SIMULIZI-NIKICHEKA, UTALIA!!! SEHEMU YA 03



Mtunzi::Eligi Gasto Tarimo.   
Simu: 0766054094/0718878887
Ijumaa  hii tulivu iliyoanza kwa kijua murua cha kuvutia, majira ya saa 2 na nusu au zaidi asubuhi wanachuo wa kozi ya BAMC walikua darasani wakifuatilia kwa makini somo la uhariri wa habari
( News editing) Profesa Mfumbuka alikua darasani akiwa na msaidizi wake Shawo. Darasa lilikua limejaa  inaonekana wanakozi wote walikuemo lakini Riziki hakuwepo. Kwa vyuo vingi mtu huweza kukosa vipindi bila kufuatiliwa lakini atajua namna ya kuongeza akili kwani somo likishafundishwa halirudiwi, au mhadhiri akitoa swali la ghafla kwa darasa zima akatoa maksi za bure zikipita hazirudi.
          Mwalimu mlezi wa darasa Madam Wedu aliingia na kijana mtanashati kisha akamsogelea profesa Mfumbuka wakateta jambo kwa sekunde kadhaa kisha Madam Wedu akasimama katikati ya darasa akasaili.
“Poleni na masomo”
“Asante Madam” Wakajibu kwa pamoja.
“Nisiwapotezee muda sana, aliye mbele yenu ni mwanachuo mwenzenu amebadilisha kozi katokea ualimu ameamua kujiunga na BAMC, anaitwa Jovin Odelo naomba mumpe ushirikiano”
Wote wakapiga makofi, Jovin Odelo akaangalia nafasi na kuketi, madam akaondoka kipindi kikaendelea.

                                                     XXXXXXXX
          Chini ya kivuli cha mti waliketi wanachuo wa kozi tofauti wakipiga soga za hapa na pale kusubiri muda wa kuingia darasani.
“Tunasoma historia wazee wetu waliishi miaka mingi sana, ukisoma mtu aliishi miaka 300 unashangaa kwanza unahisi ni uongo kwa sasa kufikisha miaka 50 kazi ipo…….. Lakini ebu tafakari kila unachotumia ni hatari kwa maisha yako. Nguo zmetengenezwa vipi?.......Wazee wetu wa kale walivaa ngozi, wazee walikunywa maji asili ya mtoni chemichemi, vyakula tunavyokula na viungo vyake vingine vimekaa kwene majokofu mwaka mzima….. chukulia mfano maziwa ya asili hayawezi kukaa wiki nzima bila kuharibika ona maziwa ya pakti…….., wakati wazee walichoma nyama waliowinda walichemsha nafaka walizovuna bila kutumia kiungo chochote……..,
umeganda na simu yenye mionzi mikali wakati ule hazikuepo. Mwili wako unajipaka mafuta, pafyumu, losheni hujui vimetengenezwaje wakati wazee wetu hawakutumia, unakaa ofisini unavuta hewa ya bandia ya kiyoyozi, unapanda gari, meli, ndege hatari ya ajali muda wowote, vinywaji unavyokunywa wiski, bia, juisi, soda lakini wazee walikunywa togwa na vingine vilivyotengenezwa kias………Wakati anaendelea kuongea alikatishwa ghafla na mwanadada aliyepokea meseji ya kushtua;
“Jamani ee nmetumiwa meseji hapa na mtu wa BASO ananiambia kuna dada anasoma BASO amefariki”
Eeeh!!!!
Unasemaaaaa…!!!
Ni kweli au unatania?....
Acha basi kuturusha roho.
“Jamani meseji hii hapa anasema alikua rum kwake na mwenzie wa kiume sjui kama ni boyfriend wake akazimia ghafla kumpeleka hospitali wanasema alikua ashakufa.
Siku inapoanza japo ni mpya bado mwendelezo wa yaliyopita hii ikiwa na maana kuwa siku zilikuepo sio zinaanza leo. Upya wa siku hutegemea na namna ya kukabiliana na majukumu yako ya siku, panga ratiba zako vizuri kukamilisha majukumu vizuri, ratiba utakayoandaa usitarajie itaenda km ulivyopanga elewa kuna mambo hujitokeza katikati ambayo hukutarajia. jiandae kukabiliana na lolote litakalojitokeza.
                                                    XXXXXXXXXX
          Kuna msemo usemao pema usijapo pema ukipema si pema tena. Haijapita wiki tangu mlinzi wa chuoni SAUT kufariki kwa kudondoka ghorofani. Kesho yake mwanachuo mwingine anapoteza maisha baada ya kushambuliwa na nyuki. Leo linakuja tukio jingine la mwanachuo mwingine anazimia chumbani kupelekwa hospitali anakutwa ameshafariki. Matukio ya vifo tofauti tofauti yanakikumba chuo cha mtakatifu Augustino.
Ni ndani ya miezi isiyozidi mitatu vimetokea vifo mbali mbali. Ingekua vya risasi au kuvamiwa na majambazi angalau mtu angesema kuna kikundi kinachohusika. Watu wanapotea, vifo vinaandamana.
Hali ilitisha!
Kufa kwa wengi harusi! Ni methali ya kale lakini ifikirie kwa undani. Harusi ni tukio la sherehe la kufurahisha lakini kifo ni tukio la kuogofya. Sio kweli kwamba vikitokea vifo vingi watu husherehekea. Laaa. Hali huwafanya watu kuwa na woga zaidi. Ni lazima kufa lakini kifo kinaogopesha.
          Chuoni wengine walisema kuna mzimu ambao unasababisha hivi vifo wengine wakasema ni majini, wenye busara wakasema kufa ni kawaida kila mtu lazima afe hata vinapotokea vifo ni mipango ya Mungu tu.
          Kumbuka duniani tunaishi kwa kupokezana, leo unaishi lakini kesho utakufa atazaliwa mwingine ataishi atakufa, hii ikiwa na maana duniani tunaishi kwetu lakini dunia sio yetu, inaweza kufanana na kuishi kwenye chumba chako cha kupanga lakini si nyumba yako. Hivyo kuna muda wako wa kupita na wenzio kuja baada yako hata uinunue Tanzania yote ni sawa, itakua yako lakini bado ukweli utabaki pale pale duniani sio kwako na utakufa na kuiacha Tanzania ikibaki duniani. Hebu tujifunze kila kilicho duniani sio chetu tunatumia kwa muda tu, leo ukila samaki mzima ukammaliza ukasema umefaidi jua samaki hawajaisha duniani wapo tena wazuri na watamu zaidi ya uliekula. usiing'ang'anie dunia km yako kumbuka nawe utapita na wengne watajimilikisha vilivyokuwa vyako.
                                                    XXXXXXXX
          Bertha Mwakanjia aliamka ijumaa hii akiwa hana hili wala lile. Alianza kufanya usafi wa chumba chake taratibu kwani ni siku ya jana tu alirejea kutoka msibani Tabora kwa mazishi ya rafiki yake kipenzi Mwanaidi Mfinga.
          Inaumiza sana kufiwa na mtu uliyempenda au mtu aliyewahi kukufanya ucheke ama kujifunza kitu. Lakini hiyo haitufanyi tusahau kuwa wote tutakufa. Muda wetu katika dunia hii una kikomo, na huwa kifo ni mshangao kwetu hasa afapo mtu ambaye hatukutegemea. Ni kama kupanda ngazi usiku wa giza nene, ufikapo sehemu na kudhani kuwa kuna ngazi nyingine mbele lakini unashangazwa na kujikuta ukitembea hewani na kuanguka, giza litakufumba macho. kila muda ni muda wa kujiweka sawa kwa muumba. tafuta kitu cha kuifanya jamii yako ikukumbuke, tafuta kitu cha kumfanya muumba wako ajisikie faraja kukupokea.
Bertha na Mwanaidi waliishi chumba kimoja na pia walisoma kozi moja ya BASO (Bachelor of Sociology). Alipomaliza alijilaza kidogo kitandani akifikiri afanye lipi na mara simu yake ya rununu ilianza kuimba kwa mlio mdogo ulioongezeka. Aliitazama namba ngeni asiyoifahamu kisha akaamua kuipokea.
“Haloo”
“Mambo” upande wa pili sauti ya kiume ikakoroma
Bertha “poa, nani mwenzangu maana namba ni mpya”
“ha haaaaaa haaaaaa NIKICHEKA UTALIAAAA” Upande wa pili ukaongea.
Bertha akastaajabu kidogo lakini akakumbuka kitu, kisha akacheka halafu akajibu kwa manjonjo;
“Mwone kwanza, halafu mpaka leo hujatujibu, ulituchekesha sana ile siku,”
“Nilikuahidi nitakwambia, hebu niambie kwanza ratiba yako ya leo nataka nikutembelee utakua na nafasi muda gani?” Sauti ikakoroma kwenye simu.
“Leo nipo muda wote sitoki, njoo tu unichekeshe tena” Bertha akaongea.
“Ilo dogo mwenda bure si sawa na mkaa bure bana huenda akaokota nyumba” Upande wa pili ukaongea.
Bertha akacheka sana “Inaonekana asili yako vituko, haya niambie…”
“Nitakuja kukwambia huko huko, nielekeze unapoishi na juisi unayopendelea nakuja kwenye saa saba mchana” Sauti ikajibu.
“Yaani juice ya embe ya kampuni ya Azam ndio mpango mzima nikinywa hadi nalala, njoo Hostel za kwa Mashau room namba 12” Bertha akaelekeza.
“Wooouu! Hamna mchecheto mengine uko uko” Sauti iliongea na kukata simu. Bertha alifanya maandalizi ya hapa na pale kisha akafanya utaratibu wa kupata kifungua kinywa kumsubiri mgeni huyu mwenye vijimambo.
          Baada ya kifungua kinywa Bertha alijilaza akifikiri hili na lile. Aliwasha komputa mpakato kisha akaunganisha na mfumo wa mziki uliokua chumbani akaweka nyimbo za dini kwa sauti ya chini iliyoishia ndani ya chumba kisha akarudi kujilaza katika kitanda chake akiwaza na kuwazua. Akakumbuka busara za mwandishi wa riwaya fulani aliyeandika;
‘“Usidhani yanayokutokea sasa, au yale uliyopitia ndiyo yatakayoonyesha wewe utakuwa mtu wa aina gani hapo baadaye. Haijalishi umetoka kwenye familia ya aina gani na wala haijalishi maisha yako ya sasa yakoje. Lakini uamuzi wako utakaoufanya sasa juu ya nini unataka kukitilia mkazo na nini maana ya vitu fulani kwako, aina ya mafanikio uyatakayo na jinsi ambavyo utafanya ili kuyafikia ndicho kitakachokupa mwanga wa mtu wa aina gani utakuwa. Kila kitu duniani chenye mafanikio kilianzishwa na mtu mmoja tu. Wazo huwa kichwani kwa mtu mmoja nayeye anaposhirikisha wengine bado tunahesabu kuwa yeye ndiye aliyeleta jambo hilo. Kila mtu mwenye mafanikio alikuwa na ndoto kabla, akazichambua ndoto zake na kuziishi huku akifanya kila njia kuzileta kwenye uhalisia. wewe una nafasi ya kufika pale utakapo kama utaacha kujidharau.”
“Aaagh, ila ni kweli kama mtu………..” akiwa katika kuwaza alikatizwa na mlio wa mlango uliokua ukigongwa taratibu. Akausogelea mlango na kuufungua.
          Udugu wa nazi hukutania chunguni. Bertha aliikumbuka hii sura, mara ya mwisho kuiona ni pale katika bustani ikipokea kibao murua kutoka kwa mlinzi. Mshtuko wa kile kibao ulifuatishwa na mshtuko na kugeuka kwa kasi halafu badala ya kukasirika, baada ya kibao au kuuliza kilichosababisha kibao, sura ilibadilika na kicheko kikamtoka mtu huyu, baada ya mlinzi kukasirishwa na kitendo cha mwenye hii sura kumcheka aliongea tena kwa ghadhabu. Ni mwenye hii sura iliyo mlangoni alimtazama tena mlinzi bila kumjibu, pengine hata kumtaka radhi lakini alimcheka tena, kisha akawatazama wakina Bertha walipoketi akacheka.
Oooooh…..Nmekuangalia nlitegemea ungecheka na wewe unashangaa….ha haaaaa leo huna kicheko? Karibu ndani mwaya” Alijirekebisha na kujichekesha kiaina. Mgeni akaingia moja kwa moja na kujikaribisha kwenye kijikiti kilichokuwemo pembeni mwa meza ndogo kwenye chumba hiki kidogo. Mgongoni alikua na kibegi ambacho hakukitua bali aliketi kikiwa mgongoni. Mgeni aliangaza macho huku na huku kama mtu atafutae kitu fulani, akapepesa macho pembe zote za chumba kisha akainuka ghafla akaongea;
“Wanachuo bana sijui wakoje yani mtu anakuja anakaribishwa ndani hata hapokewi mzig….” Kabla hajamalizia akakatishwa na mwenyeji.
“Acha visa vyako we si umekuja mpaka ndani, ningekubamba njiani ndo ungelalamika, haya niambie umeniletea nini maana hutui hata mzigo mwenzangu” Bertha alisaili.
“Wanachuo bana mi nimekuja na mabomu, kwanza kumbuka hunifahamu hata jina mi mwenyewe sikufahamu na kama ningepotea huku umezima simu sijui ningeuliza nani” Mgeni alichombeza zaidi.
“Haya mi naitwa Bertha au kifupi Betty wewe je” Bertha alijitambulisha.
“Hahaaa hapo sawa, mi naitwaaaa aaghhh ngoja kwanza jina langu gumu kutamka ngoja nikalete msosi najua hata we hujala mgonjwa haulizwi uji, nikirudi nikala kidogo ntapata nguvu ya kutamka” Aliongea hayo huku akinyanyuka akatua kibegi kwenye meza akaondoka nyuma akimwacha Betty hana mbavu alicheka sana mpaka machozi yakamtoka lakini mgeni huyu tangu afike hajaonekana kucheka wala kutabasamu.
          Betty alibaki na furaha akimwaza mgeni huyu mcheshi, mgeni mwenye visa alikumbuka kisa cha mlinzi kumpiga kofi mgeni akageuka badala ya kukasirika akaishia kucheka. Mlinzi alipokasirika zaidi mgeni huyu alicheka zaidi.
Itaendelea.................

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2