RAIS MAGUFULI AAGIZA MACHINGA WASIONDOLEWE JIJINI MWANZA

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli amemuagiza Waziri na Katibu Mkuu katika Ofisi ya Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) kusitisha mara moja utekelezaji wa zoezi la kuwaondoa wafanyabiashara wadogo maarufu kwa jina la Machinga katika Jiji la Mwanza mpaka hapo mamlaka husika itakapokamilisha maandalizi ya maeneo watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha wamachinga wenyewe.
Rais Magufuli akiwa na Makamu wa Rais Mhe. Samia Suluhu Hassan ametoa agizo hilo leo tarehe 06 Desemba, 2016 Ikulu Jijini Dar es Salaam huku akionya kuwa kiongozi yeyote ambaye hayupo tayari kutekeleza agizo hilo aachie ngazi.

“Kumeibuka tabia ya Wakuu wa Mikoa, Wakuu wa Wilaya na Wakurugenzi kuwafukuza Wamachinga bila utaratibu wowote wa wapi wanawapeleka na wakati mwingine wanapelekwa maeneo ya mbali ambayo hayafai hata kwa kufanya biashara, hili jambo sio sawa hata kidogo.

“Sipendi Wamachinga wafanye biashara kwenye hifadhi ya barabara lakini hakuna sheria katika nchi hii inayosema mtu wa biashara ndogondogo au Mmachinga hatakiwi kukaa katikati ya mji, tukianza kwenda kwenye utaratibu wa namna hiyo maana yake tunaanza kutengeneza  madaraja ya Watanzania, kwamba kuna Watanzania fulani wa daraja fulani wanapaswa kukaa katikati ya mji na Watanzania wa daraja fulani hawatakiwi kukaa katikati ya mji, huo sio mwelekeo wetu na wala Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi ambayo mimi na wewe (Makamu wa Rais) tulipita kuinadi, haisemi tutengeneze madaraja ya watu wanaostahili kukaa mjini na wengine hawastahili kukaa mjini, sasa nimeona hili nilizungumze na nataka kulirudia kwa mara ya mwisho” amesema Rais Magufuli.

Dkt. Magufuli ameelekeza kuwa Wamachinga waliondolewa katika maeneo yao Jijini Mwanza waachwe waendelee na shughuli zao mpaka hapo Halmashauri ya Jiji la Mwanza itakapokamilisha maandalizi ya mahali watakapohamishiwa na kwa kuwashirikisha Wamachinga wenyewe.

“Narudia na hii ni mara ya mwisho, kawaambieni hata Wamachinga wa Mwanza warudi kwenye maeneo yao mpaka watakapowatengenezea utaratibu mzuri, Kigamboni hapa palikuwa na wamachinga eneo fulani wamehama vizuri kweli, wakatengenezewa miundo mbinu yao katika soko lao na sasa hivi wanafanya kazi vizuri, na waliwashirikisha viongozi wa Wamachinga, lakini Mwanza imekuwa ni amri tu na wengine wanatumia hata msemo wa Hapa Kazi Tu, mimi sikusema msemo wa Hapa Kazi Tu wa namna hiyo, nadhani mmenielewa” amesisitiza Rais Magufuli alipokuwa akiwaekeleza Naibu Waziri wa TAMISEMI Mhe. Suleiman Jafo na Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Mussa Iyombe.

Wakati huo huo, Rais Magufuli ameagiza Wizara ya Nishati na Madini kusitisha mara moja zoezi la kuwaondoa wachimbaji wadogo katika Kijiji cha Nyaligongo kilichopo katika Kata ya Mwakitolyo Mkoani Shinyanga na badala yake wachimbaji hao waachwe waendelee na shughuli zao, na leseni ya mwekezaji anayedai eneo hilo ni lake aondolewe.

“Wale waliofukuzwa Shinyanga wabaki palepale, kama ni leseni ya huyo mwekezaji ifutwe, Mhe. Makamu wa Rais fuatilia hili, mweleze Waziri wa Nishati na Madini, waache kufukuza wananchi hovyohovyo, wale wanapata riziki yao, wanasomesha watoto wao lakini wanafukuzwa tu.

“Na hizi ndio ajira zenyewe, tulisema tunatengeneza ajira, wewe mwekezaji ni mmoja unakwenda kuwafukuza watu 5,000? haiwezekani na wala haingii akilini” amesisitiza Rais Magufuli.

Rais Magufuli amekemea vitendo vya wawekezaji wakubwa kupewa maeneo ambayo wachimbaji wadogo wanaendesha shughuli zao tena kwa mtindo kwa kutengeneza nyaraka zinaonesha mwekezaji husika alipewa eneo hilo kabla ya wachimbaji wadogo na kusisitiza kuwa mchezo huo hautavumiliwa.

Hata hivyo Rais Magufuli amesema maagizo yake hayana maana kuwa Wamachinga na Wachimbaji wadogo waendeshe shughuli zao kwa kuvunja sheria bali wazingatie sheria na Mamlaka zisiwanyanyase watu wanyonge.

Gerson Msigwa
Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, IKULU
Dar es Salaam

6 Desemba 2016

0/Post a Comment/Comments

Previous Post Next Post

Ad

Ads1

Sponsor Ad

Ads2