiana na ubinadamu na utu? Binadamu kaumbwa na vitu vitatu tofauti ndani yake. Kuna roho, moyo na nafsi…… Moyo ni kiungo ambacho kinaweza kuonekana na kushikika lakini kipo ndani, ukijishika upande wa kushoto mwa kifua chako unaskia kinachopiga kila baada ya sekunde kadhaa, hapa naomba tuelewane kinachopiga ni mapigo ya moyo sio roho kama wengine mnavyosema. Roho ni pumzi ya uhai tunaweza kusema ni uhai wenyewe. Na roho haionekani wala haishikiki lakini ni kitu ambacho kipo ndani ya kiumbe chochote chenye uhai. Roho ikikutoka inamaanisha mtu au kiumbe si hai tena. Ni makosa mtu kusema ‘roho inaniuma’. Je kitu ambacho hakionekani wala hakishikiki kinawezaje kuuma? Tukisema nafsi(Conscience) ni kitu ambacho kipo ndani ya mtu lakini hakionekani wala hakishikiki, hakuna tafsiri sahihi ya kwamba nafsi ni kitu gani aidha labda ni ubinadamu au utu.” Madam Kiprop aliendelea kufundisha hakika somo liliwagusa.
Riziki akiwa viti vya katikati alikua katika utulivu wa hali ya juu akisikiliza na kutafakari kwa makini sana huenda kwa makini kuliko wote. Mhadhiri aliendelea kukoleza somo;
“Nafsi inaweza kuwa sauti fulani iliyo ndani ya mtu lakini ni sauti isiyosikika aidha ni ya kuonya, kushawishi au kukemea. Na kitu cha muhimu nafsi na akili vyaweza kuwa vitu tofauti sana. Ngoja niwape mfano mdogo. Kuna mtu anachukizwa au mtu anamuudhi kwa kiwango kikubwa. Kuna kama hali fulani ya kuumiza ambayo ipo ndani ya mtu huyu. Anafikiri kwa makini anaamua kwa aliemfanyia ubaya lazima akamtoe uhai na anaamini dhahiri akimuua ile hali ya kuumizwa lazima itaondoka. Moja kwa moja ubongo unaamua kwenda kuua. Akili imeshafanya maamuzi ya kuua lakini wakati akiwa njiani kwenda kuua anaskia hali fulani ya kumkataza yaani kama sauti fulani inamuonya asifanye anachotaka kufanya, hiyo hali inayomtokea ya kumuonya au kumkataza tunaweza kusema sauti isiyosikika ndiyo nafsi yenyewe. Baada ya nafsi kumuonya ubongo wa huyu mtu unaamua kuahirisha hapo ni maamuzi yamefanyika na kilichoamua sio nafsi bali ni akili”
Uuuuuhhhh………. Riziki alishusha pumzi taratibu Mhadhiri akaendelea.
“Mtazame mtu kama kichaa sio kama hana akili, akili anayo lakini hana nafsi. Kichaa anaweza kufanya maamuzi yoyote, anaweza kuua kujeruhi kupiga na anafanya kwa uamuzi wa akili. Utamwona anatembea lakini ghafla akili inamtuma, yaani ubongo wake unaamua aokote fimbo, au kopo, hapo hapo akaamua kuokota jiwe, ghafla akaanza kukimbia tena anakimbia huku anapiga kelele na tena anakimbia huku akipiga kelele na akiwa anageuka geuka nyuma. Hapa ni ubongo unafanya maamuzi bila nafsi kuwepo. Kama nafsi ingalikuwepo angaliokota fimbo halafu nafsi imwonye acha naye angaliacha.”
Mhadhiri akaendelea “kama nafsi yako itakuonya jambo fulani, yakupasa uifuate sauti inayokuamuru. Ikikwambia nenda kaue yakupasa kufanya hivyo la sivyo baadae kuna itakua inakulaumu kwanini hujafanya hivyo. Simaanishi nawashauri muue hapana, msininukuu vibaya nmesema fuata nafsi yako inavyokushauri kutenda jambo sahihi”
Darasa likacheka.
Riziki akatabasamu!
          “Binadamu anazaliwa na nafsi huru lakini nafsi huweza kubadilishwa, hakuna aliyezaliwa katili, mkorofi, muuaji au namna yoyote mbaya. Binadamu kazaliwa huru kabisa lakini nafsi huweza kubadilishwa na mazingira, ukuaji, watu anaishi nao, mambo anayozoea………..” Mhadhiri aliendelea kuelezea.
          Kipindi kikamalizika  wanachuo wakatawanyika kwenda nyumbani. Riziki akaingia kwenye gari akawasha gari kisha akawasha kiyoyozi ndani ya gari akazama katika dimbwi la tafakari. Kama haitoshi akabetua kidogo kiti cha gari akajilaza kidogo kisha akaendelea kuwaza
          Nafsi imeumbwa na huruma na uzuri wa kutenda yaliyo mazuri, Nafsi imeumbwa kuvipiga vita vilivyo vibaya. Ndio utu. Nafsi ni utu unaomfanya mtu kuitwa binadamu. Ndio, na nafsi imeumbwa kuogopa mabaya. Ni rahisi sana kumchinja kuku na kuku wengine wakishuhudia wala wasione jambo geni na pengine baadae huja kufukua pahali umechinja wakitafuta chochote lakini ni vigumu sana kwa binadamu kumshuhudia binadamu anararuliwa na simba au anachinjwa mbele yake nae abaki katika hali ya kawaida. Ndio, nafsi imeumbwa na huruma sana lakini nafsi hubadilika. Ndio, hubadilika tena inabadilishwa na jambo Dogo sana. Binadamu alieumbwa kuwa na huruma huwa katili kupindukia ni rahis kumchinja mwenzake bila kuhisi chochote. Mwenye nafsi huru hushuhudia baadae utalia sana. Ndio, tena kilio kikuu kumsikitikia ukatili aliotendewa. Ndio, nilizaliwa kwenye shida, dhiki matatizo nafsi imevumilia lakini imefika mwisho, sasa ni kikomo ukisimama nakuua, ukikimbia nakuua, ukikaa chini nakuua, na chochote utakachofanya nakuua. Ndio, nafsi hubadilika. Binadamu huzaliwa mlemavu au na kasoro fulani ni sawa. Lakini kamwe hazaliwi na roho mbaya, ukatili, ukaidi, hasira, ugomvi na matendo mengine yaliyo maovu na yasiovutia. Ndio binadamu huzaliwa na akili huru, ni haki yake mlemavu aliezaliwa nao kumlilia Mungu, ndio kumlilia kwa kilio kikuu na apaze sauti kwa uchungu mwingi, ndio kwa uchungu, tena uchungu na simanzi na masikitiko makuu kumlilia Muumba. Nae mkaidi na mwongo asifanye huu utakua unafiki, ndio, ni unafiki hakuzaliwa na ukaidi wala kiburi wala hasira wala uongo. Kwanini kawa hivi? Swali la msingi sana. Nalo lina majibu. Binadamu kazaliwa na nafsi huru. Ndio, tena huru kabisa. Lakini hubadilishwa, ndio, hubadilishwa na mazingira anayokulia, watu anaoishi nao, mambo yanayomtokea namna anavyolelewa na vitu anavyotamani kuwa navyo, kuviona na kutaka kuvimiliki. Ndio, ukiishi na wazazi walevi ni rahis kuwa mlevi, si ndivyo tunda ni sawa na mti? Ndivyo, nafsi huweza kubadilishwa na jambo au wazo dogo sana, ndio yaweza. Na tena hubadilika kabisa. Ndio na sababu ipo, lazima sababu iwepo, ni lazima. na je itakuaje baada ya nafsi kubadilika? Ndio, itakuwaje? Na je ikibadilika daima? Ooooh nafsi. Nafsi, nafsi, ndio, nafsi yangu mimi, naililia nafsi yangu. Je nafsi yangu, imebadilika imebadilishwa au imebadilisha nafsi ya mtu mwingine. Je kama nafsi yangu imebadilika, imebadilishwa au imebadilisha nafsi ya mtu mwingne nitajuaje na nitafanya nini.? Lakini fuata nafsi itakavyo. Kama kuua nenda kaue ili nafsi iridhike…………
Piiiiiiii………….
Riziki akashtuka!
Akiwa amezama kwenye lindi la mawazo kumbe wakati anajigeuza mguu uligusa kwenye honi ya gari nayo haikufanya ajizi ikatoa sauti ya nguvu. Riziki akageuza gari kisha akatokomea kwa mwendo wa kawaida kuelekea kunako makazi yake.
Itaendelea...............................................

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2