SIMULIZI-NIKICHEKA UTALIA!! SEHEMU YA 06


Baada ya kufukuzwa darasani Riziki na Jovin waliketi katika viti vilivyokua nje ya darasa wakitafakari hali iliyotokea darasani.
“Sasa kama katutimua hapa tujue wazi ndio mwanzo wa kufeli kabisa, maana testi, na majaribio hatuwezi kufanya” Jovin aliongea
“Achana nae tutajua la kufanya, hana ishu wala nini. Hivi ulikua unasema ulianza mwaka pamoja na sisi?” Riziki akaongea.
“Hapana, inaonekana hukuwa darasani juzi Ijumaa, mimi nilikua nasoma kozi ya Ualimu (BAED) nimeamua kubadilisha kozi nimekuja BAMC sikuipenda kozi ya ualimu mi sipendi kufundisha” Jovin alielezea.
“ahaa sawa, Mbona ni vigumu kubadilisha kozi we uliwezaje, na mbona kuna vitu vilishakupita unawezaje kukava vyote maana ni miezi mitatu tangu tuanze” Riziki akahoji.

“Hiyo rahisi mbona, ni namna ntakavyopanga ratiba zangu na kuongea na walimu ntaweza bila shida” Jovin akaelezea.
          Baada ya hapo walipeana namba za simu wakawa marafiki waliokutana kwenye shida ya kufukuzwa darasani. Wakatawanyika kila mtu akaenda njia zake. Riziki aliingia katika kigari chake akaamua kuondoka zake nyumbani. Ni dhahiri hakutaka kusoma vipindi vilivyosalia aliamua siku ndio imeisha. Alifika kwenye makazi yake akatafakari tukio la darasani na rafiki yake huyu mpya Jovin waliyefahamiana baada ya kukutana nje walipotolewa darasani.
          Katika maisha ya binadamu kuna marafiki na maadui, kwa mtazamo wa kawaida unaweza kudhani rafiki wa kweli ni huyu uliye nae mnafurahi pamoja na kuambizana siri na mambo yenu mbali mbali lakini huwezi kumjua kiundani kwene nafsi yake yukoje huenda ndie adui yako namba moja na anatumia wasaa huo kukuangamiza taratibu, ni kweli mnashirikiana kwa kila jambo mnacheka na kufurahi lakini laiti ungejua kajivika mwanya huo kufanikisha mambo mengne ungelimkataa tangu zamani kabla ya kesho kujuta. Kwa upande mwingnie unayemwona ni adui yako namba moja usishangae anapogeuka na kuwa rafiki yako kipenzi, zamani ulidhani anafanya mambo kukukomoa na kukuangamiza kumbe alifanya kukuokoa na kukulinda lakini ulifungwa na upofu wa akili yako katika kung'amua. Kinyume huwa kweli na kweli hugeuka kinyume.
          Riziki aliamka masaa mawili baadae akiwa na njaa kali huku kichwa kikiwa kimevurugwa na mawazo lukuki.Tumbo liliunguruma kutoa madai.
 “Hivi ingekuaje kama kila kiungo cha mwili kingefanya madai kama lilivyo tumbo? Hakika haliachi kudai na kila siku lazima ufanye jitihada za kuhakikisha Tumbo limeridhika, sio hiari kulipa lakini ni lazima kufanya hivyo, ingawa naweza kujitahidi angalau ukakwepa kulipa kwa siku moja lakini adhabu yake ntaiona na ni vigumu kuendelea kufanya ivyo kwa siku mbili au tatu zaidi, kwa juhudi zote za kila siku za kazi na masomo lakini tunajitahidi kuliridhisha tumbo, lakini  kama tumbo lingekua halidai namaanisha kungekua hakuna kula ingekuaje???”
Aliamka akaenda kujitafutia chochote.
                                            ▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄
          Wiki ilipita ni kipindi cha katikati ya wiki mwalimu wa somo la uhariri wa habari (News Editing) ambae ni Profesa Mfumbuka alikua amesafiri na hivyo ilitegemewa msaidizi wake Mr Shawo angekaimu nafasi yake kufundisha lakini alikua hajafika bado hivyo kiongozi wa darasa aliamua kutumia nafasi hii kujadili hili na lile.
“paa paa paaa, Jamani tusikilizane kidogo” CR alipiga makofi kuweka hali ya utulivu darasani kisha akaendelea.
          “Jamani tukamilishe michango kwa ambao hatujachanga, tumchangie mwenzetu hali yake bado si nzuri, jana nilipata taarifa anatakiwa afanyiwe upasuaji wa kuunga mifupa, alipigwa  X-Ray imeonesha amevunjika mivupa na mingine imekaa upande hivyo gharama ni kubwa tujitahidi jamani.” CR aliongea kisha akaendelea.
“Ngoja niende kwa H.O.D nikaulize nijue kama kipindi kipo au hakipo.” Cr Zawadi Chama alimaliza. H.O.D(Head of Department) ikiwa na maana ya mkuu wa idara. Katika nyanja za elimu kunakua na idara mbali mbali mfano idara ya sayansi, uchumi na nyinginezo.
          Ni siku nne zimepita baada ya mwanachuo mmojawapo wa darasa hili Sarapia Pelemunge apate ajali mbaya ya pikipiki maeneo ya karibu na chuo. Aliumia sana na tangu hapo alikua katika hospitali kubwa ya Bugando hajiwezi hali yake ikiwa ni mbaya.
          Baada ya muda CR alirudi kutoa taarifa kwa darasa. Aliwapa ishara ya kutulia kumsikiliza kisha akaanza kuongea.
“Jamani nimetoka kwa H.O.D. kuulizia, majibu niliyopewa ni kwamba Mr shawo hamna taarifa zake na kwenye simu hapatikani kwa siku tano sasa, uongozi wa chuo uliwasiliana na familia yake nao wanamtafuta hamna mwenye taarifa zake na wala hawajui yupo wapi, wanasema wameshatoa taarifa mpaka polisi mpaka jana uongozi wa chuo umefuatilia bado hajaonekana hivyo kipindi cha leo hakitakuepo.” CR alimaliza wanachuo walitawanyika lakini wakiwa na maswali na mada nyingi zisizo na majibu.
                                                   ▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄
          Ndani ya ofisi ya idara polisi kitengo maalum cha upelelezi kanda ya ziwa ambayo makao makuu yapo Mkoa wa Mwanza katika ofisi moja aliketi mwanamama mmoja mnene ambae kwa mbali sura ikianza kuonyesha makunyanzi ishara tosha uzee unaanza kubisha hodi. Mwanamama huyu kwa cheo ni  DCP (Depurty Commissioner of Police). DCP Mary Timkii alikua amesimama dirishani akiangalia madhari ya jiji la Mwanza ndani ya ofisi yake iliyo ndani ya jengo hili refu. Ni punde kwenye taarifa ya habari amesikia habari ya kutoonekana kwa mmoja wa wakufunzi wa chuoni hapa kwa takriban wiki nzima sasa. Mwanamama huyu hupendelea sana kusikiliza Redio Saut Fm ambayo inamilikiwa na Chuo kikuu SAUT. Sababu za kupendelea kuisikiliza wakati kuna redio nyingi sana jijini mwanza ni mpangilio mzuri wa vipindi hasa vya habari na matukio. Kwa mtu wa kazi na wadhifa kama wake hupenda kupata habari kuhusu jamii na nini kinachoendelea katika jamii. Pia hupendelea kuisikiliza idhaa hii sababu humpa habari nyingi za kanda ya ziwa hasa mwanza ambapo ni eneo lake la kazi.
          Katika kipindi kifupi kilichopita amesikia matukio na mikasa mingi ikitokea katika Chuo hiki. Katika muda wake wa kazi akiwa Mwanza hakuwahi kushuhudia visa mfululizo kama hivi.Ingawa yalikua matukio yenye sababu na visababishi vilikuepo lakini alibaki na utata wa matukio kuwa mengi kwa kipindi kifupi tu.
          Alishatuma kijana wake wa kazi ni kama wiki mbili zilizopita ajaribu kunusa hili na lile labda kuna kinachoendelea. Kijana aliyetumwa alikua kwenye mazoezi ya kazi tu hakua tayari ameshafuzu na alifanya hivyo kwa hisia ndogo tu kuamini ni matukio ya kawaida na kumpa kijana wake kazi ya kufanya kwa lolote atakaloambulia hata kama akikosa lakini kumpima kama anafaa kwa kazi. Aliamini msemo panapofuka moshi pana moto.
                                      ▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄▀▄
          Waliketi kwenye viti vilivyo karibu kabisa na maji lakini sehemu yenye mwavuli wa kukinga jua na palipotengenezwa kuzuia maji kuwagusa. Riziki na Jovin waliendelea kupiga stori za hapa na pale huku wakifurahia upepo mwanana na mvumo wa mawimbi katika ufukwe huu mdogo wa ziwa Victoria sehemu ijulikanayo kama Tamala.
          Ni siku ya Jumapili Riziki alipompitia Jovin katika chumba chake kilichopo maeneo ya nyumba za wahadhiri. Ni chumba cha peke yake na anaishi mwenyewe. Kwakua Riziki alikua na gari aliamua ampitie wakapunge upepo kidogo.
“Hivi kaka wewe ni mtu wa wapi, ujue hata sikusomi fresh, hata hujawai kunipeleka unapoishi kila siku nakuona unatokea mkolani” Jovin aliendeleza mazungumzo.
“Ohoo hilo mbona suala dogo, mie kwetu Moshi Mchaga pori kabisa yani” Riziki alijibu kimasihara kidogo.
“Hapo sawa, mimi kwetu ni Mkoa wa Mara natokea wilaya ya bunda, kwetu asili yetu sime, mapanga, visu ukija mgeni jipange kuzoea mazingira” Jovin aliyaendeleza
“Huko mkae wenyewe, lakini hata mimi mikiki naimudu” Riziki akaongeza.
“Ungeimudu ile siku tunatimuliwa na Shawo ungemchapa hata kangumi basi……..eheeee halafu nimekumbuka kuna jambo linanitatiza kidogo” Jovin alitoa ukakasi rohoni mwake.
“Kwanini likutatize we ropoka pointi” Riziki akaruhusu.
“kwenye ile siku tunatolewa class mbona baada ya yule dada sjui anaitwa nani yule alipoongea karaha we ulicheka na ticha mwenyewe ulimcheka wakati hakukua na cha kuchekesha?”
“Kuna mtu anacheka bila sababu? Ujue kila mtu ana hisia zake wewe linaweza kukukera mimi likanifurahisha” Riziki akajibu.
“Halafu baada ya lile tukio siku mbili baadae yule msichana alipata ajali mbaya isitoshe Mr Shawo mpaka leo hajulikani alipo,… Unahusika nini mwanangu….. “ Jovin alimchimba kiaina.
Riziki alimtazama Jovin kwa muda kidogo kisha akawaza jambo halafu akasita kidogo kisha akasema
“aaaahh…. Hamna bana mbona matukio ya kawaida tu” alijibu.
“we ni best yangu bana usinbanie, hata mi nlifurahi ujue yule dada anajiona sana, isitoshe huyu ticha angetuharibia nimegee mwanangu kama kuna kinachoendelea, itakua siri yetu sisi wanaume bana” Jovin alikandamiza maelezo ya kina.
“acha hizo bana, hamna jipya” Alisema Riziki.
“Sio ishu we kuna kitu unanificha, mi mwenyewe kuna ticha anazingua nataka nimfanyizie mwenyewe utaona lakini siri yako, sasa siku ile ulikua unacheka nini kama huhusiki mwanangu”
“Tulia ntakutafta wikiendi ijayo tutachonga kila kitu” Riziki akajibu
“acha izo nidokezee basi kama unahusika wewe angalau niridhike” Jovin alizidi kusaili.
“Mi sihusiki wangu wikiendi ntakwambia bana”
                           XXXXXXXXXXXXXXXXXXX
 ITAENDELEA

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2